Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Padre Seraphine Lesiriam, alisema hayo 
kwenye risala aliyosoma kwa mgeni rasmi Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar 
es Salaam, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo wakati wa ufunguzi wa 
kliniki ya upasuaji wa watoto hospitalini hapo.
Padre Seraphine alifafanua kwamba katika kipindi cha kuanzia mwaka 
2006 hadi 2012 watoto waliohitaji huduma za upasuaji hususani wa moyo 
hupelekwa katika Hospitali ya Bambino Gesu iliyopo Italia.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, kipindi hicho jumla ya watoto 13 
wamenufaika na huduma za upasuaji, kati yao 12 walifanyiwa upasuaji wa 
moyo na mmoja alifanyiwa ‘plastic surgery’.
Hata hivyo aliweka wazi kwamba mwaka jana jumla ya wagonjwa wa nje 
9,450 wenye chini ya miaka mitano walihudumiwa wakati wagonjwa wengine 
wa nje 36,353 wenye zaidi ya miaka mitano walihudumiwa hospitalini hapo.
Kuhusu wagonjwa waliolazwa, alisema kwa kipindi cha mwaka uliopita 
jumla ya wagonjwa 8,133 ambao kati yao watoto ni 3,711 walilazwa 
hospitalini hapo.
Padre Lesiriam alibainisha kwamba uwepo wa huduma za upasuaji kwa 
watoto na tiba nyingine katika hospitali hiyo ni tunda la moyo wa 
ukarimu na ushirikiano kati ya hospitali ya Bambino Gesu na Shirika la 
Wamishenari wa Damu Azizi.
Akifafanua zaidi, mkurugenzi huyo alisisitiza kwamba hospitali ya 
Bambino Gesu imechangia euro 250,000 sawa na zaidi ya sh 525,000,000 ili
 kuanzisha huduma za upasuaji kwenye kliniki ya watoto.
“Fedha hizo zimetumika kwenye ununuzi wa vifaa na kufanya marekebisho
 kwenye mojawapo ya majengo katika idara ya watoto ili kuanzisha huduma 
hizi za upasuaji,” alisisitiza padre huyo.
Rais wa hospitali ya Bambino Gesu, Profesa Giuseppe Profiti, akinukuu
 maandiko matakatifu alisema: “Msifanye mambo mema kwa ajili yetu tu 
bali mnapaswa kufanya mambo mema kwa ajili ya wengine pia.”
Hata hivyo, aliweka bayana kwamba wao wanapenda kushirikiana nao na 
watafanya kila kitu ambacho wataweza kukifanya, hivyo alitumia fursa 
hiyo kuomba msaada kwa watendaji wa hospitali hiyo ili wafanikishe 
malengo yao.
Akifungua kliniki hiyo, Kardinali Pengo alitumia fursa hiyo kuwaasa 
viongozi wa vyama vya siasa na serikali kutoingilia na kuharibu ufanisi 
wa huduma zinazotolewa na wafadhili kwa Watanzania ambao kwa namna moja 
au nyingine hawana uwezo  wa kuzilipia.
Alifafanua kuwa huduma zinazoanzishwa kwa faida ya watu wasiokuwa na 
uwezo, hususani watoto, zinatakiwa zisiingiliwe na baadhi ya watu ambao 
wanataka kwa manufaa yao.
Awali Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Hassani Liana, alisema 
serikali inatambua ushirikiano unaofanywa na watu binafsi na mashirika 
ya dini hasa kwenye afya na elimu hapa nchini.
Chanzo;Tanzania Daima  
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
0 comments:
Post a Comment