Home » » HATARI HII: Binti wa kazi ajeruhiwa vibaya kwa kumwagiwa uji wa moto na mke wa bosi wake, kisa wivu wa kimapenzi

HATARI HII: Binti wa kazi ajeruhiwa vibaya kwa kumwagiwa uji wa moto na mke wa bosi wake, kisa wivu wa kimapenzi


jeraha
Msichana Jackline Lasway akiwa amelazwa katika wodi ya kina mama namba mbili katika hospitali ya Mkoa wa Singida baada ya kujeruhiwa kwa kumwagiwa uji wa moto wakati akiwa dukani kwa bosi wake eneo la soko kuu Manispaa ya Singida.
Na Mwandishi Wetu , Singida.
Msichana mmoja mkazi wa eneo la Minga Manispaa ya Singida amenusurika kifo baada ya kumwagiwa uji wa moto na mke wa tajiri wake wa dukani  kutokana na kile kinachosadikiwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.
Msichana huyo Jackline Lasway maarufu kwa jina la Pendo amelazwa wodi namba mbili katika hospitali ya Mkoa wa Singida, huku akiwa na majeraha ya moto  sehemu ya sikio la upande wa kulia na mgongoni.
Akizungumza kwa taabu katika wodi hiyo, Pendo alisema kuwa tukio hilo limetokea juzi mchana wakati akiwa dukani kwa bosi wake aliyemtaja kwa jina la Charles Kamnde “Frarucha”.
Alisema akiwa anaendelea na kazi yake ya kuuza bidhaa mbalimbali dukani hapo gafla alitokea mke wa bosi wake akiwa na chupa yenye uji wa moto na kumtaka kumwagia usoni.
majeruhi
Hili ni jeraha ambalo Jackline ameumia.
Alisema aligeuka ili uji ule usimwagikie usoni na ndipo ulimuunguza sikio la kulia na mgongoni ambapo baada ya mke wa bosi wake kumkosa uso alitoa kisu kutaka kumchoma kifuani.
“Mimi sikua na ugomvi nae wala sijui chanzo cha yeye kufika dukani na kufanya hili tukio, maana kama ni kazi mi nafanya kulingana na maelekezo kutoka kwa bosi wangu Chale.” Alisema.
Alisema katika kurupushani za kujiokoa asichomwe kisu hicho alifanikiwa kumkamata mkono mwanamke huo na kupiga kelele ambapo watu walifika na kumwokoa.
Hata hivyo alisema alichukuliwa na bosi wake hadi kituo cha polisi mjini Singida na kupewa PF 3 kwa ajili ya matibabu na kuletwa katika hospitali hiyo ambako amelazwa huku akiwa na majeraha makubwa mgongoni.
waandishi
Waandishi wa habari wakimchukua maelezo msichana huyo.
Muuguzi wa zamu katika wodi namba mbili ya wanawake, Anna Sprian alisema hali ya mgonjwa huyo inaendelea vizuri, na anaendelea kupatiwa matibabu ya majeraha ya moto aliyopata.
Kwa upande wake mmiliki wa duka hilo Chale Kamnde ‘Frarucha’ alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa hayuko tayari kulizungumzia kwani maelezo aliyotoa binti huyo yanajitosheleza.
Baadhi wa kinamama waliohojiwa kuhusiana na tukio hilo wameonesha masikitiko yao kutokana na hatua ya mwanamke huyo kumwagia uji msichana huyo.
akilia
Msichana Jackline akilia wakati akiwaonesha waandishi wa habari jeraha alilomwagiwa uji na mke wa bosi wake.
Amina Ramadhani alisema hicho ni kitendo cha kinyama kwa binti mdogo kama huyo na kwamba kama aliona kuna mahusiano ya kimapenzi na mumewe angetumia busara na kumwondoa dukani na sio kumuunguza kwa uji wa moto.
Veronika Masawe alisema amesikitishwa na tukio hilo na kusema kuwa hakiendani na haki za binadamu kwa kuwa ni kumdhalilisha msichana huyo ambaye alikuwa akifanya kazi kwa ajili ya kujipatia kipato.
Kamanda wa polisi Mkoani Singida, Geofrey Kamwela amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanamshikilia mtuhumiwa kwa mahojiano baada ya upelelezi kukamilika atafikishwa mahakamani.
muuguzi
Muuguzi wa zamu katika wodi namba mbili Anna Sprian akizelelezea maendeleo ya Jackline.
kinamama
Hawa ni majirani waliofika kumjulia hali majeruhi Jackline katika hospitali ya mkoa wakihojiwa na waandishi wa habari.
wodini
Jack akiwa wodini kabla ya kuzungumza na vyombo vya habari.
hospitli
Kibao cha hospitali ya mkoa wa Singida.
kibao
Kibao cha wodi namba mbili hospitali ya mkoa wa Singida.(PICHA ZOTE NA KAMERA YA MOblog SINGIDA).
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa