Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MBUNGE wa Singida
Mashariki, Bw. Tundu Lissu (CHADEMA), amedai Serikali imekuwa ikitoa
taarifa za uongo kwa wananchi juu ya mgawanyo wa madawati katika
halmashauri mbalimbali nchini yaliyotokana na fedha zilizozidi kununulia
rada 'chenchi ya rada'.
Bw. Lissu aliyasema
hayo bungeni Mjini Dodoma jana wakati akichangia Bajeti ya Serikali Kuu
kwa mwaka wa fedha 2014/15. Alisema katika hotuba ya Waziri Mkuu,
jedwali la mgawanyo wa madawati lilionesha Serikali iligawa madawati
93,740 lakini Naibu Waziri alidai madawati hayo hayajatolewa yote.
Alisema katika jedwali
hilo, lilionyesha kulikuwa na mgawo wa madawati hewa 3,048 kwenye Mkoa
wa Singida ikifafanua kila halmashauri ilipewa madawati 508 wakati
hakuna dawati hata moja hivyo ni wazi kuwa wananchi wamedanganywa na
Serikali yao.
Naye Mbunge wa Tumbe,
Bw. Rashid Ally Abdallah (CUF), alisema Bajeti ya Serikali Kuu kwa mwaka
2014/15, haiendani na hali halisi ya maisha ya wananchi kwani haiwezi
kutekelezeka.
Alisema kasi ya ukuaji
uchumi haiendani na mahitaji ya wananchi kutokana na matumizi makubwa
kuliko mapato kama ilivyotokea katika Bajeti ya 2013/14 ambapo Wizara ya
Fedha imeshindwa kutekeleza sera mbalimbali za Serikali.
"Ipo haja ya kujua
tatizo ni nini, Wizara mbalimbali hazipewi fedha wanazoomba kwa ajili ya
kutekeleza mipango mbalimbali... baadhi ya wabunge walishauri vyanzo
vipya vya mapato, mimi naona ushauri huu ni kazi bure kama Serikali
inakosa fedha," alisema.
Aliongeza kuwa,
Serikali haina nidhamu ya matumizi ya fedha kutokana na vitendo vya
rushwa, ufisadi ambavyo ni janga la kitaifa kwenye sekta mbalimbali
ikiwemo ya ujenzi wa miundombinu na utoaji tenda.
"Ripoti ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imeeleza wizi mkubwa wa fedha
katika halmashauri... kama wananchi wanalipa kodi na fedha zinafujwa
kwanini tuendelee kuishauri Serikali kuwa na vyanzo vipya vya mapato,"
alihoji Bw. Abdallah.
Alionesha wasiwasi wake
juu ya ziara za viongozi kutumia fedha nyingi ikihoji sera ya Wizara ya
Mambo ya Nje kutokana na msafara wa Rais kuwa na watu wengi pamoja na
matumizi ya vyombo vya usafiri hivyo alishauri jambo hilo liangaliwe.
"Lazima Wizara iweke
utaratibu kuhusu safari za viongozi vinginevyo kila siku watakuwa
wakitumia zaidi ya bilioni 50...ifahamike watu ambao wanaongozana na
Rais wanakwenda kwa lengo gani," alisema.
Mbunge wa Kisesa, Bw.
Luhaga Mpina (CCM), aliishukia Kamati ya Bajeti kuendelea na vikao vyake
nje ya Bunge wakati wabunge wakijadili Bajeti ya Serikali Kuu.
Alisema lipo tatizo
kubwa la kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania hivyo ni vyema
Serikali ikatoa majibu na kufafanua juu ya hatua zilizochukuliwa hadi
sasa.
0 comments:
Post a Comment