Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Ukibahatika kuutembelea Mkoa wa Singida na kurejesha kumbukumbu
zako miaka 10 nyuma unaweza usiamini yanayotokea hivi sasa kwenye mkoa
huo. Unaweza kushangaa na kujiuliza maswali mengi jinsi mkoa huo
unavyobadilika na kuvutia watu wengi sasa.
Singida sasa wamejenga nyumba za kisasa, barabara
za lami na wakazi wake wameongeza uzalishaji wa zao la alizeti, karanga
na vitunguu na hivyo kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja.
Uzalishaji wa mazao ya biashara; alizeti, pamba na
vutungu umeongezeka kwa kasi ukilinganisha na miaka minane iliyopita
kwa mfano, mwaka 2007 Mkoa wa Singida ulivuna tani 28, 000 za alizeti
wakati mwaka 2012 Singida ilivuna tani 202,000 za zao hilo.
Ukuaji na kuwapo kwa mabadiliko ya kiuchumi katika
mkoa huo hasa kuongezeka kwa pato la mtu mmoja mmoja kunachangiwa na
shughuli za kilimo, ufugaji na ujenzi wa barabara ya lami ambayo
imekamilika mwaka 2007.
“Pato la mtu mmoja, mkoani Singida, kabla ya mwaka
2007 lilikuwa Sh280,000 kwa mwaka, sasa ni Sh650,000 kwa mwaka,”
anasema Liana Hassan, Katibu Tawala wa mkoa huo.
Mabadiliko yalivyotokea
Mabadiliko hayo hajatokea kirahisi kwenye mkoa huo
bali mambo mengi yamebalika kutokana na juhudi za Mkuu wa Mkoa wa
Singida, Dk. Parseko Kone na Benki ya Dunia (WB) ambayo imetoa mkopo wa
Sh44.506 bilioni kwa Serikali ya Mkoa wa Singida.
Mradi wa ujenzi wa kilometa 109 ya barabara
kuanzia Singida mpaka Shelui kupitia Mlima wa Sekenke, uko chini ya
Central Transport Corridor Project (CTCP). Wakala wa Barabara nchini
(Tanroads), Mhandisi Yustaki Kangolle anasema Barabara ya Singida hadi
Shelui imejengwa katika awamu tatu; kuanzia Singida hadi Iguguno, awamu
ya pili Iguguno hadi Sekenke na Sekenke hadi Shelui.
Ujenzi wa barabara hiyo umewavutia wakazi wa mkoa
huo kuongeza bidii katika kilimo cha alizeti na kununua na kuanzisha
viwanda vidogo vya kukamua mafuta kutokana na fursa ya kusafirisha kwa
wingi mafuta hayo jijini Dar es Salaam, Arusha na mkoani Kilimanjaro.
Mwitikio wa wananchi wa Singida kupenda kulima na
kutekeleza maagizo ya Serikali ya Mkoa wa Singida chini Dk. Kone
wameleta mabadiliko kilimo cha alizeti na kusababisha kuongezeka kwa
viwanda vya kukamua mafuta.
Kutokana na juhudi za wakulima, Ofisa Mtendaji wa
TCCIA wa mkoa huo, Calvent Nkulu anabainisha kuwa miaka saba iliyopita
kulikuwa na viwanda 50 vya kukamua mafuta, lakini sasa kuna viwanda 120
mkoani Singida.
“Kutokana na kipato cha wananchi kuongezeka,
tumewahamasisha wajenge nyumba za kisasa badala ya nyumba za tembe.
Wananchi wanapata urahisi wa kusafirisha vifaa vya ujenzi kutoka Singida
mjini hadi vijijini,” anaeleza mkuu wa mkoa huo.
Mazao ya biashara yanasafirishwa hadi nchi za jirani; Rwanda,
Kenya, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na mazao ya
chakula kwa mfano, samaki, maparachichi yanasafirishwa na kuuzwa jijini
Dar es Salaam kutoka mkoani Mwanza na Rwanda.
“Biashara imekua hapa Singida, wafanyabiashara
wanatoka Kenya kwa ajili ya kununua vitungu na kuku, Singida ya leo siyo
ile ya zamani,” anasema Julius Madebwe ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa
Kitengo cha Biashara mkoani Singida.
Mkoa huo sasa umekuwa na maendeleo makubwa ya
shughuli za ujenzi wa nyumba za kisasa kutokana na kuwapo kwa barabara
hiyo na kukua kwa shughuli za kilimo baada ya kuwapo kwa mvua za
kutosha.
Biashara ya mafuta ya alizeti imepata soko kubwa
nchini na kuwavutia watu wengi kuifanya akiwamo Mhandisi Mstaafu wa
Wakala wa Barabara nchini, John Shailla ambaye ananunua mbegu za alizeti
Wilaya ya Bariadi na kuzikamua kwenye mashine yake na kuuza kwa walaji.
Jambo kubwa la kujivunia kwa wakazi wa Singida ni
bidhaa mbalimbali zinazosafirishwa kutoka nchini Rwanda kwa mfano,
maparachichi na maharagwe hivi sasa yanauzwa sokoni mkoani Singida
tofauti na awali magari ya mizigo yalikuwa yakikwama njiani.
Baada ya kukamilika kwa barabara hiyo, mkazi wa
Shelui katika mkoa huo, Mohamed Hassani anasema kuwa ajali zimeongezeka
kwenye Mlima wa Sekenke na baadhi ya wananchi wameiomba Serikali
iwaruhusu madereva watumie barabara ya zamani wakati wa kuteremka mlima
huo.
Baadhi ya wakazi wa Kata ya Iguguno, Misigiri,
Ulemo na Kijiji cha Kyengege akiwamo dereva wa malori ya mizigo, Henry
Michael na mkulima wa Kata ya Iguguno, Hatibu Sambai wanapendekeza
kuwekwa kwa alama za barabarani katika maeneo muhimu ya pembezoni mwa
barabara ambako kuna shule, hospitali na miji midogo ili kupunguza
ajali.
Wakazi wa wengi wa kata hizo wameshangazwa na
barabara hiyo kuharibika mapema na kuwa mashimo mengi huku wakiitupia
lawama Tanroads kwa kuitengeneza barabara hiyo chini ya kiwango na
kutoweka mitaro ya kupitisha maji wala barabara za waendesha baiskeli,
pikipiki na barabara ya waenda kwa miguu.
“Matatizo ni mengi kwenye barabara hii, haina
mitaro ya kupitisha maji na matokeo yake maji yanaingia kwenye makazi ya
watu,” anabainisha Nikodemmonti Maigai, mkazi wa Kijiji Kyengege.
Hata hivyo mkazi wa kijiji hicho, Josephat Mginza
anawalaumu Tanroads kwa kuwa hawawashirikishi wakazi wa Singida wakati
wa kutengeneza barabara na matokeo yake kusababisha wananchi wengi
kulalamika kutokana na kupoteza fursa za biashara zilizokuwapo pembezoni
mwa barabara.
Kutokana na kuwapo kwa kasoro hizo Meneja wa
Tanroads mkoani Singida, Mhandisi Kangole alikiri kwamba barabara hiyo
imejengwa chini ya kiwango kwa kuwa fedha walizopata hazikutosheleza
kujenga barabara ya kiwango cha juu.
“Barabara hii imejengwa kwa kiwango cha TLC 10- ni
aina ya barabara ya kiwango cha chini. Sasa tunafikiria kuweka lami juu
ya hii ya sasa na kilometa moja ya barabara ya milimita 50 inaweza
kugharimu Sh600 mpaka Sh800 milioni,” anabainisha Mhandisi Kangole.
Kutowekwa kwa alama za barabarani na vibao, Mhandisi Yonennes
Mbegalo anabainisha kwamba ni tatizo linalosababishwa na baadhi wananchi
ambao wanaviiba na hivyo amewataka kuvilinda vibao hivyo.
Wakati Mhandisi Kangole akisema hayo Mhandisi
Masige Matari anatoa sababu za kuharibika kwa barabara hiyo kwamba wingi
wa magari ya mizigo umesababisha kuwapo mashimo.
“Kabla ya Barabara ya Singida hadi Shelui kuwekwa
lami, malori ya mizigo 117 yalikuwa yakitumia barabara hii kwa siku, leo
yanapita malori 1,135 kwa siku kwenda Rwanda, DRC, Kagera na Mwanza.
Baadhi ya wananchi wanapongeza jitihada hizo
wakisema kuwa ikiwa harakati za maendeleo zitaendelea mkoa huo unaweza
kuwa na maendeleo ya kasi zaidi.
Chanzo;mwananchi