Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MFUGAJI na mkulima wa Kijiji cha Ufana, Kata ya Mgungira, Tarafa ya
Sepuka, wilayani hapa mkoani Singida, Sawaka Kujelwa, ametishia
kuwafungulia mashtaka mahakamani viongozi wawili wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), kata hiyo kwa madai ya kuuza zaidi ya ekari 500 anazozitegemea
kwa ajili ya makazi, kilimo na malisho.
Kujelwa, aliwataja viongozi hao kuwa ni Mwenyekiti wa CCM wa Kata,
Nhende Shija na Diwani Mussa Ng’imba, ambao alidai waliamua kuvamia
maeneo yake baada ya yeye kuugua ugonjwa wa kushindwa kwenda haja
ndogo, Desemba 21, 2009.
Alisema baada ya kuugua ndipo alilazimika kwenda kwenye matibabu
ambako alipita hospitali ya misheni ya Mtakatifu Gasper mjini Itigi,
Makiungu, Puma na hatimaye hospitali ya Rufaa ya KCMC Moshi, mkoani
Kilimanjaro mwaka 2010 alikopona.
“Baada ya kupata matibabu KCMC, madaktari walinishauri kukaa karibu
na hospitali hiyo kwa uchunguzi zaidi, ambapo nilikaa hadi mwaka 2012
ndipo niliporudi nyumbani, lakini nikilazimika kufuata masharti ya
madaktari ya kutofanya kazi ngumu,” alisema.
Aliongeza kuwa wakati akiwa kwenye matibabu Moshi KCMC, ndipo diwani
kwa kushirikiana na mwenyekiti wa chama wa kata, walipoanza kuyavamia
maeneo yake aliyokuwa akiyategemea kwa kilimo na malisho ya mifugo, na
mwaka jana wakati anaendelea na mapumziko ya matibabu, watu walizidi
kuvamia.
Alisema kuwa baada ya kuona hali hiyo, aliandika barua kwa Kaimu
Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, kumjulisha, lakini bila mafanikio na
ndipo mwaka jana alimwandikia mwenyekiti wa kijiji kumfahamisha juu ya
uvamizi huo.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Matinje, Elius Milekwa na Mwenyekiti wa
Kijiji cha Ufana, Machiya Nyorobi, walipotakiwa kuzungumzia malalamiko
hayo, walikiri eneo lililovamiwa ni la Kujelwa na kwamba wanaoendesha
shughuli za kilimo na malisho kwa sasa ni wavamizi na hawataki
kuyaachia.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mgungira, Nhende Shija alipoulizwa sababu
za kuvamia maeneo hayo, alidai hakuvamia bali ni mali yake.
Diwani Ng’imba alisema kuwa, malalamiko hayo hayana ukweli wowote ila
ni mali yake na mwenyekiti huyo, na kwamba Sawaka ni tapeli tu.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment