Na Jumbe Ismailly, Singida
MKAZI wa mjini Singida, Muna Abubakari (37) ambaye ni fundi ujenzi, amefariki dunia juzi baada ya kupigwa risasi na askari wa Jeshi la Magereza mkoani hapa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Linus Sinzumwa, alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi, majira ya saa saba mchana.
Alisema askari aliyehusika na tukio hilo ametambuliwa kwa jina la CPL Abdalla Kabwe (31) na kwamba baada ya kutekeleza azma yake hiyo alitoroka na haijulikana alikokwenda.
Alisema kabla ya tukio hilo, Abubakar alikuwa na askari wa gereza huyo wakijenga katika jengo la ofisi mpya ya jeshi hilo iliyopo maeneo ya Mtaa wa Bomani.
Alieleza kuwa wakati wakiendelea na ujenzi huo ndipo askari wa kawaida wa magereza aliyetambulika kwa jina la Fred John (24) alimkabidhi bosi wake, CPL Kabwe bunduki aina ya SAR yenye namba 1123457 ikiwa na risasi 10 naye aliondoka kwenda kufuata vifaa vingine vya ujenzi.
Kwa mujibu wa msemaji huyo wa jeshi, inadaiwa Abubakari na askari huyo alikuwa marafiki na kwamba ghafla walisikia mlio wa risasi.
“Watu wengine waliokuwa ndani ya jengo hilo na majirani waliposikia mlio huo walianza kukimbilia kwenye eneo la tukio na kumkuta Abubakari akiwa amelala chini huku akibubujikwa na damu nyingi huku bunduki iliyotumika ikiwa imeachwa pembeni ya mwili wake na askari Kabwe akiwa ametoweka,” alisema.
Kamanda huyo alisema jeshi hilo limeanzisha msako wa kumtafuta askari Kabwe na wakati huohuo wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha mauaji hayo.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Singida, Dk. Suleiman Muttani, alisema kuwa fundi ujenzi huyo amefariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment