Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Rais mstaafu, Benjamin Mkapa akipokewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk
Parseko Kone kwenye viwanja vya zahanati ya Kijiji cha Senenemfuru,
wilaya ya Singida kuzindua nyumba za watumishi
zilizojengwa na Taasisi
ya Benjamin Mkapa.
Rais mstaafu, Benjamin Mkapa amewataka Watanzania kuwa
waangalifu ili mchakato wa Katiba Mpya usiwe sababu ya kupigana au
kufarakana ili kupata Katiba itakayoendelea kudumisha amani, upendo,
utulivu na ushirikiano.
Mkapa alitoa wito huo juzi, alipokuwa akizungumza
kwenye hafla ya kukabidhi nyumba 30 za watumishi wa vituo vya huduma ya
afya mkoani hapa zilizojengwa na Taasisi ya Mkapa HIV/AIDS Foundation
kwa zaidi ya Sh1.9 bilioni.
“Vyovyote mchakato wa Katiba utakavyoishia,
tuhakikishe tunabaki na amani na utulivu wetu kwa ajili ya ustawi wa
nchi yetu, tuhitilafiane bila kupigana,” alisema.
Alisema Watanzania wanapaswa kwa pamoja
wasiiharibu nchi yao na kuhakikisha kizazi cha sasa na kijacho,
vinaendelea kuwaenzi waasisi wa Taifa kwa uadilifu mkubwa.
Akabidhi nyumba
Akikabidhi nyumba hizo, Mkapa alisema ana imani
wananchi wanaohudumiwa na zahanati 15 zilizojengewa nyumba hizo
wataendelea kufaidika na huduma bora kwa kuwa watumishi wameboreshewa
mazingira ya kazi.
“Kama mnavyoona nyumba hizi ni za kisasa, zina
maeneo muhimu yote yanayokidhi mahitaji ya binadamu, zipo imara na
zimekidhi viwango vya ujenzi vinavyostahili,” alisema.
Aliitaka halmashauri zinazohusika kuhakikisha
nyumba hizo zinatumika kama ilivyokusudiwa, kutunzwa vizuri na kutengewa
bajeti ya kutosha kwa ajili ya ukarabati pale utakapohitajika ili
ziweze kudumu kwa muda mrefu.
Vijiji vilivyonufaika vipo katika wilaya za Singida Vijijini, Iramba na Manyoni.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment