na Jumbe Ismailly, Singida
WAFUNGWA watano waliohukumiwa kuanza kutumikia adhabu ya kifungo cha jumla ya miaka 62 jela baada ya kupatikana na hatia ya kosa la unyang’anyi wa kutumia nguvu, wamegoma kuvaa sare za wafungwa baada ya kufikishwa gerezani.
Wamesema kuwa hawavaa sare mpaka hapo majibu yao ya rufaa yatakaporudi.
Taarifa za kuaminika zilizopatikana kutoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Singida na kuthibitishwa na Mkuu wa Gereza la Wilaya ya Singida, T. Mbuta zimeeleza kuwa wafungwa hao walitoa tamko hilo mara tu baada ya hukumu ya kesi yao kutolewa na Hakimu wa Mahakama hiyo, Flora Ndale wakati wakisindikizwa na askari kupelekwa gerezani kuanza kutumikia adhabu hiyo, Agosti 10, mwaka huu.
Wafungwa hao walioitisha mgomo wa kuvaa sare gerezani ni Abdallah Masoud, Hassan Jumanne, Rashidi Mwela, Jumanne Mjoi na Seif Ismaili Ngura.
Alipotakiwa kuzungumzia suala hilo, mkuu wa gereza la Wilaya ya Singida, Mbuta licha ya kukiri kuwepo, alisema kitendo hicho kilifanyika kutokana na wafungwa hao kutofahamu haki zao wanazotakiwa kudai.
Alisema baada ya wafungwa hao kufikishwa gerezani hapo, waliwaelimisha nini cha kufanya ili waweze kutimiza matakwa yao ya kisheria na wakakubali kuvaa sare.
“Kwa kweli tukio hilo lilikuwepo kwanza tu walipofikishwa wafungwa hao gerezani… madai yao ni kweli yana msingi kabisa, lakini tuliwaambia ili waweze kufanikiwa kwanza ni lazima wakubali kuvaa sare ili waweze kutambuliwa kuwa ni wafungwa,” alisema Mbuta.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment