Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Dk. Kitilla alisema kabla ya hapo, mbunge huyo alikuwa tayari 
kuwaachia viongozi wa chama chake wamvue uanachama kama alivyofanyiwa 
yeye na aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.
Alitoa kauli hiyo juzi wakati akiendesha mafunzo ya siku moja kwa 
viongozi wa mikoa na wajumbe wa Chama cha ACT–Tanzania juu ya historia, 
misingi, itikadi na falsafa ya chama hicho.
Alisema kwamba jopo la wasomi walimuelezea Zitto umuhimu wa kuangalia
 maslahi ya watu waliomchagua na njia inayotaka kutumika kufikia uamuzi 
wa kumvua uanachama wake katika chama hicho.
“Sisi tuliridhia kuvuliwa uanachama kwa kuwa hakukuwa na maslahi ya 
moja kwa moja yanayoweza kuathiri maisha yetu na familia zetu, lakini 
kwa Zitto hilo lingetokea na kumuathiri kwa mazingira yote mawili,” 
alisema.
Kuhusu kuandaa waraka unaodaiwa kuwa ni wa usaliti ndani ya CHADEMA, 
Dk. Kitilla alisema katika utatu wao wakiwa wanachama wa CHADEMA wakati 
huo walikuwa na nia ya mabadiliko ya muda mrefu ndani ya chama hicho 
baada ya kubaini baadhi ya mambo hayaendi sawa.
“Mimi, Mwigamba na Zitto tumekuwa na nia ya muda mrefu ya kuleta 
mabadiliko ndani ya CHADEMA, matamanio yetu ya mabadiliko yalihitimishwa
 kwa kuandika waraka wa mabadiliko, ukiainisha sababu za mabadiliko na 
mikakati yetu ya kushinda uchaguzi ndani ya chama,” alisema Dk. Kitilla.
Aliongeza baada ya Mwigamba kukutwa na waraka wa mabadiliko 
uliodhaniwa kuwa ni uhaini, walifukuzwa ndani ya chama hicho na kwamba 
hawakuona sababu ya kujiunga na chama kingine chochote cha siasa katika 
vyama vilivyopo.
Kwamba baada ya hali hiyo, vyama mbalimbali viliwafuata na kutaka 
wajiunge navyo, ikiwamo CCM, na waliwakatalia kwa kuamini kujiunga na 
chama hicho ni usaliti wa dhamira zao katika kufikia mabadiliko, na kuwa
 nchi ilipofika sio muda wa kukisaidia kuendelea kubaki madarakani.
Alisema matatizo yaliyopo katika vyama vya upinzani ni ya asili na 
yanafanana kwa kiasi kikubwa, ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa umakini,
 kuwepo kwa hisia umiliki pamoja na kukosekana kwa demokrasia.
Dk. Kitilla ambaye kwa sasa ni mshauri wa ACT-Tanzania, alisema iwe 
ni marufuku kwa mwanachama wa chama hicho kuzungumzia vyama vingine 
badala ya kuwazungumzia wananchi na matatizo yao.
Chanzo:Tanzania Daima 
0 comments:
Post a Comment