Home » » DIALLO, GUNINITA WACHUKUA FOMU CCM

DIALLO, GUNINITA WACHUKUA FOMU CCM



Na Waandishi Wetu, Dar na mikoani


*Wana CCM wamuonya Lembeli Shinyanga
MCHUANO mkali wa kuwania nafasi za wenyeviti wa CCM wa Mikoa, Tanzania Bara, umeanza.

Katika mchuano huo, baadhi ya vigogo wa CCM katika mikoa mbalimbali wameanza kuchukua fomu ili kutetea nafasi zao na wengine kuwang’oa wenzao walioko madarakani.

Katika Mkoa wa Mwanza, Mbunge wa zamani wa Ilemela, Anthony Diallo (CCM), jana alichukua fomu kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Mwanza.

Wakati Diallo alichukua fomu mkoani humo, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita, naye alichukua fomu ili kutetea nafasi yake hiyo.

Wakati hayo yakiendelea, mkoani Shinyanga nako mchuano mkali unatarajia kuwa kati ya Mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM) na Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Shinyanga, John Mgeja.

Katika Mkoa wa Mwanza, Diallo, ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, (NEC), alichukua fomu hiyo jana saa mbili asubuhi na alikabidhiwa na Katibu Msaidizi wa CCM, Mkoa wa Mwanza, Zubeda Mbaruku, katika makao makuu ya CCM, Mkoa wa Mwanza.

Akizungumza baada ya kuchukua fomu hiyo, Diallo alisema amechukua fomu hiyo kama sehemu ya kutimiza wajibu wake wa kidemokrasia na aliahidi kuwatumikia kikamilifu wana CCM, Mkoa wa Mwanza.

"Mimi ni kiongozi wa watu, naijua CCM, kwa hiyo, nitakaposhinda, nitahakikisha nawaunganisha wana CCM wote bila kubagua na nitapambana na ubaguzi pamoja na makundi ndani ya chama chetu, ili kukifanya kiendelee kuaminika kwa wanachama na wananchi wa kawaida," alisema Diallo.

Wakati Diallo akichukua fomu, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Mwanza anayemaliza muda wake, Clement Mabina, naye alichukua fomu ili kutetea nafasi yake hiyo.

Mbunge wa Kwimba, Shanif Hiran Mansoor (CCM), yeye alichukua fomu ili kutetea nafasi yake ya Mweka Hazina wa chama hicho, Mkoa wa Mwanza kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Wakati mchuano ukiwa hivyo jijini Mwanza, jijini Dar es Salaam nako mchuano umeanza, baada ya Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita, kuchukua fomu ya kutetea nafasi yake hiyo jana.

Guninita alikabidhiwa fomu hiyo jana na Katibu wa CCM, Mkoa wa Dar es Salaam, Abilahi Mihewa, makao makuu ya chama hicho, Mkoa wa Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa kuchukua fomu hiyo, Guninita alisema akifanikiwa kuendelea na nafasi hiyo, atajenga uchumi wa kisasa na kiusalama kupitia miradi mbalimbali ya chama hicho.

Alisema pia kwamba, anatarajia pia kujenga mazingira ya kukuza uchumi kwa kuimarisha miradi yote ya chama.

Pia alijigamba kwamba, katika kipindi cha miaka mitano alichokuwa madarakani kwa kushirikiana na viongozi wenzake mkoani Dar es Salaam, amefanikiwa kutambua mali zote za chama, vikiwemo viwanja 300 na kwamba kati ya viwanja hivyo, 150 vimepata hati kwa ajili ya kupata uwekezaji unaoeleweka.

“Nimekuwa mwenyekiti kwa miaka mitano, nimejipima na kuona naweza kuwaongoza wana CCM katika kipindi kingine, ninawaomba na wanachama wapime uwezo wangu kama ninafaa tena kuonyesha uwezo wangu.

“Kikubwa tunachotaka ni kuhakikisha tunajenga uchumi wa kisasa na kiusalama kwa mali za CCM, vikiwemo viwanja.

Kuhusu changamoto za vyama vya upinzani, kikiwamo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho kinaaminika kuungwa mkono zaidi na vijana, alisema:

“Kigezo cha chama chochote cha siasa kukubalika ni ushindi katika chaguzi zinazoshirikisha vyama vyote, kwa hiyo, CCM bado tuko juu, maana katika majimbo ya Dar es Salaam, tuliweza kushinda viti sita kati ya vinane, udiwani tulifanikiwa kuchukua kata 77 kati ya 90, sasa kwa nini tusiseme bado tunakubalika?” alihoji Guninita.

Kwa upande wake, Mihewa aliwaonya wana CCM wanaoomba nafasi za kugombea katika Mkoa wa Dar es Salaam, wahakikishe wanafuata sheria na kanuni zilizowekwa na chama chao.

“Nawasihi wagombea wote wasifanye kampeni za aina yoyote, wasubiri mpaka siku ya uchaguzi, ni marufuku kukutana, kuwakusanya wapiga kura na kuwasalimia, wasubiri siku yenyewe watakapokutana na wajumbe, atakayebainika akikiuka taratibu, ajue vikao vitamwengua mara moja” alionya Mihewa.

Wakati Dar es Salaam na Mwanza mchuano ukianza, mvutano mkali unatarajiwa pia mkoani Shinyanga, ambako Mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM), anatarajia kupambana na Mwenyekiti wa CCM, Mkoa huo, Khamis Mgeja, ingawa hadi sasa hakuna aliyechukua fomu kuwania nafasi hiyo.

Baada ya Lembeli kutangaza hivi karibuni, kwamba atamng’oa madarakani Mgeja, baadhi ya viongozi wa chama hicho mkoani humo ambao pia ni wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM, Mkoa wa Shinyanga, wamemuonya mbunge huyo na kumtaka asiingilie uhuru wa wajumbe wa mkutano mkuu, kwa kuwa ndiyo wenye uwezo wa kuwang’oa viongozi wa ngazi ya mkoa.

Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti mjini hapa jana, wajumbe hao wamesema kitendo cha Lembeli kusema atamng’oa Mgeja hakiwezi kukubalika, kwa kuwa wajumbe wa mkutano mkuu ndiyo wenye uwezo wa kuwaondoa viongozi wao madarakani.

Mmoja wa wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho, Mkoa wa Shinyanga, Charles Shigino, alisema yeye na wenzake hawawezi kukaa kimya kwa kuwa kauli ya Lembeli inaonyesha anataka kuwachagulia kiongozi anayetakiwa kukiongoza chama hicho mkoani hapa.

“Kwa ujumla wajumbe wa mkutano mkuu hawakutegemea kusikia kauli hiyo kutoka kwa Lembeli, kwa sababu kauli hiyo inaingilia uhuru wa wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM mkoa wa Shinyanga.

“Suala la kupigiwa kura na kushindwa au kushinda siyo kazi ya mgombea, hiyo ni kazi ya wapiga kura ambao ni wajumbe, wala siyo Lembeli.

“Sasa sisi kama wajumbe, tunamuonya Lembeli aache tabia ya kujitangaza eti anakuja kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kumng’oa kigogo, hivi anataka kumng’oa kigogo huyo kwa umuhimu gani alionao?

“Haya majigambo hayana tija kwa sababu wapiga kura ndio wenye uamuzi na wenye mamlaka ya kumpa nafasi hiyo, sasa kwa kauli yake hiyo, ina maana Lembeli tayari ndiye Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Shinyanga.

“Lembeli ni Mwanachama wa CCM na ni Mbunge wa Kahama, kwa hiyo, ni vema kwanza ajue wazi kuwa hana uwezo wa kumng’oa kiongozi, kwani kazi hiyo ni ya wajumbe na wapiga kura tu na si vinginevyo, hivi ameshaongea na kila mjumbe na kumhakikishia kwamba atampa kura za kumng’oa kigogo huyo anayemtaja?

“Namuomba ndugu yangu Lembeli pamoja na wagombea wengine katika mkoa huu wa Shinyanga, waanze kuweka maji kichwani na kusubiri kunyolewa na wapiga kura ambao ni wajumbe na siyo Lembeli,” alisema Shingino.

Mbali na kiongozi huyo, mwingine aliyekerwa na kauli ya Lembeli ni Mwenyekiti wa CCM, Kata ya Shinyanga Mjini ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM mkoani hapa, Rajabu Makubuli, aliyesema Lembeli anahitaji msaada ili ajue namna mchakato wa uchaguzi unavyokwenda.

“Huyu jamaa ni mbunge, lakini inaonekana hajui taratibu za uchaguzi zinavyokwenda, kwa hiyo, nadhani kuna kila sababu ya kumweleza namna uchaguzi unavyofanyika, ingawa kwa kauli zale hizo wajumbe sasa wameshaanza kumjua tabia yake,” alisema Makubuli.

Naye Peter Lubinza ambaye pia ni Mjumbe wa CCM, Mkoa wa Shinyanga, alisema Lembeli alikosea kukaririwa na vyombo vya habari, akitamba kuwa atahakikisha anamng’oa Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Shinyanga.

“Kutokana na kauli yake anapaswa kutambua kuwa CCM na hasa wajumbe hivi sasa ni waelewa sana, wanajua kuchagua pumba na mchele” alisema.

“Yeye angekuja na hoja ya kujenga chama, hasa wakati huu ambao kinakabiliwa na changamoto nyingi za kisiasa, ikiwemo ya ushindani unaokikabili, badala yake anakuja na porojo zake kwamba anakuja kumng’oa kigogo, ngoja tumsubiri aje,” alisema Lubinza.

Chanzo: Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa