Home » » RAIS JAKAYA KIKWETE ATOA ZAWADI YA PASAKA KWA WAZEE WA KAMBI YA SUKAMAHELA WILAYANI MANYONI.

RAIS JAKAYA KIKWETE ATOA ZAWADI YA PASAKA KWA WAZEE WA KAMBI YA SUKAMAHELA WILAYANI MANYONI.

 Katibu tawala mkoa wa Singida (kulia) akikabidhi mbuzi watatu wakiwa ni zawadi kutoka kwa Rais Kikwete kwa wazee wasiojiweza wa kambi ya Sukamahela wilayani Manyoni.
 Katibu tawala mkoa wa Singida Liana Hassan (kulia) akikabidhi dumu la mafuta ya alizeti moja ya zawadi zilizotolewa na Rais Kikwete kwa wakazi wa kambi ya wazee ya Sukamahela.
 Katibu tawala mkoa wa Singida Liana Hassan (kulia) akimvisha shati mmoja wa wakazi wa kambi ya wazee ya Sukamahela.
 Katibu tawala mkoa wa Singida,Liana Hassan akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi zawadi zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete, kwa wakazi wa kambi ya Sukamahela wilayani Manyoni.Kushoto ni mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Manyoni,Fotunata Malya na anayefuata ni mke wa Ras, Liana Hassani.
Mkazi wa kambi ya wazee wasiojiweza ya Sukamahela wilayani Manyoni Kareudia Madoli akitoa shukurani kwa niaba ya wenzake kwa Rais Kikwete kwa msaada wake kwa ajili ya sherehe ya pasaka.Picha zote na Nathaniel Limu
---
Katibu tawala mkoa wa Singida,Liana Hassan amewahimiza  wakazi mkoani humo kujenga utamaduni wa kusaidia makundi ya watu wenye mahitaji ili pamoja na mambo mengine kuwapunguzia makali ya maisha.
Liana ametoa wito huo wakati akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi zawadi mbalimbali zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete, kwa wakazi wa kambi ya Sukamahela wilayani Manyoni.Msaada huo ni kwa ajili ya wakazi hao, kusheherekea pasaka.



Alisema upo umuhimu mkubwa kwa wakazi mkoani humo, kutambua kwamba wana wajibu wa kusaidia kwa hali na mali,makundi mbalimbali yenye mahitaji wakiwemo wazee wasiojiweza.



“Kwa hiyo ndugu zangu nawaombeni sana tumuunge mkono rais wetu Kikwete katika kuyasaidia makundi haya.Mwaka jana rais Kikwete alitoa msaada kwa watoto waishio kwenye mazingira magumu cha kituo cha Kititimo, na leo hii anawasaidia wakazi wa kambi hii ya Sukamahela”,alisema na kuongeza;“Hebu kila mmoja wetu kwa kadri ya uwezo wake utakavyomuruhusu,tumuunge rais kwa kuyasaidia makundi haya wakati wa sherehe mbalimbali na hata siku za kawaida”.



Awali afisa jamii mfawidhi wa makazi ya Sukamahela,Fredrick Mbyoya alitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili kambi hiyo, kuwa ni uhaba wa maji,wakazi hawajapata mavazi kwa muda mrefu na watoto wanaosoma Day care centre,shule ya msingi na sekondari,hawana viatu,sare,madaftari na kalamu.Kwa mujibu wa Mbyoya, kituo hicho kina wakazi 73 na nyumba za kuishi 54.



Zawadi zilizotolewa na rais kwa wakazi wa kambi ya Sukamahela, ni mchele kilo 112,lita 40 za mafuta ya alizeti na beberu (mbuzi) tatu wakubwa.Pia ofisi ya mkuu wa mkoa wa Singida,imemuunga mkono rais kwa kutoa msaada wa nguo mbalimbali kwa wakazi hao ambao baadhi,ni wagonjwa wa ukoma.Wakati huo huo, tarehe (7/4/2012) mbunge wa jimbo la Manyoni mashariki,John Chiligati,alitarajiwa kuwasaidia wakazi wa Sukamahela mchele kilo 100,mbuzi wawili na mafuta ya alizeti lita 20.


 


Lengo la msaada ni kuwawezesha wakazi hao kufurahia sikukuu ya pasaka.Pia Chiligati,alitarajiwa kuwasaidia wazee wasiojiweza wa Majengo Manyoni mjini,mchele kilo 20,mbuzi moja na mafuta ya alizeti,lita kumi.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa