RC DKT NCHIMBI: MADIWANI ACHENI KUWACHEKEA WATUMISHI, "WAMESABABISHA HATI CHAFU MIAKA MITATU MFULULIZO”

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akizungumza na madiwani na wakuu wa idara wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba wakati wa Baraza Maalumu la kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali.
Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba wakifuatilia hoja wakati wa Baraza Maalumu la kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali. 
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt Angelina M Lutambi (wa kwanza kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Iramba Emmanuel Luhahula wakiandika baadhi ya maoni na maelekezo katika Baraza Maalumu la kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Iramba Linno Mwageni akimshukuru Dkt Nchimbi kwa kuwakumbusha kuwajibika katika Baraza Maalumu la kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali.  
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akimkabidhi Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Simioni Tiyosera baadhi ya mashuka yaliyotolewa na Rais Magufuli kwa ajili ya halmashauri yake. 
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Iramba Boniphace Richard akimshukuru Rais Magufuli kwa kuwapatia mashuka, vitanda na magodoro ambayo yamesaidia kupunguza uhaba wa vifaa hivyo na kuwaboreshea mazingira ya kufanya kazi.

MADIWANI wametakiwa kuacha mzaha wa kuwachekea na kuwaendekeza watumishi ambao wamesababisha Halmashauri ya Wilaya ya Iramba kupata hati chafu ya Mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za Serikali katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi ameyasema hayo jana wakati wa baraza maalum la madiwani la kujadili hoja 122 za mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za serikali katika halmashauri hiyo.

Dkt Nchimbi amewaambia madiwani kuwa wao ndio wazawa na ndio wawakilishi wa wananchi hivyo wanapozembea kuwasimamia na kuwabana watumishi ili wafuate kanuni, sheria na miongozo, watakaoumia ni wananchi wao pamoja na halmashauri yao kukosa ruzuku ya serikali.

“Madiwani acheni mzaha wa kuwachekea hawa watumishi, unapoona hoja ujue kiwanda ni watumishi, lakini mmepata hati chafu miaka mitatu mfululizo hamshtuki tu kuna watu wana wanawahujumu? Au mnaweza kujiendesha bila ya ruzuku ya serikali? Semeni leo? Wananchi wamewaamini hebu watumikieni ipasavyo,” amesema Dkt Nchimbi.

Ameongeza kuwa halmashauri inapoendelea kupata hati chafu hiyo ni sifa mbaya kwao na hata kwa mkoa mzima kwakuwa watendaji wa ngazi za mkoani mpaka halmashauri wanaonekana wameshindwa kutekeleza wajibu wao vema.

Dkt Nchimbi amesema madiwani waweke utaratibu ili wakuu wa idara waliothibitishwa wabaki katika halmashauri hiyo kwa kipindi kirefu kwakuwa wamekuwa wakithibitishwa kisha wanahama jambo linalowafanya wakose wakuu wa idara wa kutosha na kubaki na wanaokaimu.

“Kuna baadhi ya watumishi wanaharibu tu kwakuwa wanajua watahama hapo, lakini ninyi madiwani na wananachi hamtaweza kuhama hapo ndio kwenu hivyo basi wekeni utaratibu tu, mkuu wa idara akithibitishwa abaki hapo kwa muda awatumikie wananchi au akitaka kuhama basi atafute wa kubadilishana naye”, amesisitiza.

Aidha Dkt Nchimbi amewataka watumishi kuacha uzembe, watumie fursa zilizopo katika kujiongezea kipato lakini wasifanye biashara na halmashauri huku akiwashauri kuwasikiliza viongozi wa dini ambao wanawahimiza uadilifu na uchapa kazi.

Naye Mkaguzi wa Nje wa Hesabu za Serikali Annamary Kakunguru amesema baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo wamekuwa wazito katika kujibu hoja, kufuta hoja pamoja na kufuata maoni ya mkaguzi wa Nje hivyo kuisababishia halmashauri kuwa na hoja nyingi zinazodumu kwa muda mrefu.

Kakunguru amesema watumishi wanapaswa kubadilika na kuwa na utendaji mzuri pamoja na kupeana ushirikiano ili kwa pamoja waweze kufuta hoja na kuweka mikakati mizuri ya kuzuia hoja.

Pia Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt Angelina M Lutambi amewaasa watumishi kufanya kazi kwa kufuata miongozo, sheria na kanuni ili kuepuka kutengeza hoja huku wakuu wa idara wanaokaimu wakitakiwa kufanya kazi kwa bidii ili utendaji wao uonekane.

Lutambi ameongeza kuwa utendaji wa ushirikiano ndio utaifanya halmashaur hiyo kusonga mbele huku akiwaeleza kuwa hoja za mkaguzi wa hesabu za serikali zinawakumbusha kuongeza uadilifu na usimamizi wa fedha na shughuli za serikali.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Iramba Linno Mwageni amemshukuru Dkt Nchimbi kwa kuwakumbusha kuwajibika ili waendane na kasi ya awamu ya tano ya hapa kazi tu.

Mwageni amemweleza Mkuu huyo kuwa siku nyingine asisite kuwaonya pale wanapoenda tofauti huku akiahidi kwa niaba ya watumishi kubadilika na kuongeza bidii katika utendaji na usimamizi wao.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amekabidhi kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli vitanda vya kuzalia vitatu, vya kawaida 20, mashuka hamsini na magodoro hamsini  vyenye thamani ya shilingi milioni 25 kwa hospitali na vituo vya kutolea huduma za afya Wilayani humo.

Dkt Nchimbi amesema Rais Magufuli ameonyesha upendo wake kwa wana Iramba hivyo wasiogope kutumia huduma za afya katika vituo vya serikali kwa kuwa sasa huduma zimeboreshwa, huku akiwaasa wakunga wa jadi wawaache wajawazito wakajifungulie hospitali na vituo vya afya.

Ameongeza kuwa watoa huduma na madaktari sasa wameboreshewa mazingira ya kufanyia kazi hiyo wanapaswa kutoa huduma kwa uadilifu mkubwa na kwa bidii.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Iramba Boniphace Richard amemshukuru Rais Magufuli kwakuwa walikuwa na upungufu wa mashuka 400, ambapo jitihada za Rais zimewapatia mashuka 150 huku wakipanga kununua mashuka 200 kwa mapato ya ndani.

Jitihada za Rais Magufuli zimeungwa mkono na Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Katibu Tawala wa Mkoa, Mwenyekiti wa halmashauri na madiwani, Mkurugenzi wa halmashauri na watumishi ambao kwa pamoja wamechangia mashuka 96, magodoro matano na pesa shilingi elfu hamsini.

MKUU WA WILAYA MKALAMA, AWATAKA BODABODA KUCHANGAMKIA FURSA NMB

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama mkoani Singida, Eng. Jackson Makata (mwenye miwani) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Tawi la Benki ya NMB Mkalama. Wengine ni maofisa wa NMB na wageni waalikwa wakishuhudia tukio hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama mkoani Singida, Eng.Jackson Makata akizindua rasmi tawi la NMB wilayani humo.
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama mkoani Singida, Eng. Jackson Makata (mwenye miwani) pamoja na maofisa wa NMB wakifurahia mara baada ya kukata utepe kuashiria uzinduzi wa Tawi la Benki ya NMB Mkalama.

MKUU wa Wilaya ya Mkalama mkoani Singida, Eng. Jackson Jonasi Masaka, amewaagiza madereva wa boda boda kuanzisha na kusajili vikundi vya ujasiriamali, ili kujijengea mazingira mazuri kupata mikopo toka tawi la NMB benki, lililozinduliwa wilayani humo. Eng. Masaka ametoa agizo hilo juzi wakati akizungumza kwenye uzinduzi rasmi wa tawi la NMB tawi la Mkalama, lililopo katika makao makuu ya wilaya hiyo, Nduguti.
Alisema kufunguliwa kwa tawi hilo kumesogeza karibu zaidi huduma mbalimbali ikiwemo ya mikopo zinazotolewa na NMB benki, kwa wakazi wa wilaya hiyo. Akifafanua, alisema huko nyuma wakazi wa wilaya hiyo pamoja na watumishi wa umma, iliwabidi kufuata huduma za kibenki Singida mjini, umbali wa kilometa 140 kwenda na kurundi.
“Kwa hiyo ninyi madereva wa bodaboda, NMB imesongeza huduma...huu ni wakati muafaka kuboresha shughuli zenu. Msilale changamkeni, jiungeni kwenye vikundi vilivyosajiliwa muweze kupata mikopo itakayokuza mitaji yenu. Mjue tu kwamba dereva mmoja mmoja ni ngumu mno kupata mkopo kwenye taasisi za kifedha”, alisema mkuu huyo wa wilaya. Eng. Makata pia ametumia fursa hiyo kuwahamasisha baba/mama lishe, wauza chips na wajasiriamali mbalimbali wakiwemo wadogo, kuchangamkia mikopo kupitia akaunti ya ‘FANIKIWA’.
“Niipongeze NMB benki kwa kubuni bidhaa hii ya akaunti ya FANIKIWA. Kupitia akaunti hii ya FANIKIWA, wajasiriamali niliowataja hapo juu, wataweza kupata mikopo kati ya shilingi laki tano na milioni 30. Nasisitiza tumieni fursa hizi zilizosongewa karibu zaidi na NMB, ili mkuze mitaji yenu iweze kukidhi mahitaji ya wakati wa sasa,” alisema.
Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa wilaya ameishukru na kuipongeza NMB benki kwa msaada wake wa vitanda 15, magodoro 15, vitanda viwili vya kujifungulia akina mama wajawazito na mashine mbili za kupimia mapigo ya moyo.
“Msaada huu wenye thamani ya shilingi milioni 10 ambao umetolewa kwa kituo cha afya, vitunzwe na kulindwa vizuri ili viweze kutumika kwa kipindi kirefu,” alisema Eng. Makata. Awali meneja wa uhusiano wa biashara kati ya serikali na benki NMB kanda ya kati, Yasin Mfinanga, alisema msaada huo ni mwendelezo wa NMB katika kumuunga mkono Rais Dk. Magufuki kuboresha sekta ya afya.
“Kila mwaka baada ya kutoa gharama zote za uendeshaji, benki yetu huwa inatenga asilimia moja ya faida, kwa ajili ya kutoa misaada inayolenga sekta ya afya na elimu. Agizo la rais Magufuli la kuchangia madawati katika shule za msingi na sekondari, NMB ilishiriki kikamilifu,” alisema Mfinanga kwa kujiamini.
Mfinanga alitumia fursa hiyo kuwataka wakazi wa kanda ya kati, kuacha kabisa utamaduni wa kutunza fedha kwenye simu zao za viganjani na badala yake wazitunze kwenye mabenki ikiwemo ya NMB. Akisisitiza, alisema fedha zinazotunzwa kwenye simu za viganjani usalama wake ni mdogo mno, ikilinanishwa na zile zinazotunzwa kwenye mabenki ya kuaminika.
“Fedha hizi zilizopo kwenye simu za viganjani na wakazi wa kanda ya kati wakijitokeza kwa wingi kuweka fedha benki, hatua hiyo itachangia NMB benki kuwa na uwezo mkubwa katika kutoa mikopo. Aidha, hatua hii itachangia benki kupunguza riba zinazokatwa kwenye gharama za uendeshaji,” amesisitiza zaidi.
Wakati huo huo.mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mkalama, James Mkwega, alisema kufunguliwa kwa tawi la NMB tawi la Mkalama, pamoja na mambo mengine, kutachochea ukuaji wa uchumi. “Binafsi nimefarijika mno…na naipongeza NMB benki kufungua tawi hapa kwetu Nduguti makao makuu ya wilaya ya Mkalama. Huko nyuma tulilazimika kufuata huduma za kibenki Singida mjini kilometa 140 kwenda na kurudi. Madhara yake yalikuwa makubwa mno,” alisema na kuongeza;
“Watumishi wa umma wakiwemo walimu nao wametaabika sana katika kufuata mishahara yao New Kiomboi wilaya ya Iramba umbali wa likometa 90. Hapo ilikuwa kabla wilaya Iramba yaijagawanywa na kuzaa wilaya ya Mkalama. Nakumbuka baadhi ya walimu walikuwa wanatumia usafiri wa baiskeli, wakifika msitu wa Gumanga, walikuwa wakiporwa mishahara yao na majambazi,”
Mwenyekiti huyo ambaye ni diwani (CCM) kata ya Gumanga, alisema kuwa kwa sasa hayo yote yatabaki kuwa histori, baada ya NMB kufungua tawi hilo.

SINGIDA UNITED YAZIDI KUJIIMARISHA, YAINGIA MKATABA WA MILIONI 250 NA KAMPUNI YA YARA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 



 Mkurugenzi Mkuu  wa kampuni ya YARA Alexander Macedo akizungumza na waandishi wa habari wakati wa utiaji saini wa makubaliano ya udhamini wa mwaka mmoja kwa timu ya Singida United wenye thamani ya kiasi cha Milioni 250.
  Mkurugenzi Mtendaji wa timu ya Singida United Festo Sanga akizungumza na waandishi wa habari wakati wa utiaji saini wa makubaliano ya udhamini wa mwaka mmoja kwa timu ya Singida United wenye thamani ya kiasi cha Milioni 250.

Wachezaji wa Simgida United wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya YARA Alexande Macedo (kulia) kocha mkuu wa timu ya Singida United Hans Van De Pluijm (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Singida United Festo Sanga wakati wa utiaji saini wa makubaliano ya udhamini wa mwaka mmoja kwa timu ya Singida United wenye thamani ya kiasi cha Milioni 250.

Mkurugenzi Mtendaji wa timu ya Singida United Festo Sanga  (kushoto) na  Mkurugenzi Mkuu  wa kampuni ya YARA Alexander Macedo wakitia saini karatasi ya makubaliano ya udhamini wa timu ya Singida wenye thamani ya Milioni 250.
Mkurugenzi Mtendaji wa timu ya Singida United Festo Sanga  (kushoto) na  Mkurugenzi Mkuu  wa kampuni ya YARA Alexander Macedo wakibadilishana nyaraka za mkataba wa udhamini wa mwaka mmoja wenye thamani ya kiasi cha Milioni 250.

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.

Timu ya Singida United imeingia mkataba wa mwaka mmoja wenye thamani ya kiasi cha Milioni 250  na kampuni ya uzalishaji mbolea ya YARA ikiwa ni katika mikakati ya kuongeza vyanzo vya mapato ya timu hiyo.

Mkataba huo umesainiwa leo mbele ya waandishi wa habari ukishuhudiwa na kocha mkuu wa timu ya Singida United Hans Van De Pluijm.

Akizungumza kabka ya utiaji saini wa Mkurugenzi Mtendaji wa timu ya Singida United Festo Sanga amesema kuwa mkataba huu wa mwaka mmoja utaizidi kmuimarisha timu yao katika masuala ya kifedha na zaidi wataendelea kuwakaribisha makampuni mengine kwa ajili ya kufanya nao kazi.

Sanga amesema kuwa, katika moja ya makubaliano yaop wameshapata shamba la ekari 10000 kwa ajili ya kilimo cha Mahindi na zitasimamiwa na kamouni ya YARA ikiwemo uwekezaji wa mazao hayo ndani na nje ya nchi.

Pia mbali na hilo, Singida United wameingua makubaliano ya kibiashara ya kusambaza bidhaa za YARA ndani ya nchi ikiwemo na kuzitangaza.

Kwa upande wa kampuni ya YARA,  Mkurugenzi Mkuu Alexander Macedo amesema kuwa wameamua kuidhamini timu ya Singida United kwani wameona ni timu nzuri na hata nembo ya timu yao ina ua la Alizeti ambalo linatumika sana kwa ajili ya utengenezaji mafuta hayo.

Macedo mwenyeji wa Brazili amesema watashirikiana na timu yya Singida ili waweze kuendeleza kilimo cha Mahindi nchini pampja na kuhakikisha wanawapatia wataalamu wazui wa soka kwa ajili ya mafunzo mbalimbali.

IGP SIRRO AMALIZA ZIARA YAKE MIKOA YA KANDA YA ZIWA KWA KISHINDO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.


Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro, akizungumza na baadhi wa  Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoa wa Singida, wakati alipofika katika Ofisi ya Mkuu wa mkoa huo kwa lengo la kujitambulisha na kuzungumza na askari na maofisa wa Jeshi hilo pamoja na kujua changamoto wanazokutananazo wakitekeleza majukumu yao. Picha na Jeshi la Polisi. 

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro, akizungumza na askari na maofisa wa Jeshi hilo na kuwataka wafanyekazi kwa kutenda haki na kusimamia misingi ya sheria na taratibu, IGP Sirro yupo mkoani Singida kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kujitambulisha na kuzungumza na askari na kujua changamoto wanazokutananazo wakitekeleza majukumu yao. Picha na Jeshi la Polisi. 
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro, akizungumza na kikosi cha Polisi wanawake baada ya kukagua gwaride la heshima lililoandaliwa kwa ajili yake alipowasili mkoani Singida, kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kujitambulisha na kuzungumza na askari na kujua changamoto wanazokutananazo wakitekeleza majukumu yao. Picha na Jeshi la Polisi. 


Na Jeshi la Polisi Nchini

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro, amemaliza ziara yake katika mikoa ya kanda ya ziwa pamoja na mkoa wa Singida, huku akiacha morali kwa watendaji wa Jeshi hilo hatua ambayo italiwezesha ieshi hilo kufanyakazi zake kwa weledi katika kukabiliana na matishio ya uhalifu na wahalifu.

IGP Sirro, amefanya ziara hiyo ikiwa ni mkakati wake aliojiwekea tangu alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Jeshi hilo kwa lengo la kujitambulisha na kuzungumza na askari na maofisa ili kujua namna wanavyotekeleza majukumu yao ya kazi za Polisi.

Katika mazungumzo yake IGP Sirro, amewataka askari na maofisa kutimiza wajibu wao kwa kutenda haki na bila uwoga wala kumuonea mtu muhali jambo ambalo litarahisisha upatikanaji wa taarifa za uhalifu na wahalifu katika jamii.

Hata hivyo, katika mabaraza ya kuzungumza na askari na maofisa baadhi ya hoja kadhaa ziliibuliwa kwa baadhi ya askari waliopata nafasi ya kutoa mawazo yao, ambapo IGP Sirro aliahidi kuzishughulikia mapema ili kuzidisha morari katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Aidha, katika ziara yake IGP Sirro, alipata fursa ya kukutanana Wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama ya mkoa huku masuala kadhaa ya kiusalama na mbinu na mikakati ikijadiliwa katika kamati hizo na kuahidi kutoa ushirikiano utakaowezesha kukabiliana na matishio mbalimbali ya kiuhalifu.

IGP SIRRO ALIPONGEZA JESHI LA POLISI MKOA WA SINGIDA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

1
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro akipiga saluti wakati wa paredi ya polisi iliyoandaliwa lililoandaliwa  kwa ajili yake kulikagua mapema leo kwenye viwanja vya kambi ya  FFU mjini hapa.

2
Mkuu wa Jeshi la Polisi  nchini IGP Simon Sirro akikagua baadhi ya askari wa jeshi la polisi  mjini  Singida leo piga saluti wakati wa paredi ya polisi iliyoandaliwa lililoandaliwa  kwa ajili yake kulikagua.
3
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada kukagua askari polisi waliokuwa kwenye  paredi kwenye viwanja vya kambi ya  FFU mjini hapa.
………………………….
Picha/Habari na Gasper Andrew.
Mkuu wa Jeshi la polisi nchini (IGP), Simon Sirro amelipongeza jeshi la polisi Mkoani Singida kwa juhudi zake za kupunguza matukio ya uhalifu yakiwemo ya utekeji wa magari kwa kiwango kikumbwa.
IGP  Siro ametoa pongezi hizo  leo asubuhi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari  kweye viwanja vya kambi  ya kikosi  cha kuzuia fujo (FFU) mjini  hapa.
Amesema matukio ya uhalifu mbalimbali mkoani Singida yamekupungua kwa kiwango kikubwa kwa  sasa, ikilinganishwa na miaka ya  nyuma.
“Hatua hii  inachangia  uwepo  wa amani  na utulivu kwa  wananchi  wa  mkoa wa Singida hivyo  kutoa fursa   kuweza  kujiletea maendeleo yao ya mkoa na  taifa   kwa ujumla” amesema.
IGP Siro  amesema  mafanikio  hayo yamechangiwa   na wananchi kwa kiwanngo  kikubwa  kwa kutoa ushuirikiano  kwa jeshi la polisi. 
Akifafanua amesema wananchi wamekuwa wakitoa  taarifa sahihi na kwa  wakati kwa jeshi la polisi  pindi wanapobaini  dalili  ama  matukio ya kihalifu.
“Kwa sasa kwa kweli  wananchi hata ninyi waandishi  wa habari mnatupa  ushirikiano  mzuri sana. Ushirikiano huu unachangia  kazi zetu kuwa nyepesi  na za mafanikio makubwa. Sasa  hivi  kule Kibiti mkoani Pwani, wananchi wanatusaidia mno taarifa  zinazohusu  mauaji ya watu  wasiokuwa  na hatia”, amefafanua zaidi.
IGP Siro amesema kwa sasa Tanzania inaonewa wivu na nchi jirani kwa namna tulivyo dhibiti matukio ya kihalifu na kupelekea nchi kuendelea kudumisha amani na utulivu.
Wakati huo huo, Mkuu huyo  wa jeshi la polisi ametumia fursa hiyo  kuwaomba wananchi  waendelee  kushirikiana na jeshi hilo, kufichua  baadhi ya watu wanaojihusisha na matukio mbalimbali   ya kihalifu ili waweze kuchukulia  hatua stahiki.

RAIS DKT. MAGUFULI AFUNGUA BARABARA YA ITIGI-MANYONI-CHAYA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akikaribishwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi alipowasili Mkoani Singida eneo la Itigi ili kufungua Barabara ya Itigi -Manyoni -Chaya yenye urefu wa kilometa 89.5 iliyojengwa na Serikali kwa asilimia mia moja. Mheshimiwa Rais alikuwa akitokea kwenye ziara ya siku tatu Mkoni Tabora kupitia Singida akiwa njiani kuelekea  Dodoma  Julai 25,2017.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli (wa pili kushoto) na viongozi wengine wa mkoa wa Singida wakiondoa kitambaa kuashiria kufunguliwa rasmi kwa  barabara ya Itigi -Manyoni -Chaya yenye urefu wa kilometa 89.5 iliyojengwa kwa fedha za Serikali kwa  asilimia mia moja.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Viongozi wengine wa Mkoa wa Singida na Tabora Wakikata Utepe kama ishara ya kufunguliwa Rasmi kwa  Barabara ya Itigi -Manyoni -Chaya yenye urefu wa kilometa 89.5 iliyojengwa kwa fedha za Serikali kwa  asilimia mia moja.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kulia akiteta jambo na Mwakilishi wa Kampuni ya PowerChina International Group Limited nchini Bw. Wang Chao wakati wa Ufunguzi wa  Barabara ya Itigi -Manyoni -Chaya yenye urefu wa kilometa 89.5 iliyojengwa kwa fedha za Serikali kwa  asilimia mia moja.
  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwashukuru na kuwasalimia kwa kupunga mikono kwa wananchi wa Itigi na Manyoni walioshiriki na Kushuhudia Ufunguzi wa  Barabara ya Itigi -Manyoni -Chaya yenye urefu wa kilometa 89.5 iliyojengwa kwa fedha za Serikali kwa  asilimia mia moja.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwaaga wananchi wa Itigi na Manyoni walioshuhudia Ufunguzi wa  Barabara ya Itigi -Manyoni -Chaya 
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwahutubia Wananchi Kijiji Cha Tula Uyui Mkoani Tabora waliojitokeza Barabarani Kumsalimia akiwa njiani kuelekea Mkoani Dodoma akitokea kwenye ziara ya siku tatu Mkoni Tabora Julai 25,2017.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisisitiza jambo akiwa njiani katika moja ya mikutano ya barabarani kwa  waliojitokeza  Kumsalimia akiwa njiani kuelekea Mkoani Dodoma akitokea kwenye ziara ya siku tatu Mkoni Tabora Julai 25,2017.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia wananchi wa Itigi na Manyoni wakati wa Ufunguzi wa  Barabara ya Itigi -Manyoni -Chaya yenye urefu wa kilometa 89.5 iliyojengwa kwa fedha za Serikali kwa  asilimia mia moja.
Wananchi wa Itigi na Manyoni wakimsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwatubia kwenye Ufunguzi wa  Barabara ya Itigi -Manyoni -Chaya yenye urefu wa kilometa 89.5 iliyojengwa kwa fedha za Serikali kwa  asilimia mia moja. 
Picha zote na IKULU


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwapungia mkono wakazi wa Itigi mara baada ya kuzungumza nao na kuzindua barabara Manyoni-Itigi-Chaya, ambapo pamoja na mambo mengine ameagiza ujenzi wa barabara ya Chaya-Nyaua yenye kilomita 85 na ujenzi uanze ndani ya siku 45 ili barabara hiyo ikamilike kwa kiwango cha lami.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na umati wa wakazi wa Itigi waliojitokeza kumlaki na kushuhudia uzinduzi wa barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya, Rais Magufuli amewataka wana Itigi kutumia fursa ya kuwa jirani na Makao makuu ya nchi kwa kufanya kazi kwa bidii na kuzalisha bidhaa ambazo zitauzwa huko Dodoma.
 Umati wa wakazi wa Itigi waliojitokeza kumlaki Rais Magufuli na kushuhudia uzinduzi wa barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya, wakazi hao wamempongeza na kumshukuru Rais Magufuli kwa kuwajengea barabara hiyo ambayo ni muhimu kwa kuwaunganisha na mikoa ya Tabora na Kigoma.
 Sehemu ya barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya ambayo imezinduliwa leo na Rais Magufuli, Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 89.3 kwa kiwango cha lami imefungua fursa ya usafirishaji kwa urahisi kutoka kanda ya Kati yaani Singida na Dodoma Kuelekea mikoa ya Tabora na Kigoma hadi nchi za jirani za Burundi na Kongo.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Makame Mbarawa akimkaribisha Rais Magufuli azungumze na wananchi wa Itigi, ambapo amesema barabara ya Manyoni Itigi Chaya imegharimu shilingi bilioni 114.692 na kiunganishi cha Mikoa ya Singida, Tabora na Kigoma kuelekea Makao makuu ya Nchi yaani Dodoma.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiambatana na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi kwenye eneo la mkutano wa hadhara mara baada ya kuwasili eneo la Njiapanda Itigi, alipozungumza na wananchi wa eneo hilo na kuzindua barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya.
 Umati wa wakazi wa Itigi waliojitokeza kumlaki Rais Magufuli na kushuhudia uzinduzi wa barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya, wakazi hao wamempongeza na kumshukuru Rais Magufuli kwa kuwajengea barabara hiyo ambayo ni muhimu kwa kuwaunganisha na mikoa ya Tabora na Kigoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amkimsikiliza kwa makini Mhandisi wa TANROADS mkoa wa Singida Leonard Kapongo mapema leo. Katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Itigi, Rais Magufuli amemuagiza Meneja huyo na Wizara ya ujenzi kupitia upya gharama za ujenzi wa barabara ya Mkiwa-Itigi itakayoelekea Makongorosi yenye urefu wa kilomita 57 ambapo gharama za ujenzi wa barabara hiyo ni bilioni 104

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO AZINDUA BODI MPYA YA USHAURI YA WIZARA - TAASISI YA UHASIBU TANZANIA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akizungumza muda mfupi kabla hajazindua Bodi mpya ya Ushauri ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA). Uzinduzi huo umefanyika hivi karibuni katika kampasi ya TIA tawi la Singida mjini.
 Mwenyekiti wa Bodi mpya ya Ushauri ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Said Chiguma akizungumza kwenye hafla fupi ya uzinduzi wa Bodi mpya ya Ushauri ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA). Uzinduzi huo umefanyika hivi karibuni katika kampasi ya TIA tawi la Singida mjini.
 Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Joseph Kihanda, akitoa nasaha zake kwenye hafla ya uzinduzi wa Bodi mpya ya Ushauri ya Taasisi hiyo. Uzinduzi huo umefanyika hivi karibuni katika kampasi ya TIA tawi la Singida mjini.
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa  Bodi mpya ya Ushauri ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA). Uzinduzi huo umefanyika hivi karibuni katika kampasi ya TIA Singida mjini. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Bodi mpya ya Ushauri TIA Said Chiguma na Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA Joseph Kihanda na kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhe. Elias Tarimo na Mjumbe wa Bodi Dkt. Leonada.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango  Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amezindua Bodi mpya ya Ushauri ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) kwa lengo la kuimarisha ufanisi wa Taasisi  na uangalizi wa karibu.

Akizungumza hivi karibuni wakati wa uzinduzi huo uliofanyika  Taasisi ya Uhasibu Tanzania kampasi ya Singida  Dkt. Kijaji amesema Bodi hiyo itamsaidia Waziri wa Fedha na Mipango kupata ushauri wa kitaalam  na hatimaye kutoa maamuzi  yenye tija kwa Taasisi na Taifa kwa ujumla.

 "Bodi hii ya Ushauri inategemewa kutoa mchango  wa mawazo na  kitaalam yanayohusu uendeshaji  na uboreshaji wa  Taasisi yetu ya TIA ili kuendana na mabadiliko yanayoendelea duniani katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, kiteknolojia, kisiasa na kijamii", amesema Dkt. Kijaji.

Dkt. Kijaji ameongeza kuwa Bodi hiyo ina wajibu wa kujua ubora wa wanafunzi wanaohitimu katika chuo hicho ikiwa ni pamoja na ubora wa vyeti vyao kuendana na uwezo wao wa kufanya kazi katika fani walizosomea na kukabiliana na changamoto kwenye maeneo ya kazi.

Nae Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania Said Chiguma amesema Taasisi hiyo inakabiliwa na changamoto ya uchache wa miundombinu kama vile kumbi za mihadhala, madarasa, maktaba na maabara za kompyuta ambavyo ni nyenzo muhimu katika utoaji wa elimu iliyo bora.

Chiguma amesema ili kupunguza changamoto hizo, Taasisi inajitahidi kutenga fedha inazozikusanya ili kukarabati na kujenga majengo mbalimbali kwa ajili ya kuboresha elimu na kuongeza uwezo wa kudahili wanafunzi wengi zaidi.

Taasisi ya Uhasibu Tanzania ni chuo cha Serikali ambacho kinatoa mafunzo katika fani za Uhasibu, Ununuzi na Ugavi, Usimamizi wa Biashara, Uongozi wa Rasilimali Watu, Masoko na Uhusiano wa Umma pamoja na Uhasibu wa Fedha za Umma kuanzia ngazi ya Astashahada (Certificate), Stashada (Diploma)  na Shahada (Degree).
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa