Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
SAKATA la wafanyakazi wa ndani kunyanyaswa na mabosi wao,  
limechukua sura mpya baada ya Valetina Kerenge (17), kumgeuzia kibao 
bosi wake.
  Mfanyakazi huyo wa ndani, mwenyeji wa Wilaya ya Ukerewe, mkoani  
Mwanza, anadaiwa kumuua bosi wake, Asha Juma (24) kwa kumchoma kisu 
sehemu ya  juu ya titi la kulia kwa madai ya kuchoshwa na manyanyaso.
  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida (SACP), Geofrey Kamwela, alisema  
tukio hilo la  kusikitisha limetokea jana majira ya saa nne asubuhi 
katika eneo la Sabasaba,  Kata ya Utemini, mkoani hapa.
  Alisema Asha alikuwa karani wa Mahakama ya Wilaya ya Singida na  
alikuwa akiishi na mfanyakazi wake huyo wa ndani kwa takribani mwaka 
mmoja  sasa.
  “Baada ya msichana huyo kumchoma bosi wake kwa kisu, alitoka nje  ya 
nyumba na kukimbilia kwa majirani kwa ajili ya kuomba msaada, lakini 
wakati  majirani wakiwa katika harakati za kumpeleka majeruhi huyo 
hospitali, alianguka  chini na kufa papo hapo,” alisema Kamanda Kamwela.
   Kwa mujibu wa kamanda huyo, mtuhumiwa huyo alikimbia  baada ya bosi 
wake kufariki dunia, lakini  majira ya saa nane alikamatwa akiwa kwenye 
harakati za kutoroka.
  “Kwa ushirikiano na raia  wema, tulifanikiwa kumkamata msichana huyo 
jana majira ya saa nane eneo la  Uwanja wa Ndege akiwa katika harakati 
za kutoroka,” alisema Kamanda Kamwela.
  Alisema mtuhumiwa anahojiwa kuhusiana na tukio hilo na uchunguzi zaidi unaendelea kujua  chanzo cha mauaji hayo.
Chanzo;Tanzania Daima  
0 comments:
Post a Comment