Home » » WATAKAO URAIS CCM MTEGONI

WATAKAO URAIS CCM MTEGONI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 

KAMATI ya Usalama na Maadili ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Agosti mwaka huu, itafanya mapitio ya mwenendo wa wanachama wake waliopewa onyo kwa kosa la kuanza kampeni za kutafuta kuteuliwa kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu 2015, kabla ya wakati kinyume na Kanuni za Uongozi na Maadili ya CCM, toleo la Februari 2010, Ibara 6(7)(i).

 

Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Bw. Nape Nnauye, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya kile kilichozungumzwa kwenye kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM iliyofanya kikao cha siku moja jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete.

 

Alisema pamoja na mambo mengine, kikao hicho kilipokea taarifa ya mazungumzo yanayoendelea kati ya CCM kwa upande mmoja na vyama vingine vya siasa ambavyo ni CHADEMA, NCCR-Mageuzi na CUF ambayo yanasimamiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis Mutungi.

Bw. Nnauye alisema, lengo la mazungumzo yaliyokutanisha vyama hivyo ni kuangalia kwa kina sababu za baadhi ya wajumbe wachache wa Bunge Maalumu la Katiba, kususia na kutoka nje katika awamu ya kwanza ya vikao vya Bunge hilo.

Lengo lingine ni kuangalia namna ambavyo wajumbe hao watarudi bungeni ili kukamilisha mchakato wa mabadiliko ya Katiba ambapo Kamati Kuu ya CCM, imeridhishwa na mwenendo wa mazungumzo hayo, kupongeza juhudi zinazofanywa na Jaji Mutungi pamoja na vyama husika vinavyoshiriki mazungumzo.

 

"Kamati Kuu pia ilipokea taarifa za harakati za baadhi ya wanachama wa CCM walioonesha nia ya kuomba ridhaa ya chama kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu 2015...baada ya kutafakari kwa kina, Kamati hii inapenda kuwakumbusha wote kuwa ili wasipoteze sifa za kugombea ni muhimu wakazingatia katiba, kanuni na taratibu za chama.

"Wanachama waliopewa adhabu na Kamati Kuu kutokana na kukiuka taratibu za chama katika suala hili, Kamati ya Usalama na Maadili ya chama itafanya mapitio ya mwenendo wao na utekelezaji wa adhabu hiyo Agosti mwaka huu.

"Ikibainika hawatekelezi ipasavyo masharti ya adhabu zao, itapendekeza kwa Kamati Kuu iongeze adhabu kwa kuzingatia taratibu za chama," alisema Bw. Nnauye.

Aliongeza kuwa ni muhimu wanachama wote wakatambua kuwa, chama ni pamoja na Katiba, kanuni na taratibu zake hivyo kutoziheshimu na kuzifuata ni kuvuruga jambo ambalo haliwezi kuvumilika.

Alisema dhamira ya CCM kusimamia Katiba, kanuni na taratibu za chama ni kuhakikisha chama hicho kinakuwa na umoja, mshikamano ambao ni wa muhimu sana hasa wanapokwenda kukamilisha kazi ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2010/15.

Februari mwaka huu, CCM ilifanya vikao vya kitaifa ambavyo vilishughulikia suala la maadili ndani ya chama vikihusisha Kamati Ndogo ya Udhibiti, Tume ya Udhibiti na Nidhamu na Kamati Kuu.

Vikao hivyo viliwahoji baadhi ya wanachama wa chama hicho ambao ni Bw. Frederick Sumaye, Bw. Edward Lowasa, Bw. Bernard Membe, Bw. Stephen Wassira, Bw. January Makamba na Bw. William Ngeleja.

Baada ya wanachama waliohojiwa, ilithibitika kuwa baadhi ya tuhuma dhidi yao ni za kweli hivyo kamati zilipendekeza adhabu na mapendekezo hayo yalipelekwa kwenye Tume ya Udhibiti na Nidhamu na hatimaye Kamati Kuu ya CCM ambayo ilitoa adhabu kwa wahusika.

Ilithibitika wanachama hao walifanya makosa mawili, mosi la kuanza kampeni za kutafuta kuteuliwa kugombea Urais kabla ya wakati kinyume na Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM, Toleo la Februari 2010, Ibara 6(7)(i).

Kosa la pili ni kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya chama na baadhi yao kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya jamii kinyume na Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM, Toleo la Februari 2010, Ibara kadhaa za kanuni hizo.

Kwa mujibu wa Bw. Nnauye ambaye alitoa tamko la CCM Februari 18 mwaka huu juu ya adhabu zilizochukuliwa kwa wanachama hao, alisema Kamati Kuu baada ya kuthibitisha makosa hayo imewapa watu hao adhabu ya onyo kali na kuwataka wajiepushe na vitendo vinavyokiuka maadili na iwapo wataendelea na vitendo hivyo, chama kitawachukulia hatua kali zaidi.

Alisema tafsiri ya adhabu ya onyo kali kwa mujibu wa Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM, Toleo la Februari 2010, Ibara ya 8(ii) (b) ni mwanachama aliyepewa adhabu ya onyo kali, atakuwa katika hali ya kuchunguzwa kwa muda usiopungua miezi 12, ili kumsaidia katika jitihada zake za kujirekebisha.

Aliongeza kuwa, Kamati Kuu iliitaka Kamati Ndogo ya Udhibiti kuwachunguza na kuchukua hatua kwa wote waliohusika kwa namna moja au nyingine (mawakala na wapambe) kufanyika kwa vitendo hivyo ambavyo vilivunja kanuni za chama.

Pia Kamati Kuu iliwaonya vikali viongozi na watendaji wa chama ikiwataka wajiepushe kujihusisha na matendo ya wanaowania urais yanayovunja na kukiuka maadili ya chama badala yake wazingatie kanuni na taratibu za chama.

Chanzo:Majira

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa