na Jumbe Ismailly, Singida
MWANAMKE mmoja, Mwanaharusi Juma (34) mkazi wa Kijiji cha Ndulungu Wilaya ya Iramba mkoani hapa, amekimbiwa na mumewe kutokana na kujifungua watoto wawili wanaofanana na nyani.
Mama huyo mwenye familia ya watoto wanne wenye baba wawili tofauti, aliolewa na mume wa kwanza na kuzaa naye mtoto mmoja, Fadhila Juma (15) mwaka 2007 - mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Ndulungu, kabla ya kuolewa na Sadick Selemani ambaye amemkimbia baada ya kumzalia watoto hao wawili wenye kasoro kimaumbile.
“Niliolewa na Sadick mwaka 2008 na nimeishi naye kwa miaka kumi nikampatia watoto watatu, wakiwemo wawili wanaofanana na nyani, na mmoja alikuwa kawaida kama binadamu wengine,” alisema.
Alisema kuwa watoto hao licha ya kuwa binadamu, lakini wamekuwa na sura za wanyama.
Mama huyo aliwataja watoto watatu aliozaa na Sadick kuwa ni Alhaji Sadick (10), Ramadhani Sadick (6) wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Ndulungu na Abdulatifu Sadick (5).
Alibainisha kuwa, watoto hao wenye matatizo wamekuwa wakishindwa kutembea mwendo mrefu bila kupumzika na kupumua kwa shida sana na matumbo yao ni makubwa.
“Matumbo ya watoto wangu wawili wenye matatizo ni makubwa, macho yao ni mekundu kama mnavyoyaona, na hupumua kwa shida sana kiasi cha kuwafanya washindwe kutembea umbali mrefu bila kupumzika,” alisisitiza Mwanaharusi.
Alisema kuwa, watoto hao walizaliwa wakiwa katika hali ya kawaida kabisa, lakini walianza kuugua mara kwa mara na kutoongea tena hadi hivi sasa.
“Mimi ni mke mdogo katika ndoa ya wake wawili, na mume wangu alipoona nimeanza kumbana sana kuhusu matibabu ya watoto hao, aliondoka mwaka 2010 na kuhamia kwa mke mkubwa,” alisema.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment