Wajumbe baraza la katiba wataka nafasi ya mgombea binafsi iondolewe kwenye katiba mpya

WAJUMBE wa baraza la maoni ya Katiba mpya katika Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, wamependekeza kuondolewa kwa kipengele cha mgombea huru katika nafasi za udiwani, ubunge na Raisi.
Wajumbe  hao wamesema kuwa ni vyema wagombea wote wa nafasi hizo wakatokana na vyama vya siasa, ili kupunguza uwezekano wa kumuingiza madarakani kiongozi ayesiyekuwa na maadili mazuri.
Wakizungumza kwenye kikao cha  baraza  la maoni ya katiba mpya wilaya ya Ikungi mkoani Singida leo,  baadhi ya wajumbe wamesema  wagombea wanaotokana na vyama vya siasa hupigiwa kura za  maoni na kuchunjwa kwenye vikao kabla ya  kuwepewa tiketi ya kuwania nafasi husika.
Wamesema kitendo cha kuruhusu mgombea huru,  kinaweza kusababisha watu wenye ushawishi mkubwa wa kifedha kutumia vibaya fursa hiyo kununua uongozi  na kuingiza nchi kwenye  utawala wa kiditeta.
Hata hivyo Mwenyekiti wa kikao hicho Ali Salehe amesema kuwa  kuondolewa kwa kipengele hicho,  pia kunaweza kuwanyima fursa baadhi ya wagombea  wazuri wanaoshindwa kupambana na wenye  fedha katika ngazi za vyama.
Baraza la maoni  ya katiba mpya Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida lenye wajumbe zaidi ya 100 limemaliza vikao vyake  vya siku mbili kwa kutoa mapendekezo mbalimbali katika rasimu hiyo ya Katiba.

Nyara za Serikali zawafikisha polisi



JESHI la Polisi Mkoa wa Singida, linawashikilia watu wawili kwa tuhuma ya kumiliki nyara za Serikali kinyume na sheria. Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Geofrey Kamwela aliwataja watu wanaoshikiliwa kuwa ni Esinasi Stephano (36) mkazi wa Kijiji cha Chikuyui. Alisema mtuhumiwa alikamatwa kwa kosa la kumiliki meno mawili ya tembo yenye uzito wa kilo tano na thamani ya zaidi ya Sh milioni 4.4.

Alisema mtuhumiwa huyo, alikamatwa juzi jioni baada ya raia wema kutoa taarifa polisi.

Alimtaja mtuhumiwa wa pili kuwa ni, Mwanandi Amani (34) mkazi wa Kijiji cha Mitundu ambaye alikamatwa na mkia wa tembo, meno mawili ya ngiri, mafuta ya samba na sare moja ya Jeshi la Polisi.

Alisema mtuhumiwa huyo, alikamatwa baada ya raia wema kutoa taarifa juu ya umilikaji wake wa nyara za serikali kinyume na sheria.

Katika hatua nyingine, alisema wameanzisha msako mkali wa kusaka watu wanne waliomvamia mmiliki wa duka Miraji Abdallah (45) mkazi wa Kijiji cha Mtunduru na kupora simu 15 za kiganjani.

Alisema watu hao, wanaodhaniwa ni majambazi, kabla ya kupora simu hizo ambazo thamani yake bado haijajulikana, walimjeruhi vibaya Miraji na watu wengine Hamisi Hamisi (30) na Hatibu Idde (18) kwa kutumia visu.

CHANZO HABARI LEO

HABARI YA KUSIKITISHA: MWANAFUNZI WA DARASA LA TATU AUAWA KIKATILI






Mwanafunzi wa darasa la tatu katika shule ya msingi Kizega wilayani Iramba Bi. Mariamu Alphonce mwenye umri wa miaka kumi ameuwawa kikatili kwa kukatwa shingo na kucharangwa kwa panga sehemu mbalimbali za mwili wake na kaka yake bwana Elibariki  Alphonce. 

Akieleza kwa uchungu baba wa mtoto huyo bwana Alphonce Msengi amesema alipofika nyumbani kwake majira ya saa kumi na moja jioni alikuta damu nyingi na alipo angali vizuri alimuona mtoto wake Mariamu Alphonce akiwa amekatwakatwa kwa mapanga na tayari alikuwa ameshafariki.

Bwana Msengi baada ya kuona hivyo alipiga yowe na walikuja majirani na watoto na wakamwambia tumemuona mtoto wako Elibariki akiwa na mapanga mawili akikimbia huku akiwa hana nguo. 


Wakieleza mwenyekiti wa kitongoji Bi Vailet Mbigu na mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kizega bwana Elisante Gyuzi wamesema pamoja na shule kuandaa taratibu zote za mashishi , kijana aliyefanya unyana huo huwa anavuta bangi na mara nyingi alikuwa akisikika kumtishia kumuuwa baba yake kwa kumkata kwa panga.




Kwa upande wake  kaimu mganga mkuu wa hospitali ya wilaya ya Iramba daktari Timoth Sumbe amesema wamempokea Mariamu Alphonce akiwa ameshafariki huku mwili wake ukiwa na majeraha ya kukatwakatwa sehemu ya shingoni,kichwani.




Akiongea kwa simu kamanda wa jeshi lapolisi mkoani Singida bwana Godfrey Kamwela amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo na jeshi lake lina endelea kumsaka mtuhumiwa bwana Elibariki Alphonce ambaye alitoweka baada ya mauaji ili aweze kufikishwa mahakamani. 



SOURCE: ITV

Magunia ya mkaa 311 yaliyovunwa kinyemela yakamatwa Singida

WAKALA wa huduma za Misitu  nchini  katika  halmashauri ya wilaya ya Singida,amefanikiwa kukamata magunia ya mkaa 311 yenye thamani ya zaidi ya shilingi 5.2 milioni, ambayo yamevunwa kinyume na sheria.

Meneja wa wakala huyo wilayani Singida bwana Hashimu Kativo, amesema magunia hayo wameyakamata  mapemawiki hii katika msako mkali unaoendelea wa kuwakamata wafanyabiashara na watu wengine wanaouza  mazao ya misitu na nyuki kinyume na sheria za  nchi.

Amesema  magunia hayo yamekamatwa katika kijiji cha Tupendane kata ya Mang’onyi baaada ya kukuta magunia hayo yakiwa yamekusanywa  bila kuwa na kibal cha kuvuna wala leseni ya kununua na kuuza mkaa.

Hata  hivyo amefafanua kuwa wamiliki wa mkaa huo waliweza kutoroka kwenda kusikojulikana.

Bw Katiyo amesema katika ukamataji huo, pia wameharibu matanuru sita makubwa ambayo yalikuwa yakitumika kuchoma mkaa kwa ajili ya kuuza.

Yunde ashinda kwa kishindo kugombea Uenyekiti wa halmashauri ya Ikungi mkoani Singida.

DSC01915
Katibu wa CCM wilaya ya Ikungi mkoa wa Singida, Joseph Rudisha akitoa mwongozo kwenye mkutano wa uchaguzi wa kuchagua mwenyekiti na makamu wake wa halmashauri ya wilaya hiyo mpya.Wa kwanza kulia ni mgombea pekee wa nafasi ya uenyekiti Celestine Yunde.
DSC01919
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ikungi, Hassan Tati akizungumza kwenye mkutano wa uchaguzi wa nafasi za mwenyekiti na makamu wake wa halmashauri ya wilaya mpya ya Ikungi. Mkutano huo ulifanyikia kwenye ukumbi wa mikutano wa chuo cha maendeleo ya wananchi mjini Singida.Wa kwanza kulia ni mgombe wa nafasi ya mwenyekiti Celestine Yunde na kushoto ni mgombe wa nafasi ya makamu mwenyekiti, Alli Nkhangaa.
DSC01926
Mgombea wa nafasi ya mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ikungi, Celestine Yunde akiomba kura kwa wajumbe (hawapo kwenye picha) wa mkutano wa uchaguzi wa kuchagua wagombea watakaopambana na wagombe kutoka CHADEMA. Kulia ni katibu wa CCM wilaya ya Ikungi, Joseph Rudisha na kushoto ni mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ikungi, Hassan Tati.
DSC01917
Baadhi ya madiwani waliohudhuria mkutano wa uchaguzi wa CCM wilaya ya Ikungi wanaowania nafasi ya mwenyekiti na makamu mwenyekiti katika halmashauri ya wilaya hiyo.Mkutano huo ulifanyikia katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha maendeleo ya wananchi mjini Singida.(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Celestine Yunde wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) halmashauri ya wilaya ya Ikungi, amechaguliwa kwa kishindo kuwania nafasi ya mwenyekiti wa halmashauri hiyo.
Yunde ambaye alikuwa mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Singida kabla ya wilaya hiyo kuzaa halmashauri mpya ya Ikungi, alipata kura 29 za ndio na moja ilimkataa.
Kwa ushindi huo mnono, Yunde atapambana na mgombea kutoka CHADEMA iwapo chama hicho cha upinzani, kitaamua kutoa mgombea.
CHADEMA ina madiwani wawili katika wilaya ya Ikungi.
Nafasi ya makamu mwenyekiti imenyakuliwa na Alli Nkhangaa ambaye naye alipata kura 29 za ndio na moja ilimkataa.
Mapema akizungumza kwenye mkutano huo wa uchaguzi, Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ikungi Hassan Tati, amewahimiza madiwani hao kuhakikisha wanaimarisha umoja wao ili chama kiendelee kuwa na nguvu za kushinda chaguzi mbalimbali.
Wakati huo huo, Katibu wa CCM wilaya ya Singida vijijini Mwanamvua Kilo, amesema mkutano wa uchaguzi wa nafasi ya mwenyekiti na makamu wake katika halmashauri hiyo umeahirishwa hadi hapo baadae.
Amesema mkutano huo uliokuwa ufanyike juzi, pamoja na madiwani wote wa halmashauri hiyo kuhudhuria, haukufanyika kutokana na hitilafu zilizojitokeza mara tu baada ya mkutano huo kuanza.
Amesema hawezi kwa sasa kusema ni nini kilichotokea kwenye mkutano wao, ila ifahamike tu kwamba uchaguzi huo utarudiwa baadae katika siku itakayopangwa.
KWA HISANI YA MO BLOLG

Wakulima wa viazi vitamu mkoani Singida walalamikia bei wanayolazimishwa na wafanyabiashara.

E83A0368
 Makuli kumi wakipakia juu ya lori gunia moja la viazi vitamu lenye zaidi ya kilo 150 lenye thamani ya shilingi 35,000.Wakulima wa zao la viazi vitamu tarafa ya Ihanja wilaya ya Ikungi mkoa wa Singida,wamelalamikia ujazo huo pamoja na bei wanayopewa kwa madai kuwa ni ya kinyonyaji.
E83A0363
Magunia ya zao la viazi vitamu katika kijiji cha Ighuka wilaya ya Ikungi,vikiwa tayari kusafirishwa ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kwenda kuuzwa.
E83A0364
Lori ambalo dereva wake aliomba lisitajwe namba zake za usajili likiwa linapakia magunia ya viazi vitamu katika kijiji cha Ighuka wilaya ya Ikungi.(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel  Limu.
Wakulima wa zao la viazi vitamu tarafa ya Ihanja wilaya ya Ikungi mkoani Singida wamelalamikia tabia ya wafanyabiashara ya kuwalazimisha kuuza gunia lenye uzito wa kilo zaidi ya 150 kwa bei ndogo ya shilingi 35,000.
 Wamedai kwamba ujazo huo wa gunia la viazi vitamu unaojulikana kwa jina la ‘polo’, unachangia wakulima kunyonywa mapato yao.
 Wakizungumza kwa nyakati tofauti na MO Blog, wakulima hao wamedai kuwa gharama wanazotumia katika kulima na ile ya kusafirisha hadi barabarani zao la viazi vitamu, haiwezi kurudi kwa bei wanayopewa na wafanyabiashara hao.
Mmoja wa wakulima hao Doricus Hussein, amesema wafanyabiashara hao wanaotoka katika mikoa ya Dodoma, Tanga, Dar-es-salaam, Zanzibar pamoja na visiwa vya Comoro, wamekuwa hawako tayari kununua zao hilo kwa kutumia vipimo kwa madai kuwa hakuna soko litakalonunua viazi vitamu kwa kutumia mizani.
 Alitumia fursa hiyo kuiomba serikali ya kijiji kwa ushirikiano na halmashauri ya wilaya ya Ikungi,kuangalia uwezekano wa kuwasaidia wakulima wasiendelee kunyanyaswa na kudhulumiwa na wafanyabiashara hao.
 Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji wa kata ya Pum Miraji Ntungu, amesema kuwa licha ya kupiga marufuku ujazo wa rumbesa unaolalamikiwa na wakulima hao, lakini ni wakulima wenyewe ndio wanaopingana na agizo hilo kwa madai kuwa serikali haijawasaidia kutafuta mbegu ya viazi vitamu.
 Ntungu amesema kwa siku moja magunia yasiyopungua 200 husafirishwa kutoka kijiji cha Puma pekee kwenda kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi, ambapo kila gunia hulipiwa ushuru wa shilingi elfu moja.
 Kwa upande wao wafanyabiashara hao wanaolalamikiwa, wamedai kuwa hakuna soko linaloweza kununua gunia la viazi vitamu  lisilo kuwa na ujazo wa rumbesa iliyopitiliza.
 Mmoja wa wafanyabiashara hao Bw. Shabani Hamisi Bilali, amesema pia wanawataka wakulima hao kujaza gunia ujazo huo wa rumbesa ili pamoja na mambo mengine, wao waweze kufidia gharama za upakiaji na  usafirishaji  na hivyo kupata faida inayokidhi mahitaji.
 Na Mo Blog

Wakulima wilaya ya Singida watakiwa kuhakikisha wanaweka akiba ya chakula pindi wanapovuna mazao yao.

MLOZI 2
Mkuu wa wilaya ya Singida mwalimu Queen Mlozi, ameiagiza idara ya kilimo na mifugo kuangalia uwezekano wa kuanzisha siku maalumu ya sherehe za wakulima ngazi za kata ili pamoja na mambo mengine, wakulima wengi zaidi waweze kutumia fursa hiyo kujifunza kilimo bora.
Mlozi ametoa changamoto hiyo wakati akizungumza kwenye kilele cha sherehe za wakulima wa halmashauri ya wilaya ya Singida zilizofanyika katika kijiji cha Masweya tarafa ya Ilongero.
Amesema utamaduni wa kuendelea kufanya sherehe za wakulima mjini Dodoma kunawanyima fursa wakulima wengi na hasa wadogo kuonyesha mazao yao na pia kujifunza mbinu bora za kilimo.
Mlozi amefafanua kuwa, kama tutasogeza maonyesho ya wakulima hadi ngazi ya kata, faida zake ni nyingi mno kuliko kufanyia mahali ambapo wakulima wetu wengi hawawezi kufika. Faida mojawapo ni kwamba wakulima watajifunza mbinu bora za kilimo na kwa njia hiyo, malengo ya kilimo kwanza, yatafikiwa.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya Mlozi amewataka wakulima kutumia vizuri mazao watakayovuna msimu huu na kuhakikisaha wanaweka chakula cha kutosha familia kwa kipindi chote cha mwaka.

CHANZO : MO BLOG

MWANAMKE AFUNGWA MIAKA 3 KWA KOSA LA KUMNG'ATA MUMEWE SEHEMU ZA SIRI HUKO IRAMBA SINGIDA







MAHAKAMA ya Wilaya ya Iramba mkoani Singida 
umemhukumu mwanamke mmoja mkazi wa kijiji
 cha Kisana wilayani humo, Sayuni Ramadhani (42)
 kwenda jela miaka mitatu baada ya kukiri kosa la 
kumng’ata mumewe sehemu zake za siri.Mwendesha 
mashitaka mkaguzi wa polisi, Vincent Ndasa alidai mbele 
ya hakimu mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Iramba,
 Kariho Mrisho kuwa Juni 4 mwaka huu saa 12.00 jioni
 katika kijiji cha Kisana, mshitakiwa kwa makusudi 
alizing’ata kwa meno sehemu za siri za mume wake, 
Onesmo Nathania (42) na kumsababishia maumivu.

Ndasa alidai kuwa siku ya tukio, wanandoa hao 
waliporejea nyumbani kutoka kwenye klabu cha 
pombe ya kienyeji kijijini hao, kulitokea kutokuelewana
 na hivyo kuanza kugombana.Alidai wakati wanaendelea 
kupigana, Onesmo alizidiwa nguvu na kuangushwa chini
 na mkewe ambaye alifungua zipu ya suruali na kufanikiwa 
kuzitoa sehemu za siri za mumewe na 
kuzing'ata nusura azitenganishe.
Mwendesha mashitaka aliendelea kudai
 kuwa mlalamikaji Onesmo alipiga yowe na 
majirani walifika mara moja na kumkimbiza
 katika zahanati ya kijiji kwa ajili ya matibabu.


Mshitakiwa alipoulizwa iwapo ni kweli alikiri 
kosa na akaiomba mahakama imwonee huruma
 kwa kumpa adhabu ndogo kwa kuwa hilo lilikuwa
 ni kosa lake la kwanza na kwamba anahitaji kuwa 
na mumewe ili waendelee kulea idadi 
kubwa ya watoto wao kwa pamoja.
Naye mwendesha mashitaka, Ndasa aliiomba
 mahakama kumpa adhabu kali mshitakiwa
 ili kuwa fundisho kwake na pia kuogofya wanawake 
wanaotarajia kuwafanyia unyama wa aina hii ya
 kung’ata sehemu nyeti za waume zao.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mfawidhi Mrisho,
 alisema mahakama yake imezingatia kwa makini 
maombolezo ya mshitakiwa na kufikia uamuzi wa
 kutoa adhabu ya kutumikia jela miaka mitatu.











Asilimia kubwa ya Wakazi wa Singida waweka wazi kuwa hawakuona umuhimu wa kusikiliza uwasilishaji wa rasimu ya katiba.



Sehemu ya wakazi wa Singida katika mkutano wa hadhara.
Na Nathaniel Limu.
Wakazi wa wa Singida mjini asilimia kubwa hawakusikiliza rasmu ya katiba iliyosomwa tarehe 3/6/2013, kwa kile walichodai kuwa kuisikiliza au kutokuisikiliza ni sawa tu, kwa madai kuwa hata wakitoa maoni yao kurekebesha baadhi ya vipengele, havitafanyiwa kazi.
Fundi cherehani Ali Soghweda.akizungumzia suala hilo amesema “Binafsi sikuona faida yo yote ya kusikiliza uwasilishaji wa rasmu ya katiba hiyo, kwa sababu imekusanya maoni ya Watanzania wengi wa ngazi mbalimbali, basi mi nipo pamoja nao katika maoni yao”.
Hata hivyo, Katibu wa TCCIA mkoa wa Singida Culvert Nkurlu, amesema rasmu hiyo haija ainisha vizuri juu ya ardhi na kwa maana hiyo, haitawanufaisha wananchi hasa wale walioishi kwenye eneo husika kwa miaka mingi.
Amesema kuiacha ardhi kwenye mamlaka ya rais, kunawanyima haki ya wananchi walioishi kwa miaka mingi kwenye maeneo hasa yanayogundulika kuwa na madini.
Amesema “Hivi sasa tunashuhudia wawekezaji wakiwatoa wananchi walikokaa kwa miaka mingi katika eneo husika, bila kuwapa fidia ya kukidhi mahitaji. Wananchi wa aina hiyo, katiba inatakiwa kuwapa umuhimu ili waweze kufaidika na ardhi yao”.
Naye Mwenyekiti wa TLP wilaya ya Singida, Athumani Nkii, ameipongeza rasimu hiyo kwa matakwa yake ya kutaka kuwepo kwa marasi watatu, Tanzania bara, Tanzania visiwani na yule wa muungano.
Nkii ambaye pia ni fundi cherehani, amepongeza pia utaratibu wa kufuta ubunge wa viti maalum na kupendekeza uwepo wa mgombea binafsi.
Ameongeza kuwa “Maoni ya kuwa spika wa bunge asitokane na wabunge, hiyo pia ni nzuri, spika na msaidizi wake atoke kwenye kamati huru ya uchaguzi ambayo haitatokana na kuteuliwa na rais”.

NA MO BLOG

DEWJI ATOA MISAADA KATIKA JIMBO LA SINGIDA


E83A0131
Picha juu na chini ni Mbunge wa jimbo la Singida mjini, Mh. Mohammed Gullam Dewji akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kituo cha mabasi cha zamani mjini Singida.
E83A0112
Baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara ulioitishwa kwa ajili ya mbunge wa jimbo la Singida mjini Mh. Mohammed Gullam Dewji kuzungumza na wananchi wa jimbo lake.
E83A0094
Mbunge wa jimbo la Singida mjini, Mh. Mohammed Gullam Dewji, akiwa anasalimiana na Wana CCM na wananchi wa Singida mjini kwenye kituo cha mabasi cha zamani mjini Singida.


Na Nathaniel Limu.
Mbunge wa Singida mjini (CCM) Mh. Mohammed Gullam Dewji amemwaga misaada mbalimbali ikiwemo kuwaongezea mitaji wauza kahawa chungu, ambayo haijawahi kutolewa jimboni humo na mbunge au mfadhili yeyote kwa wakati mmoja, kabla na baada ya Tanzania kupata uhuru.
Misaada hiyo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 87.9, ni pamoja na mabati 100 na mifuko ya saruji 100, kwa kila shule 17 za sekondari jimboni humo.
Misaada mingine ni vyereheni viwili kwa kila kata 19 na cherehani moja kwa kila tawi la CCM jimboni humo.

Pia vikundi 16 vya wajasiriamali vikiwemo vya kung’arisha viatu, mafundi baiskeli, wapiga debe wa vituo vya mabasi, wasukuma matoroli, wakereketwa wa mashina ya CCM, watengeneza viatu vya kienyeji na baba, mama lishe, kila kimoja kimeongezewa mtaji wa shilingi 500,000 taslimu.

Vifaa hivyo na mitaji ya biashara, vimetolewa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kituo cha zamani cha mabasi mjini Singida.

Akizungumza kwenye mkutano huo wa hadhara uliohudhuriwa na maelfu ya wana-CCM na wananchi kwa ujumla, Mh. Dewji amesema msaada huo ni mwendelezo wa misaada yake anayoitoa kwa ajili ya kuiunga mkono serikali katika kuwatumikia wananchi.

Amesema pia kuwa misaada hiyo ni sehemu yake ya utekelezaji wa ilani ya CCM katika kuwatumikia wananchi wa jimbo la Singida mjini.

Amesema “Tunatakiwa tujitume usiku na mchana, ili tuhakikishe kila tuliyoyaahidi kwenye ilani yetu, yote tumeyakamilisha, vinginevyo wananchi hawatatuelewa. Wananchi wanahitaji utimilifu wa ahadi na sio uhodari wa kujieleza kwenye majukwaa”.

Katika hatua nyingine, Mh. Dewji ametumia fursa hiyo kuwaomba viongozi na watendaji kuendelea na moyo safi wa kuwatumikia wananchi bila kuchoka.
Amesema pia wawe waaminifu na waadilifu kwa wananchi na waongozwe kwa dhamira iliyo njema, yenye uzalendo wa kuipenda nchi yetu na watu wake.

Mbunge Dewji amesema “Tuendelee kuhubiri amani na utulivu kwenye majukwaa, wakati wote tuwaelekeze wananchi kwenye kujiletea maendeleo endelevu ya wakati huu na wakati ujao”.

Kesi ya diwani wa kata ya Mungaa mkoani Singida kupitia tiketi ya CHADEMA ya kukatakata Ng’ombe sita kuunguruma kesho.


DSC01222

Diwani wa CHADEMA kata ya Mungaa jimbo la Singida Mashariki, Matheo Alex (wa pili kushoto aliyenyanyua mkono juu) akiwa katika chumba cha mahakama ya hakimu mkazi mjini Singida akisubiri kusomewa shitaka lake la kukata kata ng’ombe sita mali ya Mary John mkazi wa kijiji cha Minyinga kata ya Mungaa.Wa pili kulia ni mtoto wa diwani Alex, Faraja na wa pili kushoto Bahati Sumbe (mwenye jacketi la njano) wameunganishwa kwenye kesi moja na diwani Alex.
Na Nathaniel Limu.
Kesi ya kukata kata ng’ombe sita inayomkabili diwani wa kata ya Mungaa kupitia tiketi ya CHADEMA, jimbo la Singida Mashariki Matheo Alex na washitakiwa wenzake wawili, inatarajiwa kuunguruma kesho asubuhi kwenye mahakama ya hakimu mkazi mjini Singida.
Washitakiwa wengine ni mtoto wa diwani huyo Faraja Matheo na mwingine ni mjomba wa diwani huyo Bahati Sumbe.
Ng’ombe hao waliokatwa katwa ni mali ya Mary John mkazi wa kijiji cha Minyinga kata ya Mungaa jimbo la Singida mashariki na wana thamani ya zaidi ya shilingi milioni 3.5 milioni.
Mei 17 mwaka huu wakati washitakiwa hao walipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza, mwendesha mashitaka Mussa Chemu amedai kuwa mnamo Mei 13 mwaka huu saa 5.00 asubuhi huko katika kijiji cha Minyinga, kwa makusudi washitakiwa wote kwa pamoja walishirikiana kukata kata ng’ombe sita mali ya Mary John.
Washitakiwa wamekana shitaka hilo na wako nje kwa dhamana ya kila mmoja amedhaminiwa na watu wawili ambao kila mmoja ametoa ahadi ya dhamana ya shilingi milioni tano.
Washitakiwa hao wanatetewa na wakili maarufu Tundu Lissu ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Singida Mashariki.
 Chanzo Mo Blog

TANGAZO LA MAUZO YA NYUMBA ZA MFUKO WA PENSHENI KWA WATUMISHI WA UMMA (PSPF)


MFUKO WA PENSHENI KWA WATUMISHI WA UMMA
(PSPF)
 


MAUZO YA NYUMBA ZA PSPF
Mfuko unapenda kuwataarifu wananchi wote kwamba inauza nyumba zilizojengwa na Mfuko katika mikoa ya Dar es Salaam- Ilala (Buyuni), Morogoro (Lukobe), Tabora (Usule), Mtwara (Mang’amba) na Shinyanga (Ibadakuli).
Bei ya nyumba ni kati ya Tsh 59,000,000.00 hadi Tsh 80,000,000.00 (Bila ya VAT) kulingana na ukubwa wa nyumba na Mkoa nyumba ilipo.   Ukubwa wa nyumba ni kuanzia vyumba viwili hadi vinne. Fomu zinapatikana kwa gharama ya shilingi elfu tano (TShs. 5,000/=) kwenye ofisi za Mfuko zilizopo mikoa yote nchini.
Waombaji wanaohitaji kuona na kukagua nyumba wawasiliane na Mfuko kupitia namba 2120912/52 au 2127376.
“PSPF - Tulizo la Wastaafu”
Kwa maelezo zaidi wasiliana na:
Mkurugenzi Mkuu,
Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF),
Golden Jubilee Towers,
Front Tower – Ghorofa ya 6-13,
Mtaa wa Ohio/Kibo,
S. L. P. 4843,
DAR ES SALAAM.
Barua Pepe: pspf@pspf-tz.org          


 Tovuti: www.pspf-tz.org  

PSPF YAFUNGUA OFISI ZAO NJOMBE NA KATAVI







Mh. Tundu Lissu amwaga sera ndivyo sivyo.

DSC01254
Mbunge wa jimbo la Singida mashariki Mh. Tundu Lissu akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni ya nafasi ya udiwani kata ya Iseke tarafa ya Ihanja wilaya ya Ikungi uliofanyika katika kijiji cha Iseke.
DSC01259
DSC01240
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Iseke tarafa ya Ihanja waliohudhuria uzinduzi wa kampeni ya udiwani kata ya Iseke uliofanywa na chama cha CHADEMA.
DSC01255
Baadhi ya viongozi wa CHADEMA waliohudhuria uzinduzi wa kampeni ya udiwani wa kata ya Iseke tarafa ya Ihanja wilaya ya Ikungi.(Picha zote na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Mgeni rasmi katika kampeni ya uzinduzi wa nafasi ya udiwani kata ya Iseke tarafa ya Ihanja wilaya ya Ikungi Mh. Tundu Lissu, ameashindwa kuuza sera za CHADEMA na badala yake ametumia muda na nguvu nyingi kuhimiza sera yake ya ‘katazo’ la wananchi kuchangia maendeleo yao .
Mh. Tundu Lissu ambaye ni mbunge wa jimbo la Singida Mashariki kupitia tiketi ya CHADEMA, alipanda jukwaani huku akiwa mabeba makabrasha ya michanganuo ya bajeti ya serikali ya kuanzia mwaka wa fedha wa 2010/2011 hadi 2013/2014.
 Akisema na kushangiliwa kwa nguvu na wananchi waliohudhuria uzinduzi huo uliofanyika katika kijiji cha iseke, Mh Tundu Lissu aliweka wazi kuwa “Mimi sitaki kabisa kuzungumzia habari za Amosi Mghenyi ambaye ametusaliti kwa kuhama CHADEMA na kurejea CCM.  Amosi kisiasa ni mfu, kwa hiyo siwezi kupoteza muda wangu kuzungumiza mambo ya mfu”.
Amesema ufunguzi wake utajikita zaidi katika kuwaelimisha wananchi wa kata ya Iseke kwamba serikali inayo fedha nyingi na za kutosha kugharamia maendeleo ya wananchi.
Akiijengea nguvu hoja yake hiyo, amesema kwa mfano katika mwaka wa fedha wa 2010/2011, mkoa wa Singida, ulipewa zaidi ya shilingi milioni 903 za undeshaji wa shule, lakini zilizotumika ni zaidi ya shilingi milioni 464 na kubaki zaidi ya shilingi 438.2.
 Amesema fedha hizo zaidi ya shilingi 438.2 zilizobaki,  hazijaainishwa zilipelekwa wapi.  “Kwa vyo vyote zitakuwa zimeishia kwenye matumbo ya mgambo na watendaji wa serikali ya CCM”.
Mh. Tundu ambaye pia ni mwanasheria kitaaluma, amewataka wakazi wa kata ya Iseke, kumchagua Emmnuel Jackson Jingu awe diwani wao, ili waondokane na manyanyaso ya michango kama walivyojikomboa wakazi wa jimbo la Singida Mashariki.
 Wagombea wengine wa nafasi ya udiwani kata ya Iseke ni Amosi Munghenyi wa CCM na Abdallah Kinyenje maarufu kwa jina la Petro wa CUF.
 
 
 

CHANZO MO BLOG

MAHAKAMA ya Rufaa yamrejeshea ubunge wa Igunga-CCM Dr. Dalali Peter Kafumu asubuhi ya leo.



 Mbunge wa jimbo la Igunga-Tabora-CCM ndugu Dalaly Peter KAFUMU
 -
Aliyekuwa mbunge wa jimbo la Igunga-Tabora ndugu Dalaly Peter KAFUMU amerudishiwa ubunge wake na mahakama leo hii asubuhi baada ya aliyekuwa mgombea kupitia CHADEMA ndugu Kashinde kushindwa kuwakilisha risiti ya hati ya kiwanja wakati wa kesi ya msingi ya kwanza,Hivyo CHADEMA wamepoteza huko Igunga.FUATILIA
 

Jela Miaka 30 kwa kunajisi mtoto

MAHAKAMA ya Wilaya Manyoni mkoani Singida imemhukumu mkazi wa kijiji cha Matangalala wilayani humo, Maduhu Dotto (31) kwenda jela miaka 30 baada ya kumkuta na hatia ya kunajisi mtoto. Aidha, Maduhu na mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo, Juliana Malungo (28), wametakiwa kulipa faini ya Sh 200,000 kila mmoja. Malungo ambaye ni mkazi wa mtaa wa Chang'ombe mjini Manyoni, alipatikana na hatia ya kula njama na Maduhu na kwamba ndiye aliyefanikisha kitendo cha kunajisi msichana mwenye miaka 14, kwa ahadi ya kumzawadia vitenge binti huyo. Mwendesha Mashitaka, Mrakibu Msaidizi wa Polisi Hamis Fussi alidai mbele ya Kaimu Hakimu wa Wilaya ya Manyoni, Terrysophia Tesha kuwa Aprili 28 mwaka jana saa 6:45 mchana washitakiwa kwa pamoja walikula njama za kumnajisi binti huyo na kumsababishia maumivu makali sehemu zake za siri. Fussi alidai kuwa siku ya tukio Juliana alikwenda nyumbani kwa mlalamikaji ( ambaye ndiye binti alinajisiwa) na kumshawishi binti huyo amsindikize mnadani. Hata hivyo, hawakwenda mnadani, badala yake mshitakiwa alimpeleka binti huyo nyumbani kwake, ambako alikuwepo Maduhu na Juliana alimfungia ndani binti huyo wakiwa na Maduhu, naye akaondoka. Alidai kuwa kutokana na kufungiwa huko, Maduhu aliamua kumwingilia kimwili binti huyo bila ridhaa yake na hivyo kumsababishia maumivu makali sehemu zake za siri. Fussi aliiomba Mahakama itoe adhabu kali kwa washitakiwa, akidai kuwa vitendo vya kunajisi vinachangia mimba zisizotarajiwa na maambukizi ya magonjwa, ikiwemo wa Ukimwi. Akitoa hukumu, Hakimu Tesha alisema kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka, umethibitisha bila kuacha shaka yoyote kuwa washitakiwa walitenda makosa hayo. 
 Chanzo Habari Leo
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa