Home » » Dewji kutoa mamilioni kusaidia kilimo

Dewji kutoa mamilioni kusaidia kilimo


Mwandishi Wetu, Singida
MBUNGE wa Jimbo la Singida mjini (CCM),  Mohamed  Dewji, ameahidi kuwapa wananchi wa jimbo lake Sh250 milioni, lengo likiwa ni kugharamia mradi wa kilimo katika eneo hilo.

Akizungumza jimboni kwake katika hafla ya uzinduzi wa kisima cha maji cha kitongoji cha Mtisi, Kijiji cha Mtamaa alisema,  fedha hizo zitatumika kununua tani 60 za mbegu za choroko, dengu na mbaazi katika msimu ujao wa kilimo.

Dewji alisema  lengo la mradi huo  ni kuwajengea mazingira mazuri wakulima wa jimbo lake ili waweze   kuboresha hali zao  kiuchumi.

Alisema pia kuwa, kila kikundu cha wakulima 25, kitapewa jembe la kukokotwa na wanyama (plau).
“Mimi, madiwani pamoja na watendaji, tutawahamasisha wakulima kila kaya ilime ekari moja ya mazao hayo ya mbaazi, dengu na choroko.  Mazao hayo yana soko la uhakika na bei zake zipo juu zaidi ya zao la mahindi”, alisema na kuongeza:

“Binafsi nitanunua mazao hayo kwa bei ambayo itakuwa na faida kubwa kwa mkulima wa mazao hayo”.
Katika hatua nyingine,  Dewji alisema Mtaalamu wa Kilimo katika ofisi yake kwa ushirikiano na wataalamu wa manispaa, watasimamia mradi huo kwa karibu, ili wakulima waweze kuzingatia ushauri wa kilimo bora.

“Lengo ni kwamba mavuno katika ekari hiyo moja ya aidha, dengu, choroko au mbaazi, yakidhi mahitaji ya kuweza kumkomboa mkulima kiuchumi,”  alisema kwa kujiamni.

Wakati huo huo, mbunge huyo  alitumia nafasi hiyo kuwataka wakulima kubadilika na kuachana na kilimo cha mazoea na kuanza kulima kilimo kinachozingatia ushauri wa taalamu.

Aidha, alisema kutokana na misimu ya mvua za miaka hii kutokueleweka vizuri, njia pekee ya kunufaika na kilimo, ni mkulima kuwahi kuandaa mashamba na mbegu bora kabla msimu haujaanza.
Chanzo: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa