Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akizungumza na madiwani na wakuu
wa idara wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba wakati wa Baraza Maalumu la
kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali.
Baadhi
ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba wakifuatilia hoja wakati
wa Baraza Maalumu la kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za
Serikali.
Katibu
Tawala Mkoa wa Singida Dkt Angelina M Lutambi (wa kwanza kushoto) na
Mkuu wa Wilaya ya Iramba Emmanuel Luhahula wakiandika baadhi ya maoni na
maelekezo katika Baraza Maalumu la kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti
wa Hesabu za Serikali.
Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Iramba Linno Mwageni akimshukuru Dkt Nchimbi kwa
kuwakumbusha kuwajibika katika Baraza Maalumu la kujadili hoja za
Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali.
Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akimkabidhi Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Simioni Tiyosera baadhi ya mashuka
yaliyotolewa na Rais Magufuli kwa ajili ya halmashauri yake.
Mganga
Mkuu wa Wilaya ya Iramba Boniphace Richard akimshukuru Rais Magufuli
kwa kuwapatia mashuka, vitanda na magodoro ambayo yamesaidia kupunguza
uhaba wa vifaa hivyo na kuwaboreshea mazingira ya kufanya kazi.
MADIWANI
wametakiwa kuacha mzaha wa kuwachekea na kuwaendekeza watumishi ambao
wamesababisha Halmashauri ya Wilaya ya Iramba kupata hati chafu ya
Mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za Serikali katika kipindi cha miaka
mitatu mfululizo.
Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi ameyasema hayo jana wakati wa
baraza maalum la madiwani la kujadili hoja 122 za mkaguzi na mdhibiti wa
hesabu za serikali katika halmashauri hiyo.
Dkt
Nchimbi amewaambia madiwani kuwa wao ndio wazawa na ndio wawakilishi wa
wananchi hivyo wanapozembea kuwasimamia na kuwabana watumishi ili
wafuate kanuni, sheria na miongozo, watakaoumia ni wananchi wao pamoja
na halmashauri yao kukosa ruzuku ya serikali.
“Madiwani
acheni mzaha wa kuwachekea hawa watumishi, unapoona hoja ujue kiwanda
ni watumishi, lakini mmepata hati chafu miaka mitatu mfululizo hamshtuki
tu kuna watu wana wanawahujumu? Au mnaweza kujiendesha bila ya ruzuku
ya serikali? Semeni leo? Wananchi wamewaamini hebu watumikieni
ipasavyo,” amesema Dkt Nchimbi.
Ameongeza
kuwa halmashauri inapoendelea kupata hati chafu hiyo ni sifa mbaya kwao
na hata kwa mkoa mzima kwakuwa watendaji wa ngazi za mkoani mpaka
halmashauri wanaonekana wameshindwa kutekeleza wajibu wao vema.
Dkt
Nchimbi amesema madiwani waweke utaratibu ili wakuu wa idara
waliothibitishwa wabaki katika halmashauri hiyo kwa kipindi kirefu
kwakuwa wamekuwa wakithibitishwa kisha wanahama jambo linalowafanya
wakose wakuu wa idara wa kutosha na kubaki na wanaokaimu.
“Kuna
baadhi ya watumishi wanaharibu tu kwakuwa wanajua watahama hapo, lakini
ninyi madiwani na wananachi hamtaweza kuhama hapo ndio kwenu hivyo basi
wekeni utaratibu tu, mkuu wa idara akithibitishwa abaki hapo kwa muda
awatumikie wananchi au akitaka kuhama basi atafute wa kubadilishana
naye”, amesisitiza.
Aidha
Dkt Nchimbi amewataka watumishi kuacha uzembe, watumie fursa zilizopo
katika kujiongezea kipato lakini wasifanye biashara na halmashauri huku
akiwashauri kuwasikiliza viongozi wa dini ambao wanawahimiza uadilifu na
uchapa kazi.
Naye
Mkaguzi wa Nje wa Hesabu za Serikali Annamary Kakunguru amesema baadhi
ya watumishi wa halmashauri hiyo wamekuwa wazito katika kujibu hoja,
kufuta hoja pamoja na kufuata maoni ya mkaguzi wa Nje hivyo
kuisababishia halmashauri kuwa na hoja nyingi zinazodumu kwa muda mrefu.
Kakunguru
amesema watumishi wanapaswa kubadilika na kuwa na utendaji mzuri pamoja
na kupeana ushirikiano ili kwa pamoja waweze kufuta hoja na kuweka
mikakati mizuri ya kuzuia hoja.
Pia
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt Angelina M Lutambi amewaasa watumishi
kufanya kazi kwa kufuata miongozo, sheria na kanuni ili kuepuka
kutengeza hoja huku wakuu wa idara wanaokaimu wakitakiwa kufanya kazi
kwa bidii ili utendaji wao uonekane.
Lutambi
ameongeza kuwa utendaji wa ushirikiano ndio utaifanya halmashaur hiyo
kusonga mbele huku akiwaeleza kuwa hoja za mkaguzi wa hesabu za serikali
zinawakumbusha kuongeza uadilifu na usimamizi wa fedha na shughuli za
serikali.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Iramba Linno Mwageni
amemshukuru Dkt Nchimbi kwa kuwakumbusha kuwajibika ili waendane na kasi
ya awamu ya tano ya hapa kazi tu.
Mwageni
amemweleza Mkuu huyo kuwa siku nyingine asisite kuwaonya pale
wanapoenda tofauti huku akiahidi kwa niaba ya watumishi kubadilika na
kuongeza bidii katika utendaji na usimamizi wao.
Wakati
huo huo Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amekabidhi kwa niaba
ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli
vitanda vya kuzalia vitatu, vya kawaida 20, mashuka hamsini na magodoro
hamsini vyenye thamani ya shilingi milioni 25 kwa hospitali na vituo
vya kutolea huduma za afya Wilayani humo.
Dkt
Nchimbi amesema Rais Magufuli ameonyesha upendo wake kwa wana Iramba
hivyo wasiogope kutumia huduma za afya katika vituo vya serikali kwa
kuwa sasa huduma zimeboreshwa, huku akiwaasa wakunga wa jadi wawaache
wajawazito wakajifungulie hospitali na vituo vya afya.
Ameongeza
kuwa watoa huduma na madaktari sasa wameboreshewa mazingira ya kufanyia
kazi hiyo wanapaswa kutoa huduma kwa uadilifu mkubwa na kwa bidii.
Mganga
Mkuu wa Wilaya ya Iramba Boniphace Richard amemshukuru Rais Magufuli
kwakuwa walikuwa na upungufu wa mashuka 400, ambapo jitihada za Rais
zimewapatia mashuka 150 huku wakipanga kununua mashuka 200 kwa mapato ya
ndani.
Jitihada
za Rais Magufuli zimeungwa mkono na Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya,
Katibu Tawala wa Mkoa, Mwenyekiti wa halmashauri na madiwani, Mkurugenzi
wa halmashauri na watumishi ambao kwa pamoja wamechangia mashuka 96,
magodoro matano na pesa shilingi elfu hamsini.
0 comments:
Post a Comment