Home » » TAASISI YA MKAPA YAKABIDHI NYUMBA 30

TAASISI YA MKAPA YAKABIDHI NYUMBA 30

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa akikabidhiwa kibuyu na akina mama wa kijiji cha Senenemfuru, Singida vijijini, kikiwa na maana ya upendo, baada ya kukabidhi nyumba, kati ya 30 zilizojengwa na taasisi ya Mkapa Foundation kwa halmashauri tano za mkoa wa Singida.
 
Rais  mstaafu awamu ya tatu, Benjamin  Mkapa, kupitia taasisi yake ‘Benjamin William Mkapa HIV/AIDS’ (BMAF), amekabidhi nyumba 30 zilizojengwa kwenye zahanati 13 na vituo vya afya viwili kwa gharama ya zaidi ya Sh. bilioni 1. 9 katika Halmashauri tano za wilaya mkoani Singida.
Akikabidhi sehemu ya nyumba hizo kwenye hafla iliyofanyika kijiji cha Senenemfuru Singida vijijini, Mkapa alishukuru wafadhili waliowezesha kazi hiyo, ukiwamo Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Ukimwi, Kifua kikuu na Malaria (Global fund) kwa kuonyesha imani kwa serikali ya Tanzania.

“Binafsi ninafarijika kufahamu kwamba wananchi wanaohudumiwa na zahanati 15 ambazo nyumba hizi zimejengwa, wataendelea kufaidika na huduma bora za afya kutoka vituo hivyo kwa sababu watoa huduma wameboreshewa mazingira ya kazi zao,” alisema Mkapa.

Nyumba hizo zimejengwa katika zahanati ya Misughaa na Mangonyi (Ikungi), Mkenge, Mpambaa na Senenemfuru (Singida), Ulemo Uwanza na kituo cha afya Ndago (Iramba), Kinyambuli na Dominiki (Mkalama). Pia kituo cha afya Itigi, Idodyandole, Heka, Mpola na Chibumagwa (Manyoni).

Mkapa alizihimiza halmashauri za wilaya husika kutunza vyema nyumba hizo na kutumika kwa matumizi yaliyokusudiwa na alizitaka kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya matengenezo ya mara kwa mara ili zidumu, kuendelea kuwa madhubuti na kuvutia zaidi.

“Hata hivyo, ili kuwa na huduma ya afya bora zaidi na kamilifu, ni lazima kuwapo na zahanati yenye dawa, vifaa vya kutolea huduma na vipimo na uwapo wa wataalamu wa kutosha, wekeni mkakati kuhakikisha hayo yote yanazingatiwa na kutekelezwa,” alisisitiza Mkapa.

Mwakilishi Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Catherine Joachim, aliishukuru taasisi hiyo na kusema kupitia mradi huo kwa mwaka wa pili sasa utahusisha ujenzi wa nyumba 220 za watumishi wa afya kwa mikoa ya Arusha, Ruvuma, Manyara, Pwani na Singida.

Aidha, afisa mtendaji Mkuu wa BMAF, Dk. Ellen Mkondya-Senkoro, alisema BMAF mkoani Singida imekuwa ikichangia shughuli mbalimbali ikiwamo kuimarisha huduma za Ukimwi, afya ya uzazi na masuala ya watumishi wa afya tangu mwaka 2006.
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa