Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WATU watatu akiwemo Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Ngimu
katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida, wamekufa na wengine 10
kujeruhiwa baada ya gari aina ya Noah waliyokuwa wakisafiria kuacha
njia na kupinduka katika Kijiji cha Ijanuka, Manispaa ya Singida.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Singida, Dk. Deogratius
Banuba, aliwataja waliopoteza maisha kuwa ni Mkuu wa Shule ya Sekondari
ya Kata ya Ngimu, Tatu Bunku mwenye umri wa kati ya miaka 45 na 50
aliyefia hospitali ya mkoa alipokuwa akipatiwa matibabu, dereva wa gari
hilo, Enock Mbaga (31) mkazi wa Arusha na Hajira Ikhala (21)
mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Ngumbu, mkoani Shinyanga aliyefariki
dunia papo hapo.
Aliwataja waliolazwa hospitali hapo kuwa ni Ramadhani Hamisi (46)
mkazi wa Kijiji cha Sepuka, Adamu Juma (28) mkazi wa Kijiji cha Mgori
na Mariamu Ramadhani (6) mkazi wa Kijiji cha Sepuka.
Wengine ni Asha Saidi (26) Neema Mwiru (44) na Teddy Kesi (24) wakazi
wa Kijiji cha Ngimu, Therecie Pantaleo (14) mkazi wa Kijiji cha
Ilongero, Wilieliamana Elisante (24) mkazi wa Kijiji cha Mang’onyi na
Adamu Kiula (24).
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Mrakibu Mwandamizi wa
Polisi (SSP), Claud Kanyorota, alisema ajali hiyo ilitokea jana, saa
moja asubuhi katika eneo la Kijiji cha Ijanuka.
Alisema uchunguzi wa awali umeonyesha chanzo cha ajali hiyo ni mwendo
kasi wa gari hilo T 227 BLN Toyota Noah uliosababisha tairi la gari
hiyo iliyokuwa na abiria 13 kupasuka na hivyo kupinduka.
Kaimu kamanda huyo alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa waendesha
vyombo vya moto kuwa makini na kuepuka kujaza abiria zaidi ya uwezo wa
vyombo husika pamoja na kuepuka mwendo kasi.
Chanzo:Tanznia Daima