Mwandishi wetu, Singida Yetu
SERIKALI imewataka watu waliovamia pori wanaloishi wananchi wa kabila la wahadzabe mkoani Singida kuondoka mara moja kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao.
Pori hilo lililopo katika Kijiji cha Munguli wilaya Mkalama umbali wa kilomita 120 kaskazini mashariki mwa mji wa Singida, limevamiwa na wahamiaji kutoka Arusha, Manyara na Shinyanga ambao wamefyeka na kuchoma moto kwa ajili ya kilimo na ufugaji.
Akizungumza baada ya kuwatembelea wananchi hao maarufu kama watindiga Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Parseko Kone amesema serikali haiwezi kuvumilia kuona uharibifu wa mazingira ukiendelea katika pori hilo lililotengwa na kuhifadhiwa kwa mujibu wa sheria.
Dokta Kone amemwagiza mkuu wa wilaya ya Mkalama na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, kuwaondoa wavamizi hao kwa nguvu iwapo hawataondoka kwa hiari yao.
Mbali na wavamizi, pori hilo linakaliwa na wahadzabe zaidi 400 ambao hujishughulisha na uwindaji na kula vyakula vya asili ambavyo ni nyama pori, asali, matunda pori na mizizi
Blogzamikoa
0 comments:
Post a Comment