Home » » Bil. 1.5/- kutumika kubadili maisha ya Wahadzabe

Bil. 1.5/- kutumika kubadili maisha ya Wahadzabe

Baadhi ya wanajamii ya Wahadzabe inayoishi Wilayan Mkalama mkoani Singida.
 
Zaidi  ya Sh. bilioni 1.5 zitatumika kusaidia jamii ya Wahadzabe inayoishi Wilayan Mkalama mkoani Singida ili ibadili maisha yao kutoka kutegemea mizizi, nyama na matunda pori kama chakula chao kikuu hadi kuwa watu wanaojishughulisha na maisha ya kisasa. 
Fedha hizo amabazo zitatokana na vyanzo mbalimbali ikiwamo serikali, wafadhili na wahisani, zitatumika kuhifadhi msitu wao wa asili, kuweka miundombinu ya maji, elimu, barabara, kilimo na ufugaji bora kulingana na mahitaji ya matumizi bora ya ardhi yao.

Kwa mujibu wa Ofisa Maendeleo wa halmashauri hiyo, Patrick Mdachi, mbele ya Baraza la Madiwani, lengo ni kunusuru kabila hilo lisipotee nchini kutokana na malezi yatakayotolewa na asasi itakayoanzishwa na kusimamiwa na Wahadzabe wenyewe.

“Wahadzabe ni kati ya makabila manane mkoani Singida, mengine ni Wanyiramba, Wanyaturu, Wakimbu, Wagogo, Wanyisanzu, Wasukuma na Wataturu (Wabarbaig)... jamii ambayo bado inaishi maisha ya  kizamani (maisha ya ujima), huku chakula chao ni nyama za porini, asali, matunda mwitu na mizizi ya miti,” alisema Mdachi.

Ofisa Maendeleo huyo alisema makabila hayo hasa Wasukuma na Wabarabaig, wamekuwa wakifanya kazi zao za ufugaji kiholela na kufyeka misitu ovyo, hivyo kusababisha wanyamapori kutoweka katika eneo lao la kijiji cha Munguli na kitongoji cha Kipamba.

Mdachi alisema uharibifu wa mazingira unachangiwa pia na baadhi ya viongozi wa vijiji na kata kukubali kupokea `kitu kidogo'  kwa maana ya fedha ili kuruhusu  jamiii ya wafugaji na wakulima kuendelea kuvamia maeneo ya Wahadzabe.

Hata hivyo, baadhi ya madiwani wakiwamo Long’ida Laiser, Hadija Kahola na Philemon Mbogo, walipongeza mpango huo kwa maelezo kuwa  mkakati huo utasaidia na kuimarisha pia sekta ya utalii kutokana na jamii ya Wahadzabe kuwa kivutio kwa wageni wa nje ya nchi.

Aidha, Maugaza Mpanda, ambaye ni Mhadzabe wa kitongoji cha Kipamba katika kijiji cha Munguli, alieleza kufurahisha na mpango huo, lakini akaiomba serikali kuwaondoa kwa nguvu wafugaji wote waliovamia eneo lao ili kurejesha hali halisi ya uoto wa asili kwenye eneo lao la hifadhi.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Mkalama, hivi sasa Wahadzabe wanafikia 352, lakini ifikapo mwaka 2022 wakati wa sensa ya watu wa  makazi, inakadiriwa jamii hiyo itaongezeka hadi kufikia watu 451.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa