Home » » SERIKALI KUTOA FIDIA YA NG’OMBE WALIOUAWA

SERIKALI KUTOA FIDIA YA NG’OMBE WALIOUAWA

Na Nathaniel Limu, Singida

SERIKALI imeahidi kutoa Sh milioni sita ikiwa ni fidia ya ng’ombe 22, wanaodaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na askari wa Pori la Akiba la Maswa lililopo Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu.

Inadaiwa ng’ombe hao walipigwa risasi na kuuawa Desemba, 2009 baada ya kuingizwa ndani ya hifadhi hiyo kinyume cha sheria zinazolinda hifadhi za wanyama pori.

Ahadi hiyo imetolewa mjini hapa juzi na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na wakazi wa Kata ya Sakasaka jimboni Kisesa.

Alisema lengo la uamuzi huo ni kuimarisha uhusiano mzuri zaidi kati ya askari wa wanyama pori na wakazi wa vijiji vinavyozunguka pori hilo.

“Pia ni sehemu ya mikakati inayochukuliwa na Serikali ya kuhakikisha mgogoro wa muda mrefu kati ya uongozi wa Pori la Akiba Maswa, wananchi wa vijiji vinavyozunguka pori hilo unamalizika na kurejesha amani na utulivu katika eneo hilo,” alisema Nyalandu.

Aidha, alisema Serikali inatarajia kuunda kamati huru itakayotafuta ufumbuzi wa mgogoro huo wa muda mrefu.

“Katika kamati hii, kutakuwepo na mwakilishi mmoja kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na wajumbe wengine watakuwa ni watu huru watakaozitendea haki pande zote mbili.

Alisema kamati hiyo itatoa taarifa yake wizarani mapema kabla ya vikao vya Bunge vinavyoendelea mjini Dodoma kumalizika.

“Napenda kukumbusha kuwa ni marufuku kuchungia, kulima, kuingiza au kufanya shughuli zozote za kijamii ndani ya hifadhi ya wanyama pori, mfugaji au mtu yeyote atakayevunja sheria halali zilizopo atachukuliwa hatua kali za kisheria,” alisema Nyalandu.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Rosemary Kirigini, alisema Hifadhi ya Pori la akiba Maswa ipo kwa mujibu wa sheria.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa