WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUWADHIBITI MAKANJANJA

Na Nathaniel Limu, Singida
KLABU za waandishi wa habari nchini, zimetakiwa kuweka utaratibu madhubuti wa kuwadhibiti watu wanaofanya kazi ya uandishi wa habari bila kuwa na taaluma ya uandishi wa habari, maarufu kama makanjanja.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida, Yahaya Nawanda, wakati akifungua mkutano mkuu wa Katiba wa Klabu ya Waandishi wa Habari, Mkoa wa Singida, uliofanyika Mjini Kiomboi.

Nawanda alisema kwamba, kumekuwapo na wimbi kubwa la watu kujiingiza kwenye uandishi wa habari bila kuusomea na kwamba, hali hiyo inasababisha ukiukwaji wa maadili katika tasnia hiyo.

Pia alisema kwamba, kitendo cha watu hao kujiingiza katika taaluma hiyo, kinakuwa chanzo cha uwepo wa habari zilizopotoshwa kwa kuwa wahusika hawajui miiko na maadili ya uandishi wa habari.

“Taaluma ya habari ni taaluma muhimu sana duniani, huwezi kujiingiza katika taaluma hii na kuanza kuandika mambo ambayo huyajui na kama unayajua unayaandika bila kufuata maadili ya taaluma yenyewe.

“Hili ni kosa kubwa ambalo haliwezi kuvumiliwa na mtu yeyote na ili kuondokana nalo, lazima kuna haja ya uwepo wa nguvu za pamoja kutoka kwa kila anayehusika,” alisema Nawanda.

Kutokana na hali hiyo, alisema kuna haja kwa klabu za wanahabari kuweka utaratibu wa kudhibiti tatizo hilo, ili kuhakikisha kuwa taaluma ya habari inakubalika na kuheshimika na jamii kutokana na umuhimu wake.

Alisema kuwa, kitendo cha kuwaacha baadhi ya watu wasiokuwa na taaluma waendelee kuitumikia taaluma hiyo, kunaifanya kazi hiyo ionekane kuwa ni kazi inayoweza kufanywa na mtu yeyote tena kwa ubabaishaji.

Klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Singida, yenye wanachama 25, hivi sasa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002, imefanya marekebisho ya katiba yake, ili iweze kuendana na wakati.

Pamoja na malengo hayo, marekebisho yamefanywa ili kuziba mianya ya watu wanaotaka kuitumia taaluma hiyo vibaya, kwa kuwa wanaweza kuhatarisha amani ya nchi.
Chanzo: Mtanzania

WAWILI WA FAMILIA MOJA WAPOTEZA MAISHA MKOANI SINGIDA BAADA YA KUGONGWA NA GARI.




Kamanda wa polisi mkoa wa Singida Linuys Sinzumwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) ya ajali iliyoua vijana wawili ndugu. (Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Vijana wawili wa familia moja wakazi wa kijiji cha Mwankoko manispaa ya Singida wamegongwa na gari aina ya Land Rover na kufariki dunia papo hapo.
Vijana hao ni Seleman Juma (42) na Mohammede Juma (33).
Kamanda wa polisi mkoa wa Singida Linus Sinzumwa amesema vijana hao wamegongwa Agosti 29 mwaka huu katika barabara ya Singida mjini – Kindaa eneo la kijiji cha Mwankoko.
Amesema siku ya tukio, vijana hao wakiwa na baskeli zao wakitokea kitongoji cha Isomia kata ya Mwankoko wakielekea Singida mjini, waligongwa na Land Rover T.501 ASG ambayo iliwafuata hadi nje ya barabara.
Akifafanua, Sinzumwa amesema Land Rover hiyo iliyokuwa ikiendeshwa na dereva ambaye hadi sasa jina lake halijafahamika, liliacha barabara na kuwafuata vijana hao ambao walikuwa nje ya barabara na kuwagonga na kusababisha vifo vyao papo hapo.
Sinzumwa amesema tayari wameanzisha msako mkali wa kumsaka dereva huyo akamatwe na kisha kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
Katika hatua nyingine, Kamanda huyo amesema kuwa jumla ya waumini wa kiislamu wanne, wanashikiliwa kwa tuhuma ya kugoma kushiriki zoezi la sensa.
Amewataja waumini hao kuwa ni Jidawi Ramadhani (31), Hussein Juma (23), Saidi Maulid (19) na Hamisi Shaban (18) wote ni wakazi wa Singida mjini.
Amesema watuhumiwa hao wamekamatwa baada ya kugoma kutoa taarifa zao kwa makarani wa sensa.
Chanzo: Mo blog

RC SINGIDA AAGIZA ZANAHATI IPEWE WAHUDUMU WENYE SIFA

 
Na Nathaniel Limu, Singida
MKUU wa Mkoa wa Singida, Dk. Parseko Kone, amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Iramba ashirikiane na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri kuhakikisha Zahanati ya Kitongoji cha Kipamba iliyopo Kata ya Mwangeza inakuwa na wahudumu wenye sifa mapema iwezekanavyo.

Agizo hilo lilitolewa mjini hapa juzi baada ya kulalamikiwa na wakazi wa Kitongoji cha Kipemba kwamba zahanati yao toka imalizike kujengwa zaidi ya mwaka moja haina muhudumu mwenye taaluma.

Imedaiwa kuwa kwa kipindi chote hicho, kuna vijana wawili wenye elimu ya msingi na ambao hawajasomea taaluma ya utoaji huduma ya afya ndio wanaotoa huduma.

“Haingii akilini zahanati ambayo imejengwa kwa msaada na Shirika la International Outreach Africa la nchini Marekani, imebaki bila mhudumu wa afya mwenye sifa stahiki. Wafadhili hawa wakija leo, hivi watatuelewaje,” alihoji Dk. Kone.

Kutokana na hali hiyo, aliagiza wahudumu wenye sifa stahiki, wapangwe haraka iwezekanavyo katika zahanati hiyo.

Kuhusu malalamiko ya ukosefu wa vitanda katika mabweni mawili ya Shule ya Msingi ya Munguli, aliagiza taratibu zifanywe haraka na hatimaye mabweni hayo yawe na vitanda vyitakavyokidhi mahitaji.

Baadhi ya wakazi wa Kitongoji cha Kipamba, wamedai kero zao nyingi hazipatiwi ufumbuzi wa kudumu kwa madai Mbunge wao, Salome Mwabu, hajawatembelea toka amechaguliwa kushika wadhifa huo.
Chanzo: Mtanzania

Wanahabari Watakiwa Kufuata Maadili Ya Uandishi Kuepuka Migogoro




MWENYEKIT wa Klabu ya wanahabari mkoa Singida SINGPRESS) Seif Takaza akizungumza kabla ya kumkaribisha Yahaya Nawanda, mkuu wa wilaya ya Iramba kufungua mkutano maalum wa kufanyia marekebesho KATIBA ya klabu hiyo(kushoto ni kuu huyo wa Wilaya).
Mkuu wa Wilaya ya Iramba Yahaya Nawanda, akifungua mkutano maalum wa klabu ya waandishi wa habari Mkoa Singida(Singpress) ulioandaliwa kwa ajili ya kuifanyia marekebisho katiba ya klabu,kuanzia kulia ni makamu Mwenyekiti wa Singpress, Jumbe Ismaely, anayefuata ni mwenyekiti wa Singpress Seif Takaza.



Mkuu wa wilaya Iramba Yahaya Nawanda (wa pili kulia - mwenye miwani),akiwa katika picha ya pamoja na wanahabari wa mkoa Singida, muda mfupi baada ya kufungua mkutano maalumu wa Katiba ya Singpress.





Na: Elisante John, Singida



Mkuu wa Wilaya Iramba Mkoani Singida, Yahaya Nawanda, ametoa wito huo alipofungua mkutano mkutano maalumu wa Katiba ya Klabu ya wanahabari mkoa Singida (SINGPRESS), uliofanyika ukumbi wa halmashauri, mjini Kiomboi.



Alisema kuna faida nyingi kwa kutii na kuzingatia katiba watakayoifanyia marekebesho, mojawapo ikiwa ni kuimarisha amani na utulivu ndani ya kikundi, nchi au sehemu yoyote ile kwa watu walioamua kushirikiana pamoja.




Pia alihimiza wanahabari hao waende sawa na mabadiliko yatakayofanyika ili kujenga umoja na upendo miongoni mwao na wadau wengine wa habari Mkoani Singida.




Aliwataka wasiingize ushabiki katika utendaji wao wa kazi za kila siku, kuepusha tasnia ya habari kuonekana kazi isiyofaa katika jamii.


WAHADZABE MKOANI SINGIDA WABAKIA NYUMBANI KUHESABIWA BAADA YA KUPEWA NYAMAPORI.




Mkuu mkoa wa Singida, Dk.Parseko Kone akimkabidhi boksi la chakula cha msaada mwenyekiti wa kitongoji cha Kipamba, Agostino (mwenye shati jeupe).Chakula hicho kimetolewa ili jamii hiyo isiende porini kuwinda ibaki kwenye kaya zao kuhesabiwa.(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Jamii ya Kihadzabe inayoishi katika kijiji cha Munguli kata ya Mwangeza jimbo la Iramba mashariki, imejitokeza kwa wingi kushiriki sensa ya watu na makazi iliyoanza Agosti 26 mwaka huu.
Jamii hiyo ilijitokeza baada ya ‘kupewa motisha ya msaada wa nyamapori ya kutosha na vyakula mbalimbali.
Jamii hiyo iliiomba serikali ya mkoa wa Singida nyamapori ya kutosha ili isiende porini kuwinda wakati wa sensa.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Parseko Kone, amesema jamii hiyo ambayo chakula chake kikuu ni nyamapori, matunda pori, asali na mizizi ya miti pori, kabla ya kuanza kuhesabiwa, iligawiwa nyama ya nyumbu wakubwa watatu na nusu na mbuzi mmoja.
Amesema kitendo hicho kilisababisha jamii hiyo isiende kuwinda porini kama kawaida yao, ilibaki kwenye kaya zao kusubiri makarani wa sensa.
Mkuu huyo wa mkoa ameongeza kusema kuwa iliwalazimu kuwakubalia ombi lao la msaada wa chakula na nyama pori ili wabaki kwenye kaya  na kambi zao, ili waweze kuhesabiwa.
Jamii hii ilibaki kwenye kaya zao na ilijibu kwa ufasaha mkubwa maswali yote iliyokuwa ikiulizwa na makarani.
Hata hivyo, kulijitokeza tatizo dogo la mawasiliano, kwa maana ya kuwa baadhi ya Wahadzabe hawajui kuongea Kiswahili, kwa hiyo walitafutwa wakalimani na walifanya kazi vizuri ya kutafsiri na hapo madodoso yalijibiwa ipasavyo.
Dk.Kone alisema pamoja na nyamapori hiyo, pia walitoa msaada wa magunia mawili ya unga wa mahindi na tani moja ya chakula kilichotolewa msaada na shirika lisilo la kiserikali la Outreach International Africa lenye makazi yake nchini Marekani.
Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa katika sehemu zingine za mkoa, mambo yamekwenda vizuri mno.
Kulikuwepo na mapungufu madogo madogo nayo yalirekebishwa bila kuleta athari yo yote.
Dkt. Kone ametumia fursa hiyo kuwashukuru wakazi wa mkoa wa Singida kwa kujitokeza kwa wingi na kutoa ushirikiano wa dhati kwa makarani wa sensa.

HAYA NDIO MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA MIONGONI MWA JAMII YA WAHADZABE MKOANI SINGIDA.


Mkazi wa kitongoji cha Kipamba kata ya Mwangeza ambaye amekataa kutaja jina lake akiwa kwenye nyumba yake ya kuishi na familia yake.  
 Mkazi wa kitongoji cha Kipamba kata ya Mwangeza wilaya ya Iramba ambaye hakuweza kujulikana jina lake mara moja akiomba alipwe fedha za kumpiga picha. 
(Picha na Nathaniel Limu).

MTENDAJI WA KIJIJI AFUNGWA KWA KUOMBA RUSHWA

 
Na Petro Sungi, Singida
AFISA mtendaji wa Kijiji cha Misuke kilichopo katika Wilaya ya Singida, Omary Mandi amehukumiwa kwenda jela miaka mitatu, baada ya kukutwa na hatia ya kuomba na kupokea rushwa.

Hukumu hiyo ilitolewa Agosti 21, mwaka huu na Hakimu Mkazi wa Mahakama mkoani hapa, Ruth Massam mbele ya Ofisa Uchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mkoani hapa (TAKUKURU), Wilson Ntiro.

Katika hukumu hiyo mtuhumiwa alikutwa na hatia ya kuomba na kupokea rushwa mara mbili na kuhukumiwa kwenda jela miaka mitatu.

Awali Ofisa wa TAKUKURU alidai kuwa mtuhumiwa huyo alitenda makosa hayo Novemba 17, 2010 kwa kupokea rushwa ya Sh 40, 000 wakati Novemba 10 alipokea rushwa ya Sh 75, 000 kutoka kwa Mwenyekiti wa Misuke, Joseph Dwash.

Mtendaji huyo alidaiwa kuwa alimdanganya Dwash kuwa anaweza kumsaidia, ili aendelee kuwa mwenyekiti. Kesi hiyo ilifunguliwa Januari 31, mwaka huu na TAKUKURU.
Chanzo: Mtanzania

RC KONE AWATAKA WALIOVAMIA PORI LA WAHADZABE KUONDOKA


Mwandishi wetu, Singida Yetu 
SERIKALI imewataka watu waliovamia pori wanaloishi wananchi wa kabila la wahadzabe mkoani Singida kuondoka mara moja kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao.
Pori  hilo lililopo katika Kijiji  cha Munguli wilaya  Mkalama umbali wa kilomita 120  kaskazini mashariki mwa mji wa Singida, limevamiwa na wahamiaji  kutoka Arusha, Manyara na  Shinyanga  ambao wamefyeka na kuchoma  moto kwa ajili ya  kilimo na ufugaji.
                                                                                 
Akizungumza  baada ya kuwatembelea wananchi  hao  maarufu kama watindiga Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Parseko Kone amesema serikali haiwezi kuvumilia  kuona uharibifu wa mazingira ukiendelea katika pori hilo lililotengwa na kuhifadhiwa kwa mujibu wa sheria.

Dokta Kone amemwagiza mkuu wa wilaya ya Mkalama na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, kuwaondoa wavamizi hao kwa nguvu iwapo hawataondoka kwa hiari yao.


Mbali na wavamizi, pori hilo linakaliwa na wahadzabe zaidi 400  ambao hujishughulisha na  uwindaji na kula vyakula  vya  asili ambavyo ni nyama pori, asali, matunda pori na mizizi
Blogzamikoa

Picha Mbalimbali Za Katibu Mkuu wa Chadema Dk Wilbrod Slaa Kwenye Mkutano wa Kuwashukuru Wananchi wa Jimbo la igunga

  Katibu
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod
Slaa, akisalimiana na aliyekuwa mgombea wa ubunge jimbo la Igunga katika
uchaguzi mdogo mwaka jana, kupitia Chadema, Mwalimu Joseph Kashindye,
walipokutana katika mkutano wa kuwashukuru wananchi wa jimbo hilo kwa
ushiriki wao katika kesi ya uchaguzi wa jimbo hilo, ambayo Chadema
kiliibuka mshindi, uliofanytika kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Igunga
 Katibu
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa
akikumbatinana na Mbunge wa Maswa Mashariki, Slyvester Kasulumbai,
walipokutana katika mkutano wa hadhara wa kuwashukuru wananchi wa jimbo
la Igunga kwa ushiriki wao katika kesi ya uchaguzi wa jimbo hilo, kwenye
Uwanja wa Sokoine mjini Igunga juzi.
Kutokana
na kilichoelezwa kuwekwa kwa lami chini yakiwango katika mlima Sekenke
mkoani Singida, imeharibika vibaya kama inavyoonyesha pichani magari
yakipita kwa shida baada ya lami hiyo kubomoka kwa kipindi kifupi tangu
iwekwe, kama ilivyokutwa jana.Picha na Joseph Senga

Katibu Mkuu wa Chadema,Dk. Willibrod Slaa Aung'uruma igunga



 Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod
Slaa akiwahutubia wananchi wa mji wa Igunga na vitongoji vyake, katika
mkutano wa hadhara wa kuwashukuru wananchi kwa ushiriki wao katika
kufanikisha kesi ya uchaguzi wa jimbo hilo, uliofanyika kwenye Uwanja wa
Kumbukumbu ya Sokoine mjini Igunga.
 Aliyekuwa mgombea wa jimbo la Igunga
katika uchaguzi mdogo mwaka jana, kupitia Chadema, mwalimu Joseph
Kashindye na aliyekuwa meneja wa kampeni,  Slyvester Kasulumbai,
wakiwasili kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mjini  Igunga, ambako
kulifanyika mkutano wa hadhara.Picha zote na Joseph Senga)


NYAMAPORI KUTUMIKA KUIHAMASISHA JAMII YA WAHADZABE KUSHIRIKI SENSA YA WATU NA MAKAZI.

Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt.Parseko Kone (mwenye suti ya bluu) akisalimiana na mzee wa Kihadzabe mkazi wa kijiji cha Munguli kitongoji cha Kipamba ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja.
Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Parseko Kone akihamasisha jamii ya Kihadzabe wa kitongoji cha Kipamba kushiriki sensa ya taifa inayotarajiwa kufanyika nchini kote Agosti 26 mwaka huu.
Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Parseko Kone (mwenye suti ya bluu)akimkabidhi msaada wa chakula Mwenyekiti wa kitongoji cha Kipamba kijiji cha Munguli Edward Mashimba (mwenye shati jeupe).
Maboksi ya msaada wa chakula kilichotolewa na shirika lisilo la kiserikali la International Outreach International na nchini Marekani. Chakula hicho kina uzito wa zaidi ya tani moja.
Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Parseko Kone, akiwa amempakata mtoto wa Kihadzabe aliyebatizwa jina lake la Kone. Mtoto huyo alizaliwa asubuhi ya siku Dkt. Kone alipofanya ziara ya kwanza ya kikazi katika kijiji hicho miaka sita iliyopita. Nyuma ya mtoto huy ni Mkuu wa wilaya ya Singida Mwalimu Queen Mlozi.
Baadhi ya akina mama wa Kihadazbe waliohudhuria mkutano wa hadhara ambao mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Parseko Kone, aliutumia kuhamasisha jamii ya Kihadzabe na nyingine kushiriki sensa inayaotarajiwa kufanyika Agosti 26 mwaka huu. (Picha zote na Nathaniel Limu).
Na.Nathaniel Limu.
Serikali ya wilaya mpya  ya Mkalama mkoani SIngida imeahidi kutoa nyama pori ya kutosha kwa Wahadzabe wa kitongoji cha Kipamba kata ya Mwangeza, ili waweze kushiriki sensa ya kitaifa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika nchini kote Agosti 26 mwaka huu.
Kwa mujibu wa mkuu wa wilaya hiyo Edward Ole Lenga, msaada wa nyama ya wanyama pori hiyo, utasaidia jamii ya Wahdzabe kubaki kwenye kaya zao kipindi chote cha sensa.
Akizungumza muda mfupi kabla ya kumkaribisha mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Parseko Kone, awahamasishe Wahadzabe na wakazi wengine wa kata ya Munguli, kushiriki sensa.
Lenga amesema msaada huo wa  nyama pori, unatokana na ombi liliotolewa na jamii hiyo ambayo chakula chake kikuu ni nyamapori, mizizi, matunda pori na asali.
Akifafanua amesema Wahdzabe hao wanaokadiriwa kufikia 227, wametoa ombi hilo ili wakati wote wa sensa wasiende porini kuwinda na badala yake wabaki kwenye kaya zao wakisubiri kuhesabiwa.
Mkuu huyo wa wilaya amesema ombi hilo tayari limeshakubaliwa na maandalizi yote muhimu ya kuwinda wanyama pori siku moja kabla ya siku ya sensa, yamekwisha kamilika.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa Dkt. Kone, ametoa msaada wa chakula chenye uzito wa zaidi ya tani moja, ambacho kitakidhi mahitaji kuanzia sasa hadi zoezi la sensa litakapokamilika.
Amesema kwa hali hiyo, kipindi chote cha sensa, hapatakuwepo na haja kwenda porini kutafuta wanyama pori, asali, matunda pori au mizizi.
Katika hatua nyingine, amewataka wahakikishe kila mmoja anahesabiwa mara moja tu, kwa madai kuwa wakishafahamika idadi yao na hali zao za maisha, itasaidia serikali kujipanga namna bora  ya kuwahudumia na kuwaletea maendeleo.
Wakati huo huo Dk. Kone, amesema pamoja na kunid la wawindaji, pia makundi mengine ya wavuvi, wachungaji wanaohama hama, watafutaji madini na baadhi ya wakulima ambao wana mashamba yaliyo mbali na makazi au makambi yao ya kawaida, warejee kwenye kaya na makambi yao ili waweze kuhesabiwa siku ya sensa.
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa