Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
KAMATI
ya Usalama na Maadili ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Agosti mwaka huu,
itafanya mapitio ya mwenendo wa wanachama wake waliopewa onyo kwa kosa
la kuanza kampeni za kutafuta kuteuliwa kugombea urais katika Uchaguzi
Mkuu 2015, kabla ya wakati kinyume na Kanuni za Uongozi na Maadili ya
CCM, toleo la Februari 2010, Ibara 6(7)(i).
Katibu wa NEC, Itikadi
na Uenezi wa CCM, Bw. Nape Nnauye, aliyasema hayo Dar es Salaam jana
wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya kile kilichozungumzwa
kwenye kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM iliyofanya kikao
cha siku moja jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya
Kikwete.
Alisema pamoja na mambo
mengine, kikao hicho kilipokea taarifa ya mazungumzo yanayoendelea kati
ya CCM kwa upande mmoja na vyama vingine vya siasa ambavyo ni CHADEMA,
NCCR-Mageuzi na CUF ambayo yanasimamiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa
nchini Jaji Francis Mutungi.
Bw. Nnauye alisema,
lengo la mazungumzo yaliyokutanisha vyama hivyo ni kuangalia kwa kina
sababu za baadhi ya wajumbe wachache wa Bunge Maalumu la Katiba, kususia
na kutoka nje katika awamu ya kwanza ya vikao vya Bunge hilo.
Lengo lingine ni
kuangalia namna ambavyo wajumbe hao watarudi bungeni ili kukamilisha
mchakato wa mabadiliko ya Katiba ambapo Kamati Kuu ya CCM, imeridhishwa
na mwenendo wa mazungumzo hayo, kupongeza juhudi zinazofanywa na Jaji
Mutungi pamoja na vyama husika vinavyoshiriki mazungumzo.
"Kamati Kuu pia
ilipokea taarifa za harakati za baadhi ya wanachama wa CCM walioonesha
nia ya kuomba ridhaa ya chama kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu
2015...baada ya kutafakari kwa kina, Kamati hii inapenda kuwakumbusha
wote kuwa ili wasipoteze sifa za kugombea ni muhimu wakazingatia katiba,
kanuni na taratibu za chama.
"Wanachama waliopewa
adhabu na Kamati Kuu kutokana na kukiuka taratibu za chama katika suala
hili, Kamati ya Usalama na Maadili ya chama itafanya mapitio ya mwenendo
wao na utekelezaji wa adhabu hiyo Agosti mwaka huu.
"Ikibainika
hawatekelezi ipasavyo masharti ya adhabu zao, itapendekeza kwa Kamati
Kuu iongeze adhabu kwa kuzingatia taratibu za chama," alisema Bw.
Nnauye.
Aliongeza kuwa ni
muhimu wanachama wote wakatambua kuwa, chama ni pamoja na Katiba, kanuni
na taratibu zake hivyo kutoziheshimu na kuzifuata ni kuvuruga jambo
ambalo haliwezi kuvumilika.
Alisema dhamira ya CCM
kusimamia Katiba, kanuni na taratibu za chama ni kuhakikisha chama hicho
kinakuwa na umoja, mshikamano ambao ni wa muhimu sana hasa wanapokwenda
kukamilisha kazi ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2010/15.
Februari mwaka huu, CCM
ilifanya vikao vya kitaifa ambavyo vilishughulikia suala la maadili
ndani ya chama vikihusisha Kamati Ndogo ya Udhibiti, Tume ya Udhibiti na
Nidhamu na Kamati Kuu.
Vikao hivyo viliwahoji
baadhi ya wanachama wa chama hicho ambao ni Bw. Frederick Sumaye, Bw.
Edward Lowasa, Bw. Bernard Membe, Bw. Stephen Wassira, Bw. January
Makamba na Bw. William Ngeleja.
Baada ya wanachama
waliohojiwa, ilithibitika kuwa baadhi ya tuhuma dhidi yao ni za kweli
hivyo kamati zilipendekeza adhabu na mapendekezo hayo yalipelekwa kwenye
Tume ya Udhibiti na Nidhamu na hatimaye Kamati Kuu ya CCM ambayo ilitoa
adhabu kwa wahusika.
Ilithibitika wanachama
hao walifanya makosa mawili, mosi la kuanza kampeni za kutafuta
kuteuliwa kugombea Urais kabla ya wakati kinyume na Kanuni za Uongozi na
Maadili za CCM, Toleo la Februari 2010, Ibara 6(7)(i).
Kosa la pili ni kufanya
vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya chama na baadhi yao kufanya
vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya jamii kinyume na Kanuni za Uongozi
na Maadili za CCM, Toleo la Februari 2010, Ibara kadhaa za kanuni hizo.
Kwa mujibu wa Bw.
Nnauye ambaye alitoa tamko la CCM Februari 18 mwaka huu juu ya adhabu
zilizochukuliwa kwa wanachama hao, alisema Kamati Kuu baada ya
kuthibitisha makosa hayo imewapa watu hao adhabu ya onyo kali na
kuwataka wajiepushe na vitendo vinavyokiuka maadili na iwapo wataendelea
na vitendo hivyo, chama kitawachukulia hatua kali zaidi.
Alisema tafsiri ya
adhabu ya onyo kali kwa mujibu wa Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM,
Toleo la Februari 2010, Ibara ya 8(ii) (b) ni mwanachama aliyepewa
adhabu ya onyo kali, atakuwa katika hali ya kuchunguzwa kwa muda
usiopungua miezi 12, ili kumsaidia katika jitihada zake za
kujirekebisha.
Aliongeza kuwa, Kamati
Kuu iliitaka Kamati Ndogo ya Udhibiti kuwachunguza na kuchukua hatua kwa
wote waliohusika kwa namna moja au nyingine (mawakala na wapambe)
kufanyika kwa vitendo hivyo ambavyo vilivunja kanuni za chama.
Pia Kamati Kuu
iliwaonya vikali viongozi na watendaji wa chama ikiwataka wajiepushe
kujihusisha na matendo ya wanaowania urais yanayovunja na kukiuka
maadili ya chama badala yake wazingatie kanuni na taratibu za chama.
Chanzo:Majira
0 comments:
Post a Comment