Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WATU sita wakazi wa wilayani ya Manyoni mkoani Singida,
wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kukutwa na nyara za
serikali zenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 200.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkuu wa Wilaya
hiyo, Fatma Toufiq, bila kuwataja watuhumiwa hao, alisema kuwa tukio
hilo lilitokea Julai 8, mwaka huu, kwenye nyumba ya kulala wageni
iitwayo Matunda.
Alizitaja nyara hizo kuwa ni vipande 28 vya meno ya tembo ambavyo ni
sawa na tembo wanane, singa za tembo bando sita, ngozi ya simba moja,
mkia wa pofu, kucha nne za simba, silaha aina ya SMG mbili, risasi 48 na
magazine tatu.
Toufiq alisema nyara hizo zote zina thamani ya sh. 202,560,000 na
kwamba Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ambapo ukikamilika
watuhumiwa hao watapelekwa mahakamani.
Katika hatua nyingine, Toufiq alisema baada ya Operesheni Tokomeza
matukio ya ujangili wa tembo yaliendelea kwenye maeneo mbalimbali ya
Ikolojia.
Alisema kuwa katika matukio matatu, askari wa Kikosi cha Kuzuia
Ujangili Kanda ya Kati (KDU) na polisi Manyoni waliwakamata watuhumiwa
wanne wakiwa na meno ya tembo sita na vipande 37 ambavyo ni sawa na
tembo 15.
Kwa mujibu wa Toufiq watuhumiwa hao ni George James maarufu kama
Maige aliyekamatwa Februari 12, mwaka huu, katika Kijiji cha Mgandu,
akiwa na vipande 21 vyenye uzito wa kilo 39.5 ambavyo thamani yake ni
sh. 34,760,000.
Mtuhumiwa mwingine ni Ally Hamadi aliyekamatwa Februari 16, mwaka
huu, katika Kijiji cha Mgandu, akiwa na vipande 16 vyenye uzito wa kilo
19.4 vyenye thamani ya sh. 17,072,000.
Wengine kwa mujibu wa mkuu wa wilaya, ni David Makasi na Joseph
Malima waliokamatwa Machi 29, mwaka huu, wakiwa na nyara mbalimbali
zenye kilo 31.1 ambazo thamani yake ni sh. 27,368,000 na kwamba nyara
zote hizo zina thamani ya sh. 79,200,000.
Alifafanua kuwa tembo wote waliuawa kwenye mapori ya akiba ya
Rungwa/Kizigo/Mhesi na kwamba Ikolojia ya Rungwa–Ruaha bado ina tembo
wengi ambao huzunguka kwenye mapori ya akiba ya Rungwa/Kizigo/Muhesi,
Swagaswaga na Mkungunero.
Toufiq aliongeza kuwa mapori mengine ni hifadhi za taifa za Ruaha,
Tarangire, Mikumi na Manyara na hujumuisha pia na mapori ya wazi ya
Mgori, Itiso, Pawaga, Pwaga Rumuma, Mtera, Chaya, Mwamagembe, Shelui na
Sambaru/Londoni.
Kwa kutambua changamoto hiyo, mkuu huyo wa wilaya alibainisha kuwa
ofisi ya Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori ilifanya mawasiliano na
wakuu wa taasisi za Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Mamlaka
ya Hifadhi za Taifa (Tanapa).
Alisema mawasiliano hayo yalifanyika ili kuwezesha wakuu wa kanda
dhidi ya ujangili (KDU-Arusha na Manyoni) katika kupambana na ujangili
kushirikiana na kikosi kazi cha Ikolojia ya Ngorongoro, Manyara-Tarangie
ambacho kimekuwa kinafuatilia mitandao ya ujangili sehemu mbalimbali
na tayari wanayo kanzi data (Data Base).
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment