na Jumbe Ismailly, Singida
BARAZA la ushauri la watumiaji wa huduma zinazodhibitiwa na EWURA (EWURA CCC), limekiri kukabiliwa na changamoto zinazokwamisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Mwenyekiti wa baraza hilo, Mhandisi Profesa Jamidu Katima aliyasema hayo jana kwenye hafla fupi ya utambulisho na uzinduzi wa Kamati ya Mkoa wa Singida ya EWURA CCC iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa.
Alisema kamati hizo zinaundwa katika kipindi kinachokabiliwa na kero lukuki, hali ambayo kwa namna moja au nyingine zimekuwa zikikwamisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi wake.
“Kamati hizi zimeundwa katika kipindi ambacho kuna kero, malalamiko na changamoto nyingi zinazowakabili watumiaji wa huduma za nishati na maji,” alifafanua Katima.
Kwa mujibu wa Katima, changamoto hizo ni ukosefu wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi, bei kubwa ya huduma za umeme, petroli na gesi.
Hivyo aliweka wazi kwamba kutokana na uduni huo wa huduma, wananchi wamelazimika kuelimishwa kwa ufasaha ni kwanini bei zinapanda kwa kiwango hicho, hususani katika kipindi wanachokabiliwa na ugumu wa maisha, ikiwemo mfumuko wa bei.
Akizindua kamati hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Parseko Kone alilipongeza baraza hilo na hakusita kulikumbusha umuhimu wa kuzingatia sheria za nchi pamoja na mipaka ya majukumu yao.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment