KUKITHIRI kwa vitendo vya ukeketaji kwa watoto wachanga katika Mkoa
wa Singida, kumefanya maadhimisho ya kupinga vitendo hivyo kwa mwaka
huu kufanyika mkoani humo ili kutoa elimu kwa wananchi.
Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), Imelda Urio,
alitoa kauli hiyo jijini Dae es Salaam jana kwa niaba ya Mtandao wa
Kupinga Ukeketaji unaojumuisha jumla ya mashirika 12.
Urio alisema maadhimisho hayo yanayotarajiwa kufanyika Februari 6,
wanaamini wataweza kufikisha elimu ya kupinga vitendo hivyo ambavyo
vina athari kwa watoto na wanawake.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, mtandao ulishajaribu kupambana na
vitendo hivyo kwa kuwakagua watoto pindi wanapopelekwa kiliniki, lakini
zoezi hilo lilishindikana kutokana na kina mama kuacha kuwapeleka
watoto, hivyo kuwanyima haki ya kupata chanjo nyingine zitakazosaidia
kulinda afya zao.
Alitaja athari zinazotokana na ukeketaji kuwa ni fistula, kupata
shida wakati wa kujifungua, kupata maumivu wakati wa tendo la ndoa na
kupata athari za kisaikolojia.
Hata hivyo, kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2012 mikoa inayoongoza kwa
vitendo hivyo na asilimia kwenye mabano ni Manyara (71), Arusha (55)
na Mara (40).
Kutokana na hali hiyo, waliitaka serikali kuonyesha utashi wa kisiasa
kwa kutekeleza sera na mpango wa kitaifa wa kupinga na kutokomeza
ukeketaji kwa kufuatilia utendaji wake ili kutokomeza mila kandamizi.
Kwa upande wa asasi, Urio alitaka ziendelee kupiga kampeni za
ushawishi na inapobidi kupitia tena mikakati ili kuleta matukio mazuri
na ya kudumu.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment