Mbunge  wa jimbo la Singida mjini Mh. Mohammed Gullam Dewji akizungumza na  wafanyabiashara wa bodaboda (hawapo kwenye picha) muda mfupi kabla  hajawakabidhi msaada wa pikipiki kumi zenye thamani ya shilingi milioni  20.Kushoto ni katibu wa umoja wa wafanyabiashara wa bodaboda, Maulid  Mpondo.Kulia wa kwanza ni Kaimu mkurugenzi wa manispaa ya  Singida,Williamu Haaly na anayefuata,ni katibu wa CCM manispaa ya  Singida.
 Mo  akizungumza na waumini wa kanisa la Pentekosti la kijiji cha Ititi muda  mfupi kabla hajakabidhi msaada wa mifuko 25 ya saruji na shilingi laki  tano taslimu.
 Mmoja wa wafanyabiashara wa bodaboda akisoma risala yao kwa mbunge wa jimbo la Singida mjini Mh. Mohammed Gullam Dewji.
Mbunge  wa jimbo la Singida mjini Mh. Mohammed Gullam Dewji akimkabidhi katibu  wa umoja wa wafanyabishara wa bodaboda msaada wa pikipiki 10. 
 Mbunge  wa jimbo la Singida mjini,Mohammed Gullam Dewji akimkabidhi Mchungaji  Daud Elia mifuko 25 ya saruji kwa ajili ya kujengea kanisa.
  Baadhi ya Wafanyabiashara Wa Bodaboda wakimsikiliza mbunge wao.
 Pikipiki  10 aina ya sanlag CC150 zilizotolewa msaada ya mbunge wa jimbo la  Singida mjini, Mohammed Gullam Dewji kwa vikundi 10 vya wafanyabiashara  wa bodaboda mjini Singida.
Baadhi  ya wafanyabiashara wa bodaboda wa mjini Singida wakiserebuka na kucheza  'KIDUKU' na mbunge wao Mohammed Gullam Dewji muda mfupi kabla ya mbunge  huyo kuwakabidhi wafanyabiashara hao msaada wa pikipiki.
 Jengo la kanisa la Pentekoste la kijiji cha Ititi jimbo la Singida mjini.
---
Na Geofrey Mwakibete na Nathaniel Limu
Wafanyabiashara  wa bodaboda jimbo la Singida mjini,wamehimizwa  kuunda/kuanzisha  vikundi ili pamoja na mambo mengine, kujijengea  mazingira mazuri ya kukopesheka.
Wito huo umetolewa na mbunge wa jimbo la Singida  mjini,Mohammed Gullam Dewji,wakati akizungumza kwenye hafla iliyofana,  ya kukabidhi pikipiki 10 aina ya sanlag CC 150 zenye thamani ya shilingi  milioni 20 kwa vikundi vya wafanyabiashara wa bodaboda.
Alisema faida za  kujiunga kwenye vikundi ni nyingi ikiwemo ya kuwa nafasi nzuri ya kupata  mikopo mbalimbali kutoka kwenye taasisi za kifedha.Mtu mmoja mmoja  akitaka kukopa fedha benki ni ngumu, kuotokana masharti yaliyowekwa na  taasisi za kifedha. 
“Siku zote umoja ni  nguvu,utegano unachangia kuleta ulegevu unaozaa udhaifu.Mahali pana  ulegevu,kwanza hakuna maendeleo ya kweli na pia kutetea haki,inakuwa  ngumu mno”,alifafanua Dewji ambaye pia ni mjumbe wa NEC CCM mkoa wa  Singida.
Kuhusu pikipiki hizo  alizotoa msaada, alisema lengo lake ni kwamba kila kikundi kitaitumia  pikipiki yake kwa ajili ya kukiongezea kikundi mapato ambayo endapo  yatatunzwa vizuri,ipo siku kila mwanakikundi anaweza akamiliki pikipiki  yake binafsi. 
Aidha, amewataka  wakati wote kuzingatia sheria halali zilizowekwa na mamlaka husika, ili  shughuli zao ziweze kuendelea bila matatizo.
“Pia napenda kutumia fursa hii, kuomba mamlaka zinazohusika na sheria za  usalama barabarani na utozaji wa kodi na ushuru, kujipanga kwa ajili ya  kutoa elimu kwa wafanyabiashara wa bodaboda,ili waweze kuzifahamu  sheria husika”,alisema na kuongeza;
“Nina imani kwamba  wafanyabiashara wa boda boda wakifahamu kwa kina sheria za usalama  barabarani,kutapunguza mno ajali na pia wakifahamu mambo ya kodi na  ushuru,hawatakwepa kulipa”.
Katika hatua nyingine,  Dewji amewahimiza waumini wa madhehebu ya dini, kuongeza kasi ya utoaji  sadaka,ili kuimarisha ustawi wa madhahebu yao.
Alisema waumini wanao wajibu mkubwa wa kuchangia  kwa hali na mali madhehebu yao kwa lengo  yaweze kutekeleza wajibu wake  kwa ufanisi zaidi.
“Sadaka  inayotolewa kwa moyo mkujufu,licha ya kusaidia ustawi wa dhehebu la  dini husika,mtoaji anakuwa amejiwekea thawabu mbele ya mwenyezi  Mungu”,alisema Dewji.
Akiijengea nguvu hoja yake hiyo,mbunge huyo,  alisema ustawi wa kweli wa dhehebu la dini,utaletwa na waumini  wenyewe,watu wengine/taasisi zingine,kazi zao ni kusaidia mahali waumini  wanapokuwa wamepelea.  
Katika siku yake ya  pili ya ziara yake ya kikazi jimboni kwake,Dewji alitoa msaada wa mifuko  ya saruji 40 kwa msikiti wa kijiji cha Manguamitogho na mifuko mingine  25 ya saruji na shilingi laki tano taslimu, kwa kanisa la Pentekoste la  kijiji cha Ititi.
Katika siku yake ya  mwisho ya ziara yake (17/6/2012),Dewji alitarajiwa kuwa na kikao maalum  na madiwani wa kata za Singida mjini,kuzindua kisima cha maji cha kijiji  cha Mtisi,kuzungumza na wanachama wa klabu ya waandishi wa habari mkoa  wa Singida na kukagua kituo cha afya cha Sokoine mjini Singida
0 comments:
Post a Comment