Na Emmanuel Michael, Singida
KAMATI za mikoa za baraza la ushauri la watumiaji wa huduma za nishati na maji nchini, zimetakiwa kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa matumizi bora ya raslimali hizo.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Parseko Kone wakati akizindua kamati hiyo.
Dk. Kone amesema licha ya kuwepo kwa changamoto ya uhaba wa nishati na maji na kupanda kwa bei zake, lakini baadhi ya watumiaji wa huduma hizo wamekuwa na matumizi mabaya.
Kutokana na hali hiyo amesema kuna haja kwa kamati za mikoa za ushauri wa baraza la watumiaji wa huduma za nishati na maji kutoa elimu kwa wananchi juu ya kutunza na kutumia vyema raslimali hizo.
Amesema hatua hiyo itasaidia katika kuhakikisha kuwa nishati kidogo na maji yanayopatikana yanatumika kwa uangalifu ili kukidhi mahitaji na kupunguza malalamiko ya kupanda bei.
Kamati hiyo yenye wajumbe sita imeundwa kwa mujibu wa sheria ya mamlaka ya udhibiti wa huduma za nishati na maji (EWURA) kifungu cha 30, ikiwa na jukumu la kusimamia maslahi ya watumiaji wa huduma hizo na kushauriana na wenye viwanda na wadau wengine.
Blogzamikoa
0 comments:
Post a Comment