Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Compassion International Tanzania Mchungaji Joseph Mitinje akipanda mti kwenye viwanja vya kanisa la FPCT kisaki nje kidogo ya mji wa Singida.(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Compassion International Tanzania (CIT) Mchungaji Joseph Mayala Mitinje, amewahimiza Watanzania kujenga utamaduni wa kupanda miti wakati wote badala ya kusubiri April mosi siku ya upandaji miti.
Mchungaji Mitinje ametoa wito huo wakati akishiriki kupanda miti kwenye viwanja vya kanisa la FPCT la kata ya Kisaki Manispaa ya Singida ambapo amesema kila mtu hivi sasa ni shahidi mzuri wa madhara yatokanayo na uhaba wa miti nchini.
Mitinje amesema baada ya miti kuvunwa ovyo, upatikanaji wa mvua sasa umekuwa adimu huku vyanzo vya maji vinaendelea kukauka na miti kwa matumizi ya binadamu nayo imekuwa ya shida katika upatikanaji wake.
Katika hatua nyingine, Mchungaji Mitinje, amewataka waumini wa kikristo na wananchi kwa ujumla, kutunza miradi ya maji inayoanzishwa katika maeneo yao na wafadhili, serikali na taasisi mbali mbali ili iweze kudumu kwa muda mrefu.
Amesema lengo la miradi hiyo ambayo inagharimu fedha nyingi mno,ni kuiunga serikali mkono katika juhudi zake za kupunguza/kuondoa tatizo la uhaba wa maji kwa wananchi wake.
Mkurugenzi huyo alikuwa katika ziara ya siku moja ya kikazi ya kuziundua visima virefu viwili vya maji viivyochimbwa katika kanisa la 814 FPCT Kisaki na 901 KLPT Singida mjini.
Kwa mujibu wa Mchungaji Mitinje visima hivyo vimegharimu zaidi ya shilingi 80.6 milioni.
0 comments:
Post a Comment