Home » » MBUNGE WA IRAMBA MAGHARIBI MH. MWIGULLU LAMECK KUWASILISHA HOJA BINAFSI.

MBUNGE WA IRAMBA MAGHARIBI MH. MWIGULLU LAMECK KUWASILISHA HOJA BINAFSI.




Mbunge wa jimbo la Iramba magharibi na katibu wa uchumi na fedha CCM taifa Mwigullu Lameck Nchemba,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) juu ya kusudio  lake la kuwasilisha hoja binafsi ya kuundwa kwa baraza maalum la kushughulikia makosa ya uhujumu uchumi na rushwa.Picha na Nathaniel Limu.
MBUNGE wa jimbo la Iramba magharibi (CCM) mkoani Singida, Mwigulu Nchemba, anakusudia kuwasilisha hoja binafsi wakati wa bunge la bajeti lijalo, juu ya kuanzishwa kwa baraza maalum litakaloshughulikia makosa ya uhujumu uchumi na vitendo vya rushwa.
Amesema amefikia uamuzi huo ambao amedai utasadia kwa kiasi kikubwa wananchi kuendelea kuiamini serikali yao , baada ya kubaini kuwa kesi zinazohusu vitendo hivyo, huchukua muda mrefu, mno kumalizika na kitendo hicho,huchangia watuhumiwa wengi kuachiliwa huru.
Akifafanua zaidi, amedai kwamba kuchelewa kumalizika kwa kesi hizo, hutoa mwanya kwa watuhumiwa kutoa rushwa ili sheria iweze kupinduliwa kwa manufaa yao .
Mwigulu ambaye pia ni Katibu wa fedha na uchumi wa CCM taifa, alisema kuachiwa kwa watuhumiwa wa makosa ya rushwa na uhujumu uchumi, kunachangia mno kuporomoka kwa maadili ya viongozi na wakati huo huo, wananchi kuichukia serikali yao.
Alisema mazingira ya usikilizaji wa kesi hizo yalivyo hivi sasa katika mahakama hizi za kawaida, yanachangia kupunguza ufanisi wakati wa kuzishughulikia, kutokana na msongamano wa kesi katika mahakama hizo za kawaida.
“Nadhani umefika wakati makosa haya mazito, yatengewe chombo chake maalum ili yashughulikiwe kwa umakini wa hali ya juu zaidi, na maamuzi yaweze kupatikana mapema iwezekanavyo”,alisema.
Akiijengea nguvu hoja yake hiyo, alisema baada ya serikali kuondoa kesi zinazohusu migogoro ya ardhi na kuanzisha baraza maalum linaloshughulikia makosa/malalamiko ya ardhi tu, kwa sasa migogoro ya ardhi imepungua kwa kiwango kikubwa.
“Maandalizi yote muhimu kwa ajili ya kuwasilisha hoja hii nzito kwenye kikao kijacho cha bunge la bajeti, yanakwenda vizuri kama itaafikiwa hoja hii, basi pamoja na mambo mengine, yafanyike marekebisho ya sheria ya upelelezi iliyopo hivi sasa na kuupa umuhimu ushahidi wa mazingira kwa kuwa kutolea ushahidi makosa ya rushwa, ni mgumu”,alifafanua Nchemba.
Mwigulu alisema pia upo umuhimu mkubwa wa kuongeza adhabu ya makosa hayo ambayo itakuwa fundisho la kweli kwa wakosaji na kuwaogofya viongozi/wananchi wanaotarajia kutoa rushwa ua kuhujumu uchumi.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa