Kaimu
mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Singida, Joseph Sabore
(anayeangalia kamera) akizungumza na maafisa wa shirika lisilo la
kiserikali la Health Actions Promotion Association (HAPA), YMC na
WaterAid Tanzania, ambao wako katika halmashauri hiyo kufanya tathimini
ya mradi wa ushiriki sawa wa wanaume katika afya ya uzazi na ujinsia.
Mradi huo unaotarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi 1.6 bilioni,
unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu na unatarajiwa kufikia
ukingoni Desemba mwaka huu.(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu, Singida
MRADI
wa ushiriki sawa wa wanaume katika afya ya uzazi na ujinsia (TMEP)
unaotekelezwa katika Halmashauri ya wilaya ya Singida,umeanza kuzaa
matunda yanayotarajiwa baada ya asilimia 89 ya wanaume kubadilika na
kuanza kusindikiza wake zao kliniki na vituo vya afya.
Hayo
yamesemwa hivi karibuni na Muuguzi Mkuu wa Halmashauri hiyo,Bertha
Herman wakati akitoa taarifa yake ya ushiriki sawa wa wanaume katika
afya ya uzazi na ujinsia, kwa maafisa wa shirika lisilo la kiserikali la
Health Actions Promotion Association (HAPA),YMC na WaterAid
Tanzania,ambao wanafanya tathimini ya mradi huo wa miaka mitatu
unaotarajiwa kumalizika desemba mwaka huu.
Amesema
katika miaka ya nyuma ambayo ilikuwa imetawaliwa na mfumo kandamizi
(mfumo dume),ilikuwa mwiko kwa mwanaume kumsindikiza mke wake kliniki au
kumsaidia kazi za nyumbani ikiwemo ya kufua nguo za watoto,kuandaa
chakula na kusafisha mazingira ya kaya yao.
Amesema
mfumo huo kwa kiasi kikubwa ulipunguza mawasiliano baina ya mke na mume
na ulijenga utamaduni wa kuwa mwanaume ana haki ya kumpa kipigo kikali
mke pindi anapoona inafaa.
“Baada
ya kuanzishwa kwa mradi huu miaka mitatu iliyopita,mambo yanaendelea
kubadilika kwa kasi kubwa.Kwa sasa si rahisi kusikia mwanaume amempiga
mke wake.
“Wanaume
wametambua kuwa wana wajibu wa kusindikiza wake zao kliniki kwa faida
kwamba wanaweza kujua mapema kama kuna tatizo.Pia wanaume wengi sasa
wanawapeleka watoto wao wachanga kliniki,kuwaogesha na kufua nguo
zao.Kwa ujumla mradi huu umeboresha mno ndoa za wanafamilia
wengi”,alifafanua.
Kwa
upande wake mkazi wa kijiji cha Mtamaa Manispaa ya Singida,Mohammed
Alute amesema elimu waliyoipata kupitia mradi wa TMEP, imesaidia mno
wanandoa kushirikiana katika kutekeleza majukumu yote ya kifamilia
ambayo hapo zamani,aliachiwa mwanamke peke na kuchangia kudhoofisha afya
za akina mama.
“Kwa
upande wangu na kwa kweli kwa wanaume wengi waliopata elimu inayotolewa
na mradi wa TMEP,hatuoni kinyaa kupika chakula,kwenda kiliniki au kufua
nguo za familia.Kumbe mwanamke akisaidiwa kazi za nyumbani,hachakai
wale hazeeki upesi na kwa ujumla ushiriki huu,unaongeza mapenzi zaidi
baina ya wana ndoa”,amesema Alute.
Naye
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Singida,Joseph Sabore
amesema mradi wa TMEP,umeleta mabadiliko makubwa kwa wakazi wa
halmashauri hiyo ambapo sasa wanandoa wanaweza kukaa pamoja na kupanga
utaratibu wa uzazi wa mpango kuliko ilivyokuwa hapo awali.
Amesema
wamejiandaa vema ili kuendeleza mradi huo wakati TMEP itakapoacha
kusimamia utekelezaji wa mradi huo.Elimu na uhamasishaji utaendelezwa
kwa jamii na katika shule za msingi,sekondari na vyuo.
Mradi huo unaotarajiwa kumalizika desemba mwaka huu,unatekelezwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi 1.6 bilioni.
0 comments:
Post a Comment