Mshitakiwa Juliana Ibrahimu akitolewa nje ya chumba cha mahakama kuu baada ya kuzirai kutokana na kuhukumiwa kutumikia jela miaka mitatu baada ya kukiri kosa la kuuwa bila kukusudia.
Askari polisi wa kike wakimpunguzia nguo mshitakiwa Juliana Ibrahimu ili waweze kupepea upepo aweze kuzinduka baada ya kuzirai kutokana na kuhukumiwa adhabu ya kwenda jela miaka mitatu kwa kosa la kuuwa jirani yake Maria Musa, bila kukusudia.(Picha zote na Nathaniel Limu).
Mwanamke mkazi wa kijiji cha Musimihi tarafa ya Ilongero wilaya ya Singida, Juliana Ibrahimu (52),ameanguka kizimbani na kisha kuzirai na kupoteza fahamu, baada ya kuhukumiwa na mahakama kuu kanda ya Dodoma, kutumikia jela miaka mitatu.
Mahakama kuu kanda ya Dodoma inayoendelea na vikao vyake mjini hapa, ilimhukumu Juliana hukumu hiyo,baada ya kukiri kosa la kumuua jirani yake, Maria Musa, bila kukusudia kwa madai ya kunyimwa makande kwenye sherehe ya harusi.
Mshitakiwa Juliana, alihukumiwa adhabu hiyo pamoja na mtoto wake Pendo Yohana, ambaye naye atatumikia jela miaka mitatu kwa kukiri kosa hilo.
Baada ya washitakiwa hao kusomewa shitaka hilo la mauaji ambalo walilitenda agosti tano mwaka 2006, wote kwa pamoja, bila hofu kila moja kwa wakati wake alikiri kosa hilo .
Awali mwanasheria wa serikali Ahmed Seif, alidai mbele ya mrajisi wa mahakama hiyo, Renatus Rutatinisibwa, kuwa mnamo agosti tano mwaka 2006, muda usiofahamika,washitakiwa wote kwa pamoja, walimpiga Maria na kusababisha kifo chake siku 27 baadaye.
Alisema siku ya tukio, mshitakiwa Juliana akiwa amefuatana na mtoto wake Pendo, walikwenda nyumbani kwa marehemu (Maria) kumuliza ni kwa nini aliwanyima makande kwenye sherehe ya harusi (harusi hiyo iifanyika 4/8/2006).
Seif alisema marehemu aliwajibu kuwa hawezi kujibu swali hilo na kwamba mwenye uwezo wa kulijibu swali hilo , ni Dilu Mohammed.
Alisema washitakiwa walikasirishwa na jibu hilo liliyotolewa na marehemu na ndipo walipoanza kumshambulia.
Baada ya kutolewa kwa uhukumu hiyo, mshitakiwa wa kwanza,Juliana akiwa bado yupo kizimbani, alidondoka chini na mrajisi Rutatinisibwa, akaamuru atolewe nje kwenda kupepewa upepo.
Kwa hisani ya Mo Blog
Kwa hisani ya Mo Blog
0 comments:
Post a Comment