WATAKAO URAIS CCM MTEGONI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 

KAMATI ya Usalama na Maadili ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Agosti mwaka huu, itafanya mapitio ya mwenendo wa wanachama wake waliopewa onyo kwa kosa la kuanza kampeni za kutafuta kuteuliwa kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu 2015, kabla ya wakati kinyume na Kanuni za Uongozi na Maadili ya CCM, toleo la Februari 2010, Ibara 6(7)(i).

 

Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Bw. Nape Nnauye, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya kile kilichozungumzwa kwenye kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM iliyofanya kikao cha siku moja jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete.

 

Alisema pamoja na mambo mengine, kikao hicho kilipokea taarifa ya mazungumzo yanayoendelea kati ya CCM kwa upande mmoja na vyama vingine vya siasa ambavyo ni CHADEMA, NCCR-Mageuzi na CUF ambayo yanasimamiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis Mutungi.

Bw. Nnauye alisema, lengo la mazungumzo yaliyokutanisha vyama hivyo ni kuangalia kwa kina sababu za baadhi ya wajumbe wachache wa Bunge Maalumu la Katiba, kususia na kutoka nje katika awamu ya kwanza ya vikao vya Bunge hilo.

Lengo lingine ni kuangalia namna ambavyo wajumbe hao watarudi bungeni ili kukamilisha mchakato wa mabadiliko ya Katiba ambapo Kamati Kuu ya CCM, imeridhishwa na mwenendo wa mazungumzo hayo, kupongeza juhudi zinazofanywa na Jaji Mutungi pamoja na vyama husika vinavyoshiriki mazungumzo.

 

"Kamati Kuu pia ilipokea taarifa za harakati za baadhi ya wanachama wa CCM walioonesha nia ya kuomba ridhaa ya chama kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu 2015...baada ya kutafakari kwa kina, Kamati hii inapenda kuwakumbusha wote kuwa ili wasipoteze sifa za kugombea ni muhimu wakazingatia katiba, kanuni na taratibu za chama.

"Wanachama waliopewa adhabu na Kamati Kuu kutokana na kukiuka taratibu za chama katika suala hili, Kamati ya Usalama na Maadili ya chama itafanya mapitio ya mwenendo wao na utekelezaji wa adhabu hiyo Agosti mwaka huu.

"Ikibainika hawatekelezi ipasavyo masharti ya adhabu zao, itapendekeza kwa Kamati Kuu iongeze adhabu kwa kuzingatia taratibu za chama," alisema Bw. Nnauye.

Aliongeza kuwa ni muhimu wanachama wote wakatambua kuwa, chama ni pamoja na Katiba, kanuni na taratibu zake hivyo kutoziheshimu na kuzifuata ni kuvuruga jambo ambalo haliwezi kuvumilika.

Alisema dhamira ya CCM kusimamia Katiba, kanuni na taratibu za chama ni kuhakikisha chama hicho kinakuwa na umoja, mshikamano ambao ni wa muhimu sana hasa wanapokwenda kukamilisha kazi ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2010/15.

Februari mwaka huu, CCM ilifanya vikao vya kitaifa ambavyo vilishughulikia suala la maadili ndani ya chama vikihusisha Kamati Ndogo ya Udhibiti, Tume ya Udhibiti na Nidhamu na Kamati Kuu.

Vikao hivyo viliwahoji baadhi ya wanachama wa chama hicho ambao ni Bw. Frederick Sumaye, Bw. Edward Lowasa, Bw. Bernard Membe, Bw. Stephen Wassira, Bw. January Makamba na Bw. William Ngeleja.

Baada ya wanachama waliohojiwa, ilithibitika kuwa baadhi ya tuhuma dhidi yao ni za kweli hivyo kamati zilipendekeza adhabu na mapendekezo hayo yalipelekwa kwenye Tume ya Udhibiti na Nidhamu na hatimaye Kamati Kuu ya CCM ambayo ilitoa adhabu kwa wahusika.

Ilithibitika wanachama hao walifanya makosa mawili, mosi la kuanza kampeni za kutafuta kuteuliwa kugombea Urais kabla ya wakati kinyume na Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM, Toleo la Februari 2010, Ibara 6(7)(i).

Kosa la pili ni kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya chama na baadhi yao kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya jamii kinyume na Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM, Toleo la Februari 2010, Ibara kadhaa za kanuni hizo.

Kwa mujibu wa Bw. Nnauye ambaye alitoa tamko la CCM Februari 18 mwaka huu juu ya adhabu zilizochukuliwa kwa wanachama hao, alisema Kamati Kuu baada ya kuthibitisha makosa hayo imewapa watu hao adhabu ya onyo kali na kuwataka wajiepushe na vitendo vinavyokiuka maadili na iwapo wataendelea na vitendo hivyo, chama kitawachukulia hatua kali zaidi.

Alisema tafsiri ya adhabu ya onyo kali kwa mujibu wa Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM, Toleo la Februari 2010, Ibara ya 8(ii) (b) ni mwanachama aliyepewa adhabu ya onyo kali, atakuwa katika hali ya kuchunguzwa kwa muda usiopungua miezi 12, ili kumsaidia katika jitihada zake za kujirekebisha.

Aliongeza kuwa, Kamati Kuu iliitaka Kamati Ndogo ya Udhibiti kuwachunguza na kuchukua hatua kwa wote waliohusika kwa namna moja au nyingine (mawakala na wapambe) kufanyika kwa vitendo hivyo ambavyo vilivunja kanuni za chama.

Pia Kamati Kuu iliwaonya vikali viongozi na watendaji wa chama ikiwataka wajiepushe kujihusisha na matendo ya wanaowania urais yanayovunja na kukiuka maadili ya chama badala yake wazingatie kanuni na taratibu za chama.

Chanzo:Majira

WAKAMATWA NA NYARAZA MIL.200/-

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

WATU sita wakazi wa wilayani ya Manyoni mkoani Singida, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kukutwa na nyara za serikali zenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 200.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkuu wa Wilaya hiyo, Fatma Toufiq, bila kuwataja watuhumiwa hao, alisema kuwa tukio hilo lilitokea Julai 8, mwaka huu, kwenye nyumba ya kulala wageni iitwayo Matunda.
 Alizitaja nyara hizo kuwa ni vipande 28 vya meno ya tembo ambavyo ni sawa na tembo wanane, singa za tembo bando sita, ngozi ya simba moja, mkia wa pofu, kucha nne za simba, silaha aina ya SMG mbili, risasi 48 na magazine tatu.
Toufiq alisema nyara hizo zote zina thamani ya sh. 202,560,000 na kwamba Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ambapo ukikamilika watuhumiwa hao watapelekwa mahakamani.
Katika hatua nyingine, Toufiq alisema baada ya Operesheni Tokomeza matukio ya ujangili wa tembo yaliendelea kwenye maeneo mbalimbali ya Ikolojia.
Alisema kuwa katika matukio matatu, askari wa Kikosi cha Kuzuia Ujangili Kanda ya Kati (KDU) na polisi Manyoni waliwakamata watuhumiwa wanne wakiwa na meno ya tembo sita na vipande 37 ambavyo ni sawa na tembo 15.
Kwa mujibu wa Toufiq watuhumiwa hao ni George James maarufu kama Maige aliyekamatwa Februari 12, mwaka huu, katika Kijiji cha Mgandu, akiwa na vipande 21 vyenye uzito wa kilo 39.5 ambavyo thamani yake ni sh. 34,760,000.
Mtuhumiwa mwingine ni Ally Hamadi aliyekamatwa Februari 16, mwaka huu, katika Kijiji cha Mgandu, akiwa na vipande 16 vyenye uzito wa kilo 19.4 vyenye thamani ya sh. 17,072,000.
Wengine kwa mujibu wa mkuu wa wilaya, ni David Makasi na Joseph Malima waliokamatwa Machi 29, mwaka huu, wakiwa na nyara mbalimbali zenye kilo 31.1 ambazo thamani yake ni sh. 27,368,000 na kwamba nyara zote hizo zina thamani ya sh. 79,200,000.
Alifafanua kuwa tembo wote waliuawa kwenye mapori ya akiba ya Rungwa/Kizigo/Mhesi na kwamba Ikolojia ya Rungwa–Ruaha bado ina tembo wengi ambao huzunguka kwenye mapori ya akiba ya Rungwa/Kizigo/Muhesi, Swagaswaga na Mkungunero.
Toufiq aliongeza kuwa mapori mengine ni hifadhi za taifa za Ruaha, Tarangire, Mikumi na Manyara na hujumuisha pia na mapori ya wazi ya Mgori, Itiso, Pawaga, Pwaga Rumuma, Mtera, Chaya, Mwamagembe, Shelui na Sambaru/Londoni.
Kwa kutambua changamoto hiyo, mkuu huyo wa wilaya alibainisha kuwa ofisi ya Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori ilifanya mawasiliano na wakuu wa taasisi za Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa).
 Alisema mawasiliano hayo yalifanyika ili kuwezesha wakuu wa kanda dhidi ya ujangili (KDU-Arusha na Manyoni) katika kupambana na ujangili kushirikiana na kikosi kazi cha Ikolojia ya Ngorongoro, Manyara-Tarangie ambacho kimekuwa kinafuatilia mitandao ya ujangili sehemu mbalimbali na tayari wanayo kanzi data (Data Base).
Chanzo:Tanzania Daima

ABIRIA WA TRENI WAKWAMA MANYONI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 

ZAIDI ya abiria 700 waliokuwa wakisafiri na treni ya abiria wakitokea Kigoma kuelekea Dar es Salaam, wamekwama kwa siku mbili wilayani Manyoni, baada ya treni ya mizigo kuanguka.
Wakizungumza na waandishi wa habari waliofika eneo hilo jana, abiria hao wamelilalamikia Shirika la Reli kutokana na kutokuwa na utaratibu mzuri wa kusafirisha abiria wake pindi tatizo linapojitokeza.
Walisema walipofika Manyoni majira ya mchana, walielezwa kuwa treni ya mizigo ilikuwa imeanguka kituo kinachofuatia cha Saranda, hivyo wasubiri utaratibu.
“Lakini cha kushangaza mabasi ambayo yalikuwa yakiletwa na Shirika la TRL yalikuwa machache kwa sababu abiria tulikuwa wengi,” alisema mmoja wa abiria hao, Anton Beni.
Walisema kutokana na hali hiyo walilazimika kulala nje huku wakiwa na watoto wadogo na wengine wagonjwa, kwani mabasi yalipokuwa yakifika kuwachukua hakukuwa na utaratibu na kusababisha watu kugombea na kusema hadi sasa baadhi ya abiria hawajui hatima yao ya kufika Dar es Salaam.
Meneja wa Kanda wa TRL kutoka Dar es Salaam, Philipo Rutizibwa, alisema suala la abiria waliokwama Manyoni wameshafanya utarabu wa mabasi na yameshaanza kuwachukua kuwapeleka wanakokwenda
 Chanzo:Tanzania Daima

WAZIRI NYALANDU AMWAGA MSAADA WA MILIONI 10 WA MABATI 420 SHULE ZA SEKONDARI KWA AJILI YA MAABARA


diwani
Diwani wa Kata ya Kinyeto, Francisco Ng’eni akipokea msaada wa mabati 200 kutoka kwa Mwenyekiti Hanje kwa niaba wa Mbunge wa Jimbo hilo Mhe, Lazaro Nyalandu.
kabidhi
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Singida Vijijini, Narumba Hanje (kulia) akimkabidhi mabati 220 yenye thamani ya shilingi milioni tano Afisa Mtandaji wa Kata ya Mtinko Jimbo la Singida Kaskazini, Eliufoo Mkanga katika hafla fupi iliyofanyika jana katika shule ya Sekondari ya Kata ya Mtinko , mabati hayo yametolewa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maabara na Mbunge wa Jimbo hilo Mhe,Lazaro Nyalandu.
maabara
Hili ni jengo la maabara ya sekondari ya Kinyeto likiwa katika hatua ya lenta.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

DC Iramba ahamia kijijini kufanikisha Ujenzi wa Zahanati

2
Mkuu wa wilaya ya Iramba mkoani Singida, Yahaya Nawanda.
Na Mwandishi wetu-Mo Blog
MKUU wa wilaya ya Iramba mkoa wa Singida,Yahaya Nawanda, ameahidi kuishi kwa siku tano katika nyumba za kabila la kisukuma kijiji cha Kizonzo tarafa ya Shelui, ili kuhakikisha zoezi la kukusanya michango ya ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho linafanikiwa.
Nawanda ametoa ahadi hiyo wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa uhamasishaji wananchi kujiunga na mfuko wa afya ya jamii (CHF),uliofanyika kwenye kijiji cha Kizonzo.
Alisema katika kipindi hicho atasimamia kwa karibu uchangiaji huo,ili ujenzi wa zahanati hiyo uweze kufanyika mapema iwezekanavyo.
“Ninyi ndugu zangu, mmekuwa mkipata taabu sana kufuata huduma ya afya kwenye zahanati ya kijiji cha Mgongo kwa kutembea umbali wa kilomita nane kwenda na kurudi. Akina mama wajawazito ndio wanaotaabika zaidi”, alifafanua Nawanda 
“Sasa tunasema hatutakubali kabisa ninyi muendelee kutaabika kufuata matibabu umbali mrefu kiasi hicho.Tunataka kipindi kifupi kijacho,matibabu muyapate hapa hapa kijijini kwenu”.
Kutokana na hali hiyo Nawanda amewataka wananchi kujiandaa mapema kwa zoezi hilo la uchangiaji wa ujenzi wa zahanati yao unaotarajiwa uanza mapema iwezekanavyo.
Kuhusu mfuko wa afya ya jamii (CHF),mkuu huyo wa wilaya,alisema suala la kujiunga na mfuko huo ni la lazima kwa madai kwamba afya bora ni mtaji wa mwili wa binadamu ye yote.
“Wilaya yetu ya Iramba, ni wilaya ya kwanza nchini kwa vituo vyake vyote vya afya kuwa na dawa za kutosha wakati wote.Kwa hiyo mwanachama wa CHF, nawahakikishia kuwa mtapata tiba wakati wote pindi watakapougua”,alisema DC huyo.
Kwa mujibu wa Dc Nawanda, kuku moja wa kienyeji mwenye thamani ya shilingi 10,000 tu, anatosha kugharamia ada ya kaya moja yenye mume, mke moja na watoto wanane, kupata matibabu kwa kipindi cha mwaka moja bila kuongeza kiasi kingine cha fedha.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

HII NDO SARAFU MPYA YA TSH. 500/= ITAKAYOANZA KUTUMIKA HIVI KARIBUNI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Sarafu mpya ya Tsh. 500/=
Baada ya kuonekana noti ya shilingi 500 ina na mzunguko mkubwa wa matumizi na inachakaa kwa haraka huku kiwango chake cha kuhimili mizunguko ni miezi sita, Benki kuu ya Tanzania (BOT) inatarajia kubadili noti hiyo na kuifanya sarafu.
Sarafu hiyo ya 500 inatarajiwa kutambulishwa na kuanza kutumika July 2014 ikienda sambamba na kipindi cha mwaka huu wa fedha ambapo unaambiwa hii sarafu ikishatoka inatarajiwa kudumu kwenye mzunguko kwa zaidi ya miaka 20 na kubaki na ubora wake uleule, yani ni imara kuliko noti.
Noti ya 500 inayotumika sasa

Afisa mkuu wa benki kitengo cha idara kurugenzi za kibenki Patrick Fata ameongea na millardayo.com na kusema “Tunafanya hivi kwasababu noti ya 500 inachakaa haraka kulinganisha na mzunguko wake na kuwafikia watu wengi pia huchakaa haraka kutokana na mzunguko wa kushikwa na watu wanaofikia mpaka milioni moja kwa siku, hiyo ni idadi kubwa kuliko ya wanaoshika noti ya elfu 10 kwa siku’

MIL.857/-KUKAMILISHA MIRADI YA MAJI MANYONI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
WIZARA ya Maji imetenga sh milioni 857 ili kukamilisha programu ya maji vijijini na usafi wa mazingira katika vijiji 10 vya Tarafa ya Kintinku wilayani Manyoni, Singida vilivyopo kwenye mradi wa Benki ya Dunia.
Fedha hizo zilizotengwa kwenye mwaka wa fedha 2014/2015 ni sehemu ya sh bilioni 1.5 kwa ajili ya tarafa hiyo kuwawezesha wakazi wa vijiji hivyo kuwa na uhakika wa majisafi na salama kabla ya mwisho wa mwaka 2015.
Naibu Waziri wa Maji, Amosi Makala, alitoa ahadi hiyo alipozungumza na wakazi wa Kata ya Chikuyu, Tarafa ya Kintinku kuhusu kumalizika kwa tatizo la maji lililowakabili kwa muda mrefu.
Makala ambaye pia ni Mbunge wa Mvomero, alivitaja vijiji vitakavyonufaika na mradi huo kuwa ni Kintinku, Lusilile, Ngaiti, Mvumi, Maweni, Chilejeho, Mtiwe, Chikuyu, Mwiboo na Mbwasa.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa tarafa hiyo, Diwani wa Viti Maalumu, Zinduna Abdallah (CCM), alimweleza naibu waziri huyo kwamba tatizo la maji limeharibu ndoa za watu.
Mhandisi wa Sekretarieti ya mkoa huo, Yunusi Rugeyamu, alisema sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 inaonyesha kuwa Singida ilikuwa na wakazi 1,370,637 na kwamba hadi Desemba mwaka jana wakazi 656,932 waishio vijijini wanapata maji.
Chanzo;Tanzania Daima  

DADA WA KAZI AMUUA BOSI WAKE KWA KISU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
SAKATA la wafanyakazi wa ndani kunyanyaswa na mabosi wao, limechukua sura mpya baada ya Valetina Kerenge (17), kumgeuzia kibao bosi wake.
Mfanyakazi huyo wa ndani, mwenyeji wa Wilaya ya Ukerewe, mkoani Mwanza, anadaiwa kumuua bosi wake, Asha Juma (24) kwa kumchoma kisu sehemu ya juu ya titi la kulia kwa madai ya kuchoshwa na manyanyaso.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida (SACP), Geofrey Kamwela, alisema tukio hilo la kusikitisha limetokea jana majira ya saa nne asubuhi katika eneo la Sabasaba, Kata ya Utemini, mkoani hapa.
Alisema Asha alikuwa karani wa Mahakama ya Wilaya ya Singida na alikuwa akiishi na mfanyakazi wake huyo wa ndani kwa takribani mwaka mmoja sasa.
“Baada ya msichana huyo kumchoma bosi wake kwa kisu, alitoka nje ya nyumba na kukimbilia kwa majirani kwa ajili ya kuomba msaada, lakini wakati majirani wakiwa katika harakati za kumpeleka majeruhi huyo hospitali, alianguka chini na kufa papo hapo,” alisema Kamanda Kamwela.
 Kwa mujibu wa kamanda huyo, mtuhumiwa huyo alikimbia  baada ya bosi wake kufariki dunia, lakini majira ya saa nane alikamatwa akiwa kwenye harakati za kutoroka.
“Kwa ushirikiano na raia wema, tulifanikiwa kumkamata msichana huyo jana majira ya saa nane eneo la Uwanja wa Ndege akiwa katika harakati za kutoroka,” alisema Kamanda Kamwela.
Alisema mtuhumiwa anahojiwa kuhusiana na tukio hilo na uchunguzi zaidi unaendelea kujua chanzo cha mauaji hayo.
Chanzo;Tanzania Daima 
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa