Home » » KIGODA ATAKA TAFITI ZITUMIKE KUTUNGA SERA

KIGODA ATAKA TAFITI ZITUMIKE KUTUNGA SERA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda
Watafiti nchini wametakiwa kuwasilisha matokeo ya tafiti zao serikalini, ili zitumike katika kutengeneza sera zinazohusiana na maendeleo ya watu.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda, amesema hayo katika ufunguzi wa mkutano wa kimataifa wa uendelezaji wa ujasiriamali  na biashara ndogo na za kati, uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Hotuba ya Dk. Kigoda ilisomwa kwa niaba yake na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Joyce Mapunjo.

Dk. Kigoda, alisema kuna tafiti nyingi zimefanywa na wanataaluma tofauti, lakini hazijaisaidia jamii kwa vile zimehifadhiwa kwenye makabati ndani ya taasisi wanazozifanyia kazi badala ya kuziweka wazi kwa jamii ikiwamo kuziwasilisha serikalini.

Aliwataka watafiti, wajasiriamali, wanataaluma  na wakurugenzi wa mashirika zaidi ya 150 wanaoshiriki mkutano huo wa siku mbili, kufanya majadaliano na tafiti ambazo zitaleta mawazo yaliyo na umuhimu kwa Watanzania.

“Haya mambo ya tafiti yana mambo mengi, sasa na ninyi myaangalie hayo, mkae chini na kutafakari na kuleta mawazo ambayo yatawasaidia Watanzania, kwani mnaweza kufanya tafiti zisiwe na faida kwa mazingira ya Tanzania, lakini yakawa ni mazuri kwa mazingira ya nchi nyingine,” alisema.

Dk. Kigoda, alisema mchango wa biashara ndogo ndogo ni mkubwa na muhimu katika kujenga uchumi wa Taifa na kupunguza umaskini, hivyo serikali itaendelea kuwasaidia wajasiriamali wadogo ili wajikomboe kiuchumi.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Utawala), Profesa Yunus Mgaya, alisema kila mwaka shule ya biashara ya chuo hicho (UDBS), inaandaa mkutano kama huo, ili kuwakutanisha watafiti kutoka vyuo vikuu mbalimbali pamoja na wajasiriamali.

Alisema lengo la mikutano hiyo ni pamoja na kubadilishana uzoefu na kusaidiana kwenye masuala ya kitaalamu.

Profesa Mgaya, alisema serikali ni lazima iwe na sera za kuwasaidia wajasiriamali, na ndiyo maana wamekuwa wakiishirikisha kwenye mikutano yao kwa kuwa mchango wa wafanyabiashara wadogowadogo ni mkubwa na unatoa ajira kwa watu wengi.
 
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa