Gasper Andrew, Shelui
OFISI ya madini Kanda ya Kati imewataka wachimbaji wadogo wa dhahabu katika mgodi wa Sekenke Halmashauri ya Wilaya ya Iramba mkoani Singida, kuacha tabia ya kuvamia maeneo yenye leseni na kuanza kuendesha shughuli zao kinyume cha sheria.
Tamko hilo la ofisi ya madini, limekuja kufuatia mgogoro uliotokana na wachimbaji wadogo kugoma kuondoka wala kuingia ubia na mwenye leseni katika eneo hilo kwa madai kuwa wapo kwa muda mrefu na leseni husika kutaja Kijiji cha Mgongo badala ya Sekenke.
Akizungumza mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Iramba juzi, Kamishna msaidizi wa madini Kanda ya Kati, Manase Mbasha alisema kitendo cha wachimbaji hao kuvamia eneo lenye leseni na kugoma kuondoka kinakiuka sheria ya madini namba sita ya mwaka 2010 na walipaswa kushtakiwa.
Kutokana na hali hiyo, Mbasha aliwataka wachimbaji hao kukaa na mwenye leseni kufikia mwafaka badala ya kuendelea kufanya shughuli zao kinyume cha sheria na kuikosesha Serikali mapato.
Hata hivyo alimtaka mmiliki wa leseni ya eneo hilo, John Bina na wenzake kuhakikisha kuwa wanalipa fidia kwa wote wanaostahili kwa mujibu wa sheria.Inakadriwa kuwa zaidi ya wachimbaji wadogo 1,000 wamejiajiri kwenye sekta ya madini katika eneo la Sekenke mkoani Singida.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment