Home » » MO awashtaki CCM Singida kwa Kinana

MO awashtaki CCM Singida kwa Kinana

kapambala
Katibu wa CCM Mkoa wa Singida Naomi Kapambala aaizungumza na waanndishi wa habari juu ya ufafanuzi wa maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo.
Na Hillary Shoo, Singida
Mbunge wa Jimbo la Singida mjini (CCM), Mohammed Dewji ameulalamikia uongozi wa Chama chake Mkoa wa Singida kwa kitendo cha kuchelewesha mchakato wa kumalizia ujenzi wa Uwanja wa michezo Namfua ikiwa ni moja ya ahadi zake alizotoa kwa wananchi wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.
Kuchelewa huko kuanza kwa mchakato wa ukarabati na uwekaji wa nyasi za bandia kwenye uwanja huo imeelezwa ni kutokana na urasimu na maslahi binafsi miongozi mwa viongozi wa CCM Mkoa wa Singida.
Katika barua yake ya Julai 31 mwaka huu kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Dewji amedai kuwa kwa kiasi kikubwa ameweza kutekeleza Ilani ya Uchaguzi kwa vipindi vyote viwili pamoja na ahadi zake binafsi, isipokuwa ahadi ya kumalizia ujenzi wa michezo Namfua.
Katika barua hiyo, ambayo pia ameinakili kwa Rais Jakaya Kikwete, Katibu Baraza la wadhamini CCM Taifa, Katibu wa Uchumi na Fedha na Katibu wa CCM mkoa wa Singida, Dewji amedai kuwa kila alipotaka kufanya hivyo alipata vikwazo kutoka kwa viongozi wa CCM mkoa wa Singida.
sehemu ya uwanja
Katikati ya kiwanja chenyewe.
Amesema kuwa matayarisho yote muhimu kuhusiana na ujenzi huo yapo tayari, ikiwa ni pamoja na kuwepo dola za kimarekani 880,000 (sawa na sh bilioni 1.46) ambazo kwa kushirikiana na Rais Kikwete aliweza kuzipata kutoka Makampuni ya Airtel Tanzania na Mohammed Ent (T) Ltd.
Dewji amesema wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 yeye pamoja na Raisi Jakaya Kikwete walitoa ahadi ya kukarabati na kuweka nyasi za bandia
kwenye uwanja huo unaomilikiwa na chama cha mapinduzi CCM.
uwanja
Hili ni jukwaa kuu la uwanja wa Namfua unaomilikiwa na CCM Mkoa wa Singida.
“Baada ya uchaguzi sote wawili tulishinda na sasa tunatumikia wananchi, na kwa kiasi kikubwa tumefanikiwa kutekeleza ilani ya uchaguzi kwa vipindi vyote viwili, pamoja na ahadi zetu binafsi, lakini ahadi tuliyotoa ya ukarabati wa uwanja mpaka sasa hatujafanikiwa kuitekeleza. Alisem MO na kuongeza
Dewji amesema anasikitishwa na uongozi wa CCM Mkoa wa Singida bila sababu za msingi wanachelewesha kuanza kwa mchakato wa ukarabati wa uwanja huo.
Aidha amesema kuna vikao vingi viimefanyika na makampuni hayo bila mafanikio na hivyo anaomba CCM Makao makuu kuingilia kati ili kama kuna jambo linasababisha kusuasua kwa mchakato huo liweze kupatiwa ifumbuzi na ukarabati ufanyike haraka iwezekanavyo.
wakicheza
Vijana wakicheza mpira uwanjani humo.
Amesema suala la uchakavu wa uwanja wa Namfua imekuwa ni kero kubwa inayowakabili wananchi wa jimbo la singida mjini kwa sasa na hivyo kuwanyima vijana fursa za kutumia uwanja huo ili kupata ajira na kukuza vipaji kwa vijana.
Kutokana na ukweli kwamba muda wa kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015 unayoyoma, Dewji maarufu kwa jina la "MO" amemwomba Katibu Mkuu wa CCM kuingilia kati urasimu huo usio wa lazima ili ujenzi uweze kufanyika mapema.
Akizungumzia madai hayo ya Mbunge Dewji, Katibu wa CCM Mkoa wa Singida, Naomi Kapambala alikiri kupata nakala ya barua hiyo na kusema kuwa wamefanya matayarisho yote muhimu ikiwa ni pamoja na kufuatilia Airtel makao makuu juu ya suala hilo.
Aidha Kapambala amesema kuwa kamati ya siasa imemaliza kazi na kupeleka baraza la wadhamini, na kinachosubiriwa na baraza kukaa ili kutoka majibu.
“Mi namshangaa ni kwa nini yeye mwenyewe Dewji hajafika hapa ofisini na kupata ufafanuzi juu ya hili matokeo yake analeta nakala ya barua kwetu, akamwulize katibu Mkuu ambaye amemwandikia hii barua.” Alisema Kapambala
Hata wakati katibu mkuu alipokuja hapa tulimweleza juu ya hilo , yeye kama anaonaje ni vyema akafika ofisini ili kujua inachoendelea.
jukwaa
Sehemu ya jukwaa la uwanja wa Namfua linalotumiwa na washabiki likiwa linaonekana kuchakaa.
Aidha Kapambala amesema Katibu mkuu msaidizi yuko jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine wamemwagiza kupitia baraza la wadhamini wa CCM ili kujua hatma ya suala hilo.
Pia Kapambala amesema pia ofisi yake imekwishatoa notisi kwa wafanyabiashara mbalimbali kuondoka kwenye eneo la uwanja ili kupisha ukarabati huo.
Mwenyekiti wa SIREFA Baltazari Kimario alisema anasikitishwa kuona maendeleo ya uwanja huo bado haujakamilika na hivyo kuathiri maendeleo ya soka katika mkoa wa singida.
Aidha wadau mbalimbali nao wametoa masikitiko yao kwa uongozi wa CCM Mkoa wa singida kuchelewesha mchakato huo kwa maslahi binafsi, huku Mbunge akiwa tayari kushughulikia kero hiyo.
Uwanja huo hivi sasa umebaki kuwa kama eneo maarufu la vijana kuvuta bangi na wengine kujisaidia hovyo kwenye vyoo na hivyo kutapakaa kwa vinyesi kila mahali ndani ya uwanja huo.
Ujenzi wa Uwanja wa Namfua,ambao ulikuwa ukienda sambamba na Jengo la CCM mkoa, ulisimama miaka ya 1990 na tangu wakati huo uwanja huo umebakia gofu na kugeuka maficho ya wahalifu mbalimbali na eneo la choo cha jumuiya.
waandishi
Baadhi ya Waandishi wa habari wa Mkoa wa Singida wakipiga picha jengo la makao makuu ya CCM Mkoa wa Singida.
bangi
Vijana hawa walikutwa wakivuta bangi kwenye majukwaa ya uwanja wa Namfua.
jengo la ccm
Hapa ndio makao makuu ya CCM Mkoa wa Singida.(Picha zote na Hillary Shoo).
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa