Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WANANCHI zaidi ya 3,000 wa Kijiji cha Ng’ang’uli, Kata ya Ulemo,
wilayani Iramba, Mkoa wa Singida, wamenufaika na huduma ya maji safi
na salama baada ya mradi wa maji ya bomba kukamilika kujengwa na kuanza
kutumika.
Mjumbe wa Kamati ya Mradi wa Maji ya Kijiji hicho, Paulo Saida,
aliyasema hayo hivi karibuni katika taarifa ya utekelezaji wa mradi huo
wakati wa uzinduzi wa bomba la maji uliofanyika katika kijiji hicho.
Alisema lengo la mradi huo ulioanza kutekelezwa Agosti 15, 2013 na
kukamilika Februari 15, mwaka huu, ni kuboresha afya za wananchi 3,669
kwa kuwapatia huduma ya maji safi na salama karibu na maeneo wanayoishi
na kwa njia endelevu.
Saida alisema historia ya mradi huo ilitokana na wananchi wa kijiji
hicho kuuchagua mpango huo uwe kipaumbele chao kutokana na shida ya maji
iliyokuwa ikiwakabili.
Kwa mujibu wa mjumbe huyo, gharama za mradi huo wa bomba la maji ni
sh 312,945,550; zikiwemo fedha za nje sh 307,245,550 na michango ya
wananchi sh 5,700,000.
“Shughuli zilizofanyika kutokana na fedha hizo ni pamoja na kujenga
tenki lenye ujazo wa lita 45,000, kujenga nyumba moja ya mtambo wa
kusukuma maji, kujenga vituo 11 vya kuchotea maji, kujenga malambo
mawili ya kunyweshea maji mifugo, kujenga choo bora kimoja, kujenga
tenki la kuvuna maji ya mvua lenye ujazo wa lita 5,000 na kufyatua
mtungi wa kuvuna maji ya mvua wenye ujazo wa lita 1,000.
“Pia zimetumika kujenga tenki la lita 3,000, kuchimba mitaro na
kufunga bomba lenye urefu wa mita 11,487, kununua na kufunga mtambo wa
kusukuma maji, kuwapatia semina na mafunzo wananchi kuunda na kusajili
vikundi vya watumia maji kwenye vituo na jumuiya ya watumiaji wa maji
(Juhudi Cowsco),” alifafanua mjumbe huyo.
Akizungumzia faida za mradi huo, alisema ni kupungua kwa magonjwa
yanayotokana na maji yasiyo salama, muda wa shughuli za kiuchumi
utaongezeka na hatimaye kipato kitaongezeka kwa wakazi wa kijiji hicho.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Halima Mpeta,
katika taarifa yake ya utekelezaji wa Programu ya Maji na Usafi wa
Mazingira, alisema lengo la programu hiyo ni kusambaza huduma ya maji
safi na salama kwa wakazi 77,015 wakiwemo 45,470 wa Wilaya ya Mkalama
na 31,545 wa Iramba ifikapo mwaka 2015.
Utekelezji wa Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira awamu ya kwanza
katika Halmashauri ya Wilaya ya Iramba ulianza mwaka 2008/2009 ambapo
vijiji 13 vya Iramba na Mkalama viliingia, wakati huo ilikuwa
ikitambulika kama Wilaya moja ya Iramba.
Chanzo:Tanzani Daima
0 comments:
Post a Comment