Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Nani atabisha kwamba hakuna jambo linalogusa Wabongo kama elimu?
Au labda tuseme hakuna jambo linalogusa Wabongo kama matokeo ya
mitihani. Ndiyo maana sikushangaa kupokea mapepe kibao wiki hii. Hebu
niwaonyeshe mbili tu.
Yes, Serikali yetu bunifu. Kwa nini tuhangaike
kuinua uwezo wakati tunaweza kushusha viwango? Achana na hawa
wanaharakati wote, ambao kazi yao ni kupinga tu utadhani wanaamka na
kula malimau tu kila asubuhi. Mimi nasema, hongera sana wote waliofaulu
mwaka huu. Hongera kwa kuzaliwa mwaka mwafaka, mwaka wa neema, mwaka wa
mafanikio. Hongera zaidi kwa wizara yetu ya shule pamoja na Baraza la
Vyakihuni kwa kuonyesha njia. Kwa njia hii tunajua Bongo yetu itasonga
mbele kwa kasi sana.
Kwanza kwenye mpira. Miaka mingapi tumelalamika
kuhusu kiwango cha mpira hapa petu? Uongozi mbovu huzaa mpira mbovu. Na
kutokana na ubovu huo, tumepata matatizo sana ya uhaba wa magoli mara
kwa mara. Tunajitahidi kuwafundisha washambuliaji wetu jinsi ya kufunga,
lakini ukweli ni kwamba magoli ni madogo mno. Hivyo, kuanzia msimu ujao
wa ligi kuu na ligi zote chini yake, magoli yatapanuliwa kwa mita tano
zaidi. Nadhani kwa njia hiyo tutaweza kushangilia magoli mengi, potelea
mbali iwapo kwenye mashindano ya kimataifa goli itakuwa dogo, lazima
wajue kwamba mabadiliko ni sisi, sisi ni wabongo na tutabonga na
kuboronga kwa njia zetu wenyewe.
Haya, upande wa fedha pia. Hawa watu wa Hazina
watumie ubunifu badala ya ubanifu. Kama pesa hazitoshi, chapa pesa
nyingi zaidi. Kwa njia hiyo, kila mtu atajisikia akibeba marundo ya
manoti. Hata kama haina thamani ni lazima tushindane na wenzetu wa
Zimbabwe, ambao hatimaye walitumia dola zao milioni moja kwa ajili ya
kununua kilo moja ya sukari. Kila mtu milionea au hata bilionea, wataka
nini zaidi?
Kwa kweli katika sayansi inaitwa sheria ya
utapiamlo ni sheria ya Mungu kabisa. Mlo ukipungua kwa mtoto, tumbo
linaongezeka, linatuna, linang’aa. Na elimu inaweza kuwa vivyo hivyo.
Tena ingawa tunafanya kwa mtindo wetu mwenyewe,
tunaendeleza vizuri sana umoja wa Afrika. Wale wenye sifa ya uaminifu na
kutokomeza utapeli walionyesha njia siku nyingi, yaani Nigeria lakini
wapumbavu wa vyuo vikuu mwisho walikataa kuamini matokeo hayo, hivyo
waliotaka kuingia vyuo vikuu vyao walilazimika kufanya mtihani wa ziada.
Kufuru kabisa na ole wake profesa atakayejaribu huo upuuzi hapa. Kama
mtu amepata cheti, wao ni nani kukihoji?
Baraza la Vihuni juuuuuu! Viwango ziiiiii, kidumu na kudumu.
Duh! Barua hii ilinishtua kidogo, lakini kabla sijaweza kuachana na mshangao wangu, ikaja nyingine.
We Makengeza,
Mimi sijui nifurahie ya mwaka huu au niomboleze ya
mwaka jana. Yaani, baada ya kuletwa hapa kwenye shule ya walimu wawili
na kitabu kimoja, nimejitahidi kwa nguvu zangu zote kuwapatia vijana
wetu angalau misingi michache ya elimu, lakini haiwezekani. Wanapata
kitu labda, lakini mbele ya mitihani lazima wafeli kwa sababu hatuna
uwezo wa kuwapatia zaidi. Sasa mwaka huu, tupo walimu walewale na kitabu
kilekile na hata notisi zilezile, maana utapata wapi zingine lakini
ghafla shule nzima imefaulu. Haiyumkiniki. Sijaongeza juhudi wala
maarifa, maana tangu niombe ualimu nimejitahidi vilevile. Na sioni
kwamba wanafunzi wangu wamebadilika pia. Tena wa mwaka huu walikuwa na
hasira zaidi wakijua watapigwa muhuri wa ujinga tu. Je, wanastahili
kusonga mbele? Labda kwa kuwa na akili, ambayo ikikutana na mazingira ya
kweli ya elimu, lakini kwa hayo waliyoyapata kutoka kwangu na
mwenzangu, mmmmh! Tunaelekea wapi?
Basi kutokana na hayo, nikajikuta natafakari kwa
kina wakati nimefunikwa na giza nene ya eneo letu. Wakati asilimia
sitini ya shule za Kenya zina umeme, kwetu ni asilimia mbili tu ya shule
za vijijini. Ndiyo maana elimu iko hoi kwa koroboi. Lakini angalau tuna
nafasi ya kutafakari.
Sasa, uzee wako lazima unakumbuka enzi zile za
kupiga deki resepsheni. Sijui inaitwaje siku hizi, lakini nimegundua
kwamba tabia za mtu mmoja mmoja zinaakisi tabia za wakubwa wetu na
mifumo yao ya kutufuma bila sisi kuwafumania. Angalia watoto wanavyohaha
barabarani kutafuta wafadhili kwa ajili ya timu yao ya mpira au
mahafali wa darasa la saba. Nani kawafundisha kwamba dunia ni kuombaomba
siyo kufanya kazi? Elimu ya Kujitegemea siyo kujiegemea iliishia wapi?
Hata ule mpango wa maskauti wa kufanya kazi ndogondogo ili walipwe kwa
ajili ya mipango yao iliishia wapi? Nani kawatonya umatonya?
Haya, hata katika elimu mambo hayo ya kuwangia viwango yalianza
leo? Tangu zamani sote tumethamini sura ya elimu, badala ya elimu
yenyewe. Zamani ilitosha kunawa vizuri kwa uso wa kawaida, yaani kusoma
kwa bidii chini ya uangalizi wa walimu wanaofundisha kwa bidii ndani ya
mazingira wezeshi. Nakumbuka, maana hata mimi nilisoma wakati ule.
Lakini hata wakati ule, bado wanafunzi wengi walijali sura ya elimu tu,
siyo elimu yenyewe maana lengo lilikuwa cheti siyo zaidi ya hapo.
Haya, sura ya elimu ikaanza kuota vipele kutokana
na sababu mbalimbali. Maarifa ikapungua na wengi walikosa vyeti ndipo
ilibidi kutafuta sabuni za kuua vijidudu vilivyoanza kujitokeza. Badala
ya kuoga vizuri, watu walitegemea sabuni itafanya kazi peke yake. Sabuni
hii kwa lugha ya kitaalamu iliitwa sabuni twisheni. Na wengine walibuni
sabuni kali zaidi iliyoitwa sabuni akademiki. Ndiyo maana tulisikia
kwamba watu wengine walipata fasticlasi ya vidato, kisha wakala disko
baada ya mwaka mmoja chuoni kutokana na kukosa sabuni hiyo (ingawa
nasikia hata kule siku hizi sabuni hizi zimetapakaa).
Kutokana na sabuni hizo pia, Serikali yetu kufuru
iliweza kubuni mpango wa viwango panuka, badala ya viwango pandisha.
Kila mtu alitakiwa kuoga hata maji yakiwa machafu namna gani au hata
kukosekana kabisa, ili mradi wanakubali kununua sabuni twisheni na wao.
Wasipokuwa na uwezo wa kupata hiyo sabuni potelea mbali. Wenye sabuni
ndiyo wenye zabuni za kujaza nafasi za juu.
Lakini mambo siyo rahisi kivile. Wasio na sabuni
walianza kuwashwa sana, ngozi zao zikaharibika hadi wakaanza kudai elimu
ya kweli na wao. Ndipo hapo tumekuja na mikorogo kabisa. Mtu anaweza
kuwa hana maji, hana sabuni, hana chakula bora, lakini ili mradi
resepsheni inapigwa deki. Nani atajua na ataweza kwenda kujinadi popote?
Cheti ni mkorogo, ndiyo maana unaona watu wana sura ya Mirinda, lakini
akili ya Pepsi.
Ndiyo maana nawahurumia wanafunzi wangu wa huko
nyuma. Kama suala ni mkorogo tu, kwa nini pepa zao zisisahihishe upya
ili na wao waingie katika ufalme wa mbingu.
Lakini mwisho, nawapa pole wanafunzi wa mwaka huu
pia. Muwe mmebebwa na daladala ya ‘T111BRN’ au la, mustakabali wa nchi
yetu uko mikononi mwenu.
Ndiyo. Siyo tu kwa sababu ambazo tumezizoea kwamba
sura ya elimu itajenga sura ya ghorofa au daraja au kutibu sura ya
magonjwa. Bali vizazi vitakavyofuata vitaweza kupata au kukosa nafasi
kutokana na maisha yenu. Kwa matokeo kama haya, wengi mtaweza hata
kuomba masomo ya nje. Iwapo nyinyi na Fasticlasi yenu (siyo First Class)
mtaonekana katika vipimo vingine kwamba hamjui, mitihani ya Bongo
itadharauliwa moja kwa moja. Na hata humu, nani atawaajiri mkorogo
ukitambulika?
Mwalimu mkereketwa.
Na mimi pia nikabaki natafakari ndani ya giza
nene. Twafunga goli au twajifunga? Kupanua goli ndiyo suluhisho.
Tukichapa pesa nyingi, mwisho si itaonekana feki? Sura ya Mirinda
itaficha daima akili ya Pepsi?
Chanzo:Mwananchi