SINGIDA
ni moja kati ya mikoa ambayo ilikuwa inafanya vizuri katika mchezo wa
riadha miaka ya 1980 na kutoa wanariadha mahiri ambao waliiwakilisha
Tanzania katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.
Mkoa huo ni wenye mandhari nzuri yenye mawe mawe pamoja na mto upande wa kushoto na kulia hususan pale unapofika mkoani hapo.
Hakika
mkoa huu ni wenye vitu vingi, lakini kikubwa zaidi ni wakimbiaji wa
riadha hususan maeneo ya Singida Vijijini ambako kama wakimbiaji hao
wataweza kupewa vifaa maalumu kwa ajili ya kukimbia na wadau wa riadha
wakajitokeza na kuchangia zaidi katika riadha, Tanzania itakuwa na
medali nyingi na kupata heshima katika nchi mbalimbali duniani.
Nasema
hivyo kwa sababu hivi karibuni Mbunge wa Singida Vijijini ambaye pia ni
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu aliandaa
mashindano ya riadha hususan vijijini kwa ajili ya kuibua vipaji kwa
kushirikiana na Mkurugenzi wa Shrika la African Wildlife Trust (AWT),
Pratic Patel.
Mbio
hizo zilizojulikana kwa jina la Singida Marathon za kilometa 21,
zilianza rasmi Novemba 9, mwaka huu kwa kushirikisha wakimbiaji zaidi ya
400 kutoka Singida Mjini na Singida Vijijini na zilianzia Kijiji cha
Mitula, Kata ya Kinyagigi na kuishia Viwanja vya Shule ya Msingu Ntunduu
(W) Singida Vijijini.
Mbio
hizo zilikuwa za kilometa 21 ambazo ni nusu marathoni na kilometa 5 na
mwisho kabisa ni kilometa 2.5 ambazo ziliwashirikisha watoto wa kiume na
wa kike. Wakimbiaji walikuwa wamejiandaa wenyewe na walijiandikisha,
lakini baadhi yao pamoja na kukabiliwa na ukosefu wa viatu, lakini
waliweza kumudu hali hiyo kutokana na mazingira waliyokua nayo na
kuonesha vipaji vyao vilivyowashangaza wengi.
Inawezekana
kukimbia bila viatu ni jambo lisiloruhusiwa, lakini kutokana na
mazingira yenyewe ya vijijini hali hiyo haikuwa kikwazo kwa wakimbiaji
hao kukimbia bila viatu ila walionesha kuwa wana moyo na nia ya dhati
kuonesha vipaji vyao hakika ilikuwa faraja kubwa kwao kwani mwisho wa
siku waliweza kuibuka washindi na wengine wakapata kifuta jasho.
Washindi
hao ni Paulo Itambi ambaye aliibuka mshindi wa kwanza kwa upande wa
wanaume ambaye alipewa zawadi ya Sh 300,000, Emmanuel Samson wa pili (Sh
200,000) na Samwel Ikungi wa tatu (Sh 100,000). Kwa upande wa wanawake,
mshindi wa kwanza Fabiola William (Sh 300,000), Zakia Abdallah (Sh
200,000) na Winfrida Hassani (Sh 100,000).
Mbio
za kilometa tano, washindi ni Gabriel Garado (Sh 200,000), Deo Lazaro
(Sh 100,000) na Jonas John (Sh 50,000) huku wanawake ni Neema Kisuda (Sh
200,000), Pascalina Silvesta (Sh 100,000) na Christina Yuda (Sh 50,000)
ambao washindi wa kilometa 2.5 wakiwa ni Julita Antony (Sh 100,000),
Editha Gabriel (Sh 50,000) na Magreth Bernado (Sh 25,000).
Wanaume
walikuwa ni Petro Pascal mshindi wa kwanza na kupewa Sh 100,000, Baraka
Sebastian (Sh 50,000), Haji Swalehe (Sh 25,000) huku washindi wengine
400 kila mmoja akipewa Sh 10,000. Baada ya washindi hao kukabidhiwa
zawadi zao, Patel ambaye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Naibu Waziri
Nyalandu, alikabidhi pia medali mbalimbali kwa washindi hao.
Aidha,
alitoa changamoto kwa wananchi hao kuacha tabia ya kuua tembo, bali
wanastahili kulindwa na kuhifadhiwa ili kukuza uchumi na kufungua
milango ya ajira.
Hata
hivyo, baadhi ya washindi walimshukuru Nyalandu kwa kuamua kuanzisha
mashindano hayo maeneo ya vijijini ili kuibua vipaji na kutoa rai kwa
wadau wa riadha mkoani humo pamoja na sehemu mbalimbali kuanzisha klabu
za michezo ya riadha ili kuendeleza vipaji na kuibuavipaji vipya.
Fabiola
ambaye ni mkimbiaji mashuhuri wa riadha na aliyeiletea sifa Tanzania,
alisema awali alikuwa akikimbia mkoani Kilimanjaro, lakini hivi sasa
yupo Singida ambako alihamia Singida Vijijini kwenye Jimbo la Nyalandu,
ndio kwao alipozaliwa na anaona fahari kubwa kuona wilaya hiyo ina
wakimbiaji wengi na ni wazuri, lakini bado wanakabiliwa na changamoto ya
ukosefu wa vifaa kwa ajili ya kufanyia mazoezi.
Fabiola
na wadau wengine wamemwomba Naibu Waziri pamoja na wadau wengine
kushirikiana kwa pamoja ili kuanzisha klabu za michezo ya riadha ili
kuibua vipaji vya wakimbiaji waliopo maeneo ya vijijini.
Alisema
mkoa huo una wanamichezo wengi, lakini hakuna klabu za michezo hali
inayosababisha baadhi ya wanariadha kufanya mazoezi bila ya kuwa na
vifaa maalumu, lakini walimpongeza Nyalandu kwa kuanzisha mashindano
hayo maeneo ya vijijini ili kuibua wanamichezo wengi watakaoweza
kuutangaza mkoa huo pamoja na Tanzania kwa ujumla pale yanapotokea
mashindano ya riadha ya ndani na nje ya nchi.
Chanzo;Habari Leo