Home » » AUNGUZWA NA UJI KISA WIVU WA MAPENZI

AUNGUZWA NA UJI KISA WIVU WA MAPENZI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
MSICHANA Jackline Lasway maarufu kwa jina la Pendo, mkazi wa eneo la Minga Manispaa ya Singida, amenusurika kifo baada ya kumwagiwa uji wa moto na mke wa tajiri wake wa dukani kutokana na kile kinachosadikiwa ni wivu wa kimapenzi.
Pendo amelazwa wodi namba mbili hospitali ya Mkoa wa Singida, huku akiwa na majeraha ya kuungua sehemu ya sikio la upande wa kulia na mgongoni.
Akizungumza kwa taabu katika wodi hiyo, Pendo alisema tukio hilo limetokea jana mchana wakati akiwa dukani kwa bosi wake aliyemtaja kwa jina la Charles Kamnde ‘Frarucha’.
Alisema akiwa anaendelea na kazi yake ya kuuza bidhaa mbalimbali dukani hapo, ghafla alitokea mke wa bosi wake akiwa na chupa yenye uji wa moto na kutaka kumwagia usoni.
Alisema aligeuka ili uji ule usimwagigikie usoni na ndipo ulimuunguza sikio la kulia na mgongoni, ambako baada ya mke wa bosi wake kumkosa uso, alitoa kisu kutaka kumchoma kifuani.
“Mimi sikuwa na ugomvi naye wala sijui chanzo cha yeye kufika dukani na kufanya hili tukio, maana kama ni kazi mi nafanya kulingana na maelekezo kutoka kwa bosi wangu Chale,” alisema.
Alisema katika purukushani za kujiokoa asichomwe kisu, alifanikiwa kumkamata mkono mwanamke huyo na kupiga kelele na watu walifika kumwokoa.
Hata hivyo, alisema alichukuliwa na bosi wake hadi kituo cha polisi mjini Singida na kupewa PF 3 kwa ajili ya matibabu na kuletwa katika hospitali hiyo, ambako amelazwa huku akiwa na majeraha makubwa mgongoni.
Muuguzi wa zamu katika wodi namba mbili ya wanawake, Anna Cyprian, alisema hali ya mgonjwa huyo inaendelea vizuri na anaendea kupatiwa matibabu ya majeraha ya moto aliyopata.
Kwa upande wake mmiliki wa duka hilo, Frarucha, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba hayuko tayari kulizungumzia, kwani maelezo aliyotoa binti huyo yanajitosheleza.
Baadhi ya kina mama waliohojiwa kuhusiana na tukio hilo, wameonesha masikitiko yao kutokana na hatua ya mwananmke huyo kumwagia uji msichana huyo.
Amina Ramadhani, alisema hicho ni kitendo cha kinyama kwa binti mdogo kama huyo na kwamba kama aliona kuna mahusiano ya kimapenzi na mumewe, angetumia busara na kumwondoa dukani na siyo kumuunguza kwa uji wa moto.
Veronica Masawe, alisema amesikitishwa na tukio hilo na kuwa hakiendani na haki za binadamu, kwa kuwa ni kumdhalilisha msichana huyo ambaye alikuwa akifanya kazi kwa ajili ya kujipatia kipato.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Geofrey Kamwela, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba, wanamshikilia mtuhumiwa kwa mahojiano na baada ya upelelezi kukamilika atafikishwa mahakamani
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa