Mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko Vicent Kone,akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC), Kulia ni katibu tawala mkoa wa Singida,Liana Hassan. Baadhi ya wajumbe wa kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa wa Singida walioshiriki Kikao kwenye ukumbi wa mikutano wa kanisa katoliki mjini singida.Picha zote na Nathaniel Limu.
IMEELEZWA kwamba halmashauri ya wilaya ya Singida,imeshindwa kufikia malengo yake ya ukusanyaji wa mapato ya ndani,kwa kile kilichodaiwa kuwa wananchi wa jimbo la Singida mashariki,kuzuiwa kuchangia maendeleo yao.
Hayo yamesemwa juzi na mkurugenzi wa halmashauri hiyo,Illuminata Mwenda,wakati akitoa taarifa yake ya kushindwa kukusanya mapato ndani kama inavyokusudiwa, kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa kanisa katoliki mjini Singida.
Alisema wananchi wa jimbo hilo,wamezuiwa kuchangia na kutekeleza miradi yao ya maendeleo na pia wasilipe ushuru wala kodi kama inavyoelekezwa na sheria ndogo za halmashauri hiyo.
Mwenda alisema siasa za aina hiyo,zimechangia ukusanyaji wa mapato ya ndani kuwa mgumu mno na vile vile zimedumaza maendeleo kwa ujumla katika jimbo hilo.
Hata hivyo, mkurugenzi huyo alisema wanaangalia utaratibu wa kisheria utakaosaidia kuwahimiza wananchi wa jimbo hilo kushiriki kuchangia na kutekeleza miradi yao ya maendeleo, kama ambavyo wananchi wengine wa majimbo mengine ya halmashauri,wanavyochangia.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Mkalama,Mussa Chang’a alisema serikali ya mkoa isiruhusu siasa uchwara kuendelea kwa vile zitapunguza kasi ya kuwaletea wananchi maendekeo endelevu.
“Ni afadhali kulaumiwa kuliko kuacha wanasiasa uchwara wanaharibu au wanadumaza maendeleo ya wananchi, yaliyofikiwa na yanayotarajiwa kufikiwa”,alisema.
Taarifa iliyotolewa kwenye kikao hicho, ni kwamba halmashauri ya wilaya ya Singida ni ya mwisho katika ukusanyaji wa mapato ya ndani katika kipindi cha kuanzia julai mwaka jana hadi machi mwaka huu.
Halmashauri hiyo, imekusanya asilimia 18.4 tu,wakati manispaa ya Singida,imekusanya asilimia 37,Iramba 71.4 na Manyoni 54.
Mbunge wa jimbo la Singida mashariki (CHADEMA) Tundu Lissu, ameapa kwamba wananchi wa jimbo lake watakuwa kwenye likizo ya kuchangia maendeleo yao,hadi hapo ubunge wake utakapokoma.
Kwa hisani ya Mo Blog
Kwa hisani ya Mo Blog
0 comments:
Post a Comment