Home » » MKUU WA WILAYA SINGIDA AKATAA KUINGILIA KESI YA MTUHUMIWA WA KUSAMBAZA VIPEPERUSHI VINAVYOHAMASISHA WAISLAMU KUTOSHIRIKI SENSA YA TAIFA.

MKUU WA WILAYA SINGIDA AKATAA KUINGILIA KESI YA MTUHUMIWA WA KUSAMBAZA VIPEPERUSHI VINAVYOHAMASISHA WAISLAMU KUTOSHIRIKI SENSA YA TAIFA.





Mkuu wa wilaya ya Singida Queen Mlozi (anayeangalia kamera) akiwa na viongozi wa dini ya kiislamu waliokwenda kumwomba asaidie kumnasua Issa Mohammed Msukuya dhidi ya kesi inayomkabili ya kugawa vipeperushi vya kuzuia waislamu kushiriki sensa.
Imam masjid Salafiy Singida mjini Abdurahman Hassan akiwa na wenzake ofisini kwa mkuu wa wilaya ya Singida. (Picha zote na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Jaribio la kutaka kumnasua Issa Mohammed Msukuya (46)  kwenye kesi inayomkabili ya kumiliki na kusambaza vipeperushi vinavyohamasisha waislamu kutoshiriki sensa ya taifa ya mwaka huu limegonga mwamba.
Jaribio hilo limegonga mwamba baada ya mkuu wa wilaya ya Singida Queen Mlozi kudai kwamba hataingilia suala ambalo tayari lipo mahakamani.
Awali Imam Masjid Salafiy Singida mjini Abdurahman Hassan, akiwa amefuatana na viongozi wenzake watatu, walifika ofisini kwa Mkuu wa Wilaya kumwomba aingilie kati suala la Issa, ili mahakama ya hakimu mkazi iweze kumwachia huru.
Imam Hassan alisema Issa  anapaswa kuachiwa huru kwa vile yeye si muasisi wa uandaaji wala  mchapishaji wa vipeperushi hivyo vinavyopinga zoezi la sensa.
Hata hivyo Mkuu wa Wilaya Mlozi aliwaomba viongozi hao wa dhehebu la kiislamau wawe  wavumilivu na kuiachia mahakama ifanye kazi yake bila kuingiliwa na upande wo  wote.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wapunguze munkhari, ili waweze kushiriki kujenga nchi katika misingi ya amani na utulivu.
Issa amefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi na kusomewa shitaka la kugawa vipeperushi vinavyowahamasisha waislamu kutokushiriki zoezi la sensa.
Mwendesha mashitaka ambaye ni mwanasheria wa serikali Geofrey Luhanga, alidai mbele ya hakimu Chiganga Tengwa kuwa mnamoAgosti saba mwaka huu huko katika viwanja vya shule ya sekondari ya kata ya Sepuka, mshitakiwa Issa alikamatwa akiwa na vipeperushi hivyo huku akijua wazi kuwa kitendo hicho ni kinyume na sheria.
Luhanga alisema kuwa mshitakiwa Issa ametenda kosa kwa mujibu wa kifungu 390 na 35 cha kanuni za adhabu sura 16 ujazo wa kwanza iliyofaniwa marejeo mwaka 2009.
Mshitakiwa amekana kosa hilo na yupo nje kwa dhamana ya watu wawili waliotoa ahadi ya shilingi milioni mbili kila moja.
Kesi hiyo sasa itatajwa tena Agosti 26 mwaka huu.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa