Home » » RC apiga marufuku walanguzi wa alizeti

RC apiga marufuku walanguzi wa alizeti


na Hillary Shoo, Singida
MKUU wa Mkoa wa Singida, Dk. Parseko Kone amepiga marufuku wanunuzi binafsi wa alizeti kununua moja kwa moja zao hilo kutoka kwa wakulima kuanzia sasa.
Badala yake amewataka wakulima kuuza mazao yao kwenye vyama vya ushirika vya msingi kwa kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani ili kunufaika na zao hilo.
Aliyasema hayo jana ofisini kwake alipokuwa akizungumza na viongozi wa vyama vya ushirika vya msingi 81 vya mkoani hapa.
“Kuanzia leo na kuendelea vyama vya ushirika vya msingi ndiyo pekee vitaruhusiwa kununua zao la alizeti kutoka kwa wakulima na wanunuzi binafsi watanunua kwenye maghala kwa maelekezo ya chama kikuu cha ushirika (SIFACU) na kwa bei watakayokubaliana.” Alisisitiza Kone.
Kone alisema wanunuzi binafsi wamekuwa wakinunua zao hilo kwa wakulima kwa bei ndogo kwa sababu ya kutumia wanunuzi wa kati licha ya halmashauri kukosa ushuru wa zao hilo na kuzinyima mapato ya kuweza kujiendesha.
“Udhibiti na ubora wa zao la alizeti umekuwa mdogo hivyo kutokuwa na soko lililo bora, mkoa unakosa takwimu  sahihi za uzalishaji wa zao hili na zaidi ya hili wanunuzi wamekuwa wakitorosha zao hili kwa njia za panya hivyo mkoa kukosa pato litokanalo na alizeti,” alisema.
Alieleza kwamba mfumo wa stakabadhi ghalani unaotumiwa na vyama vya msingi vya ushirika ndiyo pekee unaoweza kumsaidia mkulima mdogo kupata pato linalolingana na jasho lake.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa