DIALLO, GUNINITA WACHUKUA FOMU CCM



Na Waandishi Wetu, Dar na mikoani


*Wana CCM wamuonya Lembeli Shinyanga
MCHUANO mkali wa kuwania nafasi za wenyeviti wa CCM wa Mikoa, Tanzania Bara, umeanza.

Katika mchuano huo, baadhi ya vigogo wa CCM katika mikoa mbalimbali wameanza kuchukua fomu ili kutetea nafasi zao na wengine kuwang’oa wenzao walioko madarakani.

Katika Mkoa wa Mwanza, Mbunge wa zamani wa Ilemela, Anthony Diallo (CCM), jana alichukua fomu kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Mwanza.

Wakati Diallo alichukua fomu mkoani humo, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita, naye alichukua fomu ili kutetea nafasi yake hiyo.

Wakati hayo yakiendelea, mkoani Shinyanga nako mchuano mkali unatarajia kuwa kati ya Mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM) na Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Shinyanga, John Mgeja.

Katika Mkoa wa Mwanza, Diallo, ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, (NEC), alichukua fomu hiyo jana saa mbili asubuhi na alikabidhiwa na Katibu Msaidizi wa CCM, Mkoa wa Mwanza, Zubeda Mbaruku, katika makao makuu ya CCM, Mkoa wa Mwanza.

Akizungumza baada ya kuchukua fomu hiyo, Diallo alisema amechukua fomu hiyo kama sehemu ya kutimiza wajibu wake wa kidemokrasia na aliahidi kuwatumikia kikamilifu wana CCM, Mkoa wa Mwanza.

"Mimi ni kiongozi wa watu, naijua CCM, kwa hiyo, nitakaposhinda, nitahakikisha nawaunganisha wana CCM wote bila kubagua na nitapambana na ubaguzi pamoja na makundi ndani ya chama chetu, ili kukifanya kiendelee kuaminika kwa wanachama na wananchi wa kawaida," alisema Diallo.

Wakati Diallo akichukua fomu, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Mwanza anayemaliza muda wake, Clement Mabina, naye alichukua fomu ili kutetea nafasi yake hiyo.

Mbunge wa Kwimba, Shanif Hiran Mansoor (CCM), yeye alichukua fomu ili kutetea nafasi yake ya Mweka Hazina wa chama hicho, Mkoa wa Mwanza kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Wakati mchuano ukiwa hivyo jijini Mwanza, jijini Dar es Salaam nako mchuano umeanza, baada ya Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita, kuchukua fomu ya kutetea nafasi yake hiyo jana.

Guninita alikabidhiwa fomu hiyo jana na Katibu wa CCM, Mkoa wa Dar es Salaam, Abilahi Mihewa, makao makuu ya chama hicho, Mkoa wa Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa kuchukua fomu hiyo, Guninita alisema akifanikiwa kuendelea na nafasi hiyo, atajenga uchumi wa kisasa na kiusalama kupitia miradi mbalimbali ya chama hicho.

Alisema pia kwamba, anatarajia pia kujenga mazingira ya kukuza uchumi kwa kuimarisha miradi yote ya chama.

Pia alijigamba kwamba, katika kipindi cha miaka mitano alichokuwa madarakani kwa kushirikiana na viongozi wenzake mkoani Dar es Salaam, amefanikiwa kutambua mali zote za chama, vikiwemo viwanja 300 na kwamba kati ya viwanja hivyo, 150 vimepata hati kwa ajili ya kupata uwekezaji unaoeleweka.

“Nimekuwa mwenyekiti kwa miaka mitano, nimejipima na kuona naweza kuwaongoza wana CCM katika kipindi kingine, ninawaomba na wanachama wapime uwezo wangu kama ninafaa tena kuonyesha uwezo wangu.

“Kikubwa tunachotaka ni kuhakikisha tunajenga uchumi wa kisasa na kiusalama kwa mali za CCM, vikiwemo viwanja.

Kuhusu changamoto za vyama vya upinzani, kikiwamo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho kinaaminika kuungwa mkono zaidi na vijana, alisema:

“Kigezo cha chama chochote cha siasa kukubalika ni ushindi katika chaguzi zinazoshirikisha vyama vyote, kwa hiyo, CCM bado tuko juu, maana katika majimbo ya Dar es Salaam, tuliweza kushinda viti sita kati ya vinane, udiwani tulifanikiwa kuchukua kata 77 kati ya 90, sasa kwa nini tusiseme bado tunakubalika?” alihoji Guninita.

Kwa upande wake, Mihewa aliwaonya wana CCM wanaoomba nafasi za kugombea katika Mkoa wa Dar es Salaam, wahakikishe wanafuata sheria na kanuni zilizowekwa na chama chao.

“Nawasihi wagombea wote wasifanye kampeni za aina yoyote, wasubiri mpaka siku ya uchaguzi, ni marufuku kukutana, kuwakusanya wapiga kura na kuwasalimia, wasubiri siku yenyewe watakapokutana na wajumbe, atakayebainika akikiuka taratibu, ajue vikao vitamwengua mara moja” alionya Mihewa.

Wakati Dar es Salaam na Mwanza mchuano ukianza, mvutano mkali unatarajiwa pia mkoani Shinyanga, ambako Mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM), anatarajia kupambana na Mwenyekiti wa CCM, Mkoa huo, Khamis Mgeja, ingawa hadi sasa hakuna aliyechukua fomu kuwania nafasi hiyo.

Baada ya Lembeli kutangaza hivi karibuni, kwamba atamng’oa madarakani Mgeja, baadhi ya viongozi wa chama hicho mkoani humo ambao pia ni wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM, Mkoa wa Shinyanga, wamemuonya mbunge huyo na kumtaka asiingilie uhuru wa wajumbe wa mkutano mkuu, kwa kuwa ndiyo wenye uwezo wa kuwang’oa viongozi wa ngazi ya mkoa.

Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti mjini hapa jana, wajumbe hao wamesema kitendo cha Lembeli kusema atamng’oa Mgeja hakiwezi kukubalika, kwa kuwa wajumbe wa mkutano mkuu ndiyo wenye uwezo wa kuwaondoa viongozi wao madarakani.

Mmoja wa wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho, Mkoa wa Shinyanga, Charles Shigino, alisema yeye na wenzake hawawezi kukaa kimya kwa kuwa kauli ya Lembeli inaonyesha anataka kuwachagulia kiongozi anayetakiwa kukiongoza chama hicho mkoani hapa.

“Kwa ujumla wajumbe wa mkutano mkuu hawakutegemea kusikia kauli hiyo kutoka kwa Lembeli, kwa sababu kauli hiyo inaingilia uhuru wa wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM mkoa wa Shinyanga.

“Suala la kupigiwa kura na kushindwa au kushinda siyo kazi ya mgombea, hiyo ni kazi ya wapiga kura ambao ni wajumbe, wala siyo Lembeli.

“Sasa sisi kama wajumbe, tunamuonya Lembeli aache tabia ya kujitangaza eti anakuja kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kumng’oa kigogo, hivi anataka kumng’oa kigogo huyo kwa umuhimu gani alionao?

“Haya majigambo hayana tija kwa sababu wapiga kura ndio wenye uamuzi na wenye mamlaka ya kumpa nafasi hiyo, sasa kwa kauli yake hiyo, ina maana Lembeli tayari ndiye Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Shinyanga.

“Lembeli ni Mwanachama wa CCM na ni Mbunge wa Kahama, kwa hiyo, ni vema kwanza ajue wazi kuwa hana uwezo wa kumng’oa kiongozi, kwani kazi hiyo ni ya wajumbe na wapiga kura tu na si vinginevyo, hivi ameshaongea na kila mjumbe na kumhakikishia kwamba atampa kura za kumng’oa kigogo huyo anayemtaja?

“Namuomba ndugu yangu Lembeli pamoja na wagombea wengine katika mkoa huu wa Shinyanga, waanze kuweka maji kichwani na kusubiri kunyolewa na wapiga kura ambao ni wajumbe na siyo Lembeli,” alisema Shingino.

Mbali na kiongozi huyo, mwingine aliyekerwa na kauli ya Lembeli ni Mwenyekiti wa CCM, Kata ya Shinyanga Mjini ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM mkoani hapa, Rajabu Makubuli, aliyesema Lembeli anahitaji msaada ili ajue namna mchakato wa uchaguzi unavyokwenda.

“Huyu jamaa ni mbunge, lakini inaonekana hajui taratibu za uchaguzi zinavyokwenda, kwa hiyo, nadhani kuna kila sababu ya kumweleza namna uchaguzi unavyofanyika, ingawa kwa kauli zale hizo wajumbe sasa wameshaanza kumjua tabia yake,” alisema Makubuli.

Naye Peter Lubinza ambaye pia ni Mjumbe wa CCM, Mkoa wa Shinyanga, alisema Lembeli alikosea kukaririwa na vyombo vya habari, akitamba kuwa atahakikisha anamng’oa Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Shinyanga.

“Kutokana na kauli yake anapaswa kutambua kuwa CCM na hasa wajumbe hivi sasa ni waelewa sana, wanajua kuchagua pumba na mchele” alisema.

“Yeye angekuja na hoja ya kujenga chama, hasa wakati huu ambao kinakabiliwa na changamoto nyingi za kisiasa, ikiwemo ya ushindani unaokikabili, badala yake anakuja na porojo zake kwamba anakuja kumng’oa kigogo, ngoja tumsubiri aje,” alisema Lubinza.

Chanzo: Mtanzania

38 WACHUANA UVCCM SINGIDA

 
Na Nathaniel Limu, Singida
JUMLA ya wanachama 38 wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) mkoani Singida, wamejitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa jumuiya hiyo, unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Katibu wa UVCCM Singida, Omary Mtua, aliwataja Dinya Shabani Hamisi, Hamisi Haji Nkuwei, Heri Shaaban Kundya, Labia Martin Zephania, Prince Antonio na Rehema Omari Sombi wanaogombea nafasi ya mwenyekiti wa UVCCM mkoa.

Alisema kwa upande wa nafasi ya mwenyekiti Singida mjini, nafasi hiyo imeombwa na Fikirini Hassan Salim, Yassin Mdima, Ibrahimu Alli na Shaaban Mhimbani.

Aidha, Mtua aliwataja Elia Sidadi, Shaaban Mangola, Madiu Ndwete na Yohana Mnyangili kuwa wameomba nafasi ya uenyekiti wilaya ya Singida vijijini.

“Kwa upande wa wilaya mpya ya Ikungi, nafasi ya mwenyekiti wa UVCCM imeombwa na Rebein Elisha Ibrahim (Anatetea nafasi yake), John Mughenyi, Joramu Ntandu, Yona Mwangu, Norman Mkola na Rajabu Njoha,” alisema katibu huyo.

Alisema nafasi ya mwenyekiti UVCCM wilaya ya Manyoni, imeombwa na Omari Miraji, Faraji Idd, Emmanuel Chitambi, Anjelo Madundoo na Jane Likuda.

Aidha aliwataja Belinda Matalu, Juliana Zingula, Mary Mkoma, Muungano Senyagwa na Athumani Rajabu ambao wameomba nafasi ya Mwenyekiti wa wilaya ya Iramba.

“Nafasi ya mwenyekiti UVCCM wilaya ya Mkalama, imeombwa na Hamidu Omari, Jofiliki Mkwega, Joseph Saeda, Kiula Solomon na Sebastian Gunda,” alisema Mtua.

Wakati huo huo, Mtua aliwataja Dinya Hamisi, Hansi Nkuwi, Prince Antonio na Sabasaba Manase ambao wameomba nafasi ya mjumbe wa NEC kupitia tiketi ya mkoa wa Singida kutoka UVCCM.

Alisema nafasi ya mjumbe wa baraza kuu taifa mkoa wa Singida, imeombwa na Heri Kundya, Dinya Hamisi, Joel Missanga, Jamila Kitila, Mazaba Warioba, Prince Antonio na Sabasaba Manase.
Chanzo: Mtanzania

SALAAM ZA EID MUBARAK KUTOKA SINGIDA YETU




WAISLAMU nchini leo watasherehekea Sikuuu ya Idd el- Fitri ambayo husheherekewa mara baada ya kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Tunapenda kuchukua fursa hii kuwatakia sikukuu njema Waislamu wote nchini na kuwaomba washerehekee kwa amani na utulivu kama vile walivyokuwa kwenye mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani ni miongoni mwa nguzo tano za Uislamu hivyo katika kipindi chote cha funga ya Ramadhani, mbali na kufunga mchana anatakiwa azidishe swala mbalimbali na kujiepusha kabisa na maovu.
Mwezi mtukufu wa Ramadhani una thamani na historia kubwa kwa Waislamu kwa sababu ndio mwezi kiliposhuka kitabu kitakatifu cha Kurani katika siku inayoitwa Lai latul Kadir usiku ambao ni bora kuliko miezi 1,000.
Si nia yetu kuanza kuzungumzia kwa undani faida za mwezi wa Ramadhani lakini katika kipindi chote cha mwezi huu tuliona idadi kubwa ya Waislamu wakivaa mavazi ya stara, kutenda matendo mema na kualikana kwenye futari.
Tusingependa Idd el- Fitri iwe mwanzo wa ajali, maasi, vifo na maovu mengi ambayo mara kwa mara tumekuwa tukiyashuhudia kwenye sikuu mbalimbali hapa nchini.
Kwa mujibu wa vitabu vya dini, Mwislamu yeyote akayetenda maovu siku ya leo ni sawa na kufanya dhambi mbele ya Mwenyezi Mungu siku ya kiama.
Tunaamini mafunzo waliyoyapata waumini wa Kiislamu kwenye mwezi mtukufu wa Ramadhani utawasaidia kuishi kulingana na maagizo ya Mwenyezi Mungu na kujiepusha na dhambi mbalimbali.
Tunachukua fursa hii kuwaomba madereva wote wa vyombo vya moto kuchukua tahadhari pamoja na kutoendesha kwa kasi wanapovitumia ili kuepusha ajali zinazozidi kuongezeka kila kukicha.
Wazazi na walezi wasiwaruhusu watoto wao kwenda matembezini, fukwe za bahari na kumbi za disko bila ya uangalizi maalumu.
Tunasema hivyo kwakuwa kila mara tumekuwa tukisikia watoto wakipata madhara kwenye kumbi za disko, kupotea, kuzama baharini na mikasa mbalimbali ambayo chanzo chake ni uangalizi mdogo wa wazazi au walezi.
Kwa wale wanaokwenda matembezini ni vema wakahakikisha majumbani mwao kunakuwa salama kwa kumuacha mtu atakayelinda au kuzifunga vizuri kwa lengo la kuzuia wezi.
Tunaamini kuwa Jeshi la Polisi litazidisha ulinzi katika maeneo mbalimbali ili kuwadhibiti wale wote waliolenga kufanya uhalifu kwenye sherehe za Idd el- Fitri.

EWURA CCC YAKABILIWA NA CHANGAMOTO


na Jumbe Ismailly, Singida
BARAZA la ushauri la watumiaji wa huduma zinazodhibitiwa na EWURA (EWURA CCC), limekiri kukabiliwa na changamoto zinazokwamisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Mwenyekiti wa baraza hilo, Mhandisi Profesa Jamidu Katima aliyasema hayo jana kwenye hafla fupi ya utambulisho na uzinduzi wa Kamati ya Mkoa wa Singida ya EWURA CCC iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa.
Alisema kamati hizo zinaundwa katika kipindi kinachokabiliwa na kero lukuki, hali ambayo kwa namna moja au nyingine zimekuwa zikikwamisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi wake.
“Kamati hizi zimeundwa katika kipindi ambacho kuna kero, malalamiko na changamoto nyingi zinazowakabili watumiaji wa huduma za nishati na maji,” alifafanua Katima.
Kwa mujibu wa Katima, changamoto hizo ni ukosefu wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi, bei kubwa ya huduma za umeme, petroli na gesi.
Hivyo aliweka wazi kwamba kutokana na uduni huo wa huduma, wananchi wamelazimika kuelimishwa kwa ufasaha ni kwanini bei zinapanda kwa kiwango hicho, hususani katika kipindi wanachokabiliwa na ugumu wa maisha, ikiwemo mfumuko wa bei.
Akizindua kamati hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Parseko Kone alilipongeza baraza hilo na hakusita kulikumbusha umuhimu wa kuzingatia sheria za nchi pamoja na mipaka ya majukumu yao.
Chanzo: Tanzania Daima

RC SINGIDA: WAELIMISHENI WANANCHI MATUMIZI BORA YA RASILIMALI


Na Emmanuel Michael, Singida

KAMATI za mikoa za baraza la ushauri la watumiaji wa huduma za nishati  na maji  nchini, zimetakiwa kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa matumizi bora ya raslimali hizo.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Parseko Kone wakati akizindua kamati hiyo.

Dk. Kone amesema licha ya kuwepo kwa changamoto ya uhaba wa nishati na maji na kupanda kwa bei zake, lakini baadhi ya watumiaji wa huduma hizo wamekuwa na matumizi mabaya.

Kutokana na hali  hiyo amesema  kuna  haja kwa kamati  za mikoa za ushauri wa baraza la watumiaji wa huduma za nishati na maji  kutoa elimu kwa wananchi  juu ya  kutunza na kutumia vyema raslimali hizo.


Amesema hatua hiyo itasaidia katika kuhakikisha kuwa nishati kidogo na maji yanayopatikana yanatumika kwa uangalifu ili kukidhi mahitaji na kupunguza malalamiko ya kupanda bei.

Kamati  hiyo yenye wajumbe sita imeundwa kwa mujibu wa sheria  ya  mamlaka ya udhibiti wa huduma za nishati na maji (EWURA) kifungu cha 30, ikiwa na  jukumu la kusimamia maslahi ya watumiaji wa huduma hizo na kushauriana na wenye viwanda na wadau wengine.

Blogzamikoa

MKUU WA WILAYA SINGIDA AKATAA KUINGILIA KESI YA MTUHUMIWA WA KUSAMBAZA VIPEPERUSHI VINAVYOHAMASISHA WAISLAMU KUTOSHIRIKI SENSA YA TAIFA.





Mkuu wa wilaya ya Singida Queen Mlozi (anayeangalia kamera) akiwa na viongozi wa dini ya kiislamu waliokwenda kumwomba asaidie kumnasua Issa Mohammed Msukuya dhidi ya kesi inayomkabili ya kugawa vipeperushi vya kuzuia waislamu kushiriki sensa.
Imam masjid Salafiy Singida mjini Abdurahman Hassan akiwa na wenzake ofisini kwa mkuu wa wilaya ya Singida. (Picha zote na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Jaribio la kutaka kumnasua Issa Mohammed Msukuya (46)  kwenye kesi inayomkabili ya kumiliki na kusambaza vipeperushi vinavyohamasisha waislamu kutoshiriki sensa ya taifa ya mwaka huu limegonga mwamba.
Jaribio hilo limegonga mwamba baada ya mkuu wa wilaya ya Singida Queen Mlozi kudai kwamba hataingilia suala ambalo tayari lipo mahakamani.
Awali Imam Masjid Salafiy Singida mjini Abdurahman Hassan, akiwa amefuatana na viongozi wenzake watatu, walifika ofisini kwa Mkuu wa Wilaya kumwomba aingilie kati suala la Issa, ili mahakama ya hakimu mkazi iweze kumwachia huru.
Imam Hassan alisema Issa  anapaswa kuachiwa huru kwa vile yeye si muasisi wa uandaaji wala  mchapishaji wa vipeperushi hivyo vinavyopinga zoezi la sensa.
Hata hivyo Mkuu wa Wilaya Mlozi aliwaomba viongozi hao wa dhehebu la kiislamau wawe  wavumilivu na kuiachia mahakama ifanye kazi yake bila kuingiliwa na upande wo  wote.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wapunguze munkhari, ili waweze kushiriki kujenga nchi katika misingi ya amani na utulivu.
Issa amefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi na kusomewa shitaka la kugawa vipeperushi vinavyowahamasisha waislamu kutokushiriki zoezi la sensa.
Mwendesha mashitaka ambaye ni mwanasheria wa serikali Geofrey Luhanga, alidai mbele ya hakimu Chiganga Tengwa kuwa mnamoAgosti saba mwaka huu huko katika viwanja vya shule ya sekondari ya kata ya Sepuka, mshitakiwa Issa alikamatwa akiwa na vipeperushi hivyo huku akijua wazi kuwa kitendo hicho ni kinyume na sheria.
Luhanga alisema kuwa mshitakiwa Issa ametenda kosa kwa mujibu wa kifungu 390 na 35 cha kanuni za adhabu sura 16 ujazo wa kwanza iliyofaniwa marejeo mwaka 2009.
Mshitakiwa amekana kosa hilo na yupo nje kwa dhamana ya watu wawili waliotoa ahadi ya shilingi milioni mbili kila moja.
Kesi hiyo sasa itatajwa tena Agosti 26 mwaka huu.

WAFUNGWA WAGOMA KUVAA SARE JELA


na Jumbe Ismailly, Singida
WAFUNGWA watano waliohukumiwa kuanza kutumikia adhabu ya kifungo cha jumla ya miaka 62 jela baada ya kupatikana na hatia ya kosa la unyang’anyi wa kutumia nguvu, wamegoma kuvaa sare za wafungwa baada ya kufikishwa gerezani.
Wamesema kuwa hawavaa sare mpaka hapo majibu yao ya rufaa yatakaporudi.
Taarifa za kuaminika zilizopatikana kutoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Singida na kuthibitishwa na Mkuu wa Gereza la Wilaya ya Singida, T. Mbuta zimeeleza kuwa wafungwa hao walitoa tamko hilo mara tu baada ya hukumu ya kesi yao kutolewa na Hakimu wa Mahakama hiyo, Flora Ndale wakati wakisindikizwa na askari kupelekwa gerezani kuanza kutumikia adhabu hiyo, Agosti 10, mwaka huu.
Wafungwa hao walioitisha mgomo wa kuvaa sare gerezani ni Abdallah Masoud, Hassan Jumanne, Rashidi Mwela, Jumanne Mjoi na Seif Ismaili Ngura.
Alipotakiwa kuzungumzia suala hilo, mkuu wa gereza la Wilaya ya Singida, Mbuta licha ya kukiri kuwepo, alisema kitendo hicho kilifanyika kutokana na wafungwa hao kutofahamu haki zao wanazotakiwa kudai.
Alisema baada ya wafungwa hao kufikishwa gerezani hapo, waliwaelimisha nini cha kufanya ili waweze kutimiza matakwa yao ya kisheria na wakakubali kuvaa sare.
“Kwa kweli tukio hilo lilikuwepo kwanza tu walipofikishwa wafungwa hao gerezani… madai yao ni kweli yana msingi kabisa, lakini tuliwaambia ili waweze kufanikiwa kwanza ni lazima wakubali kuvaa sare ili waweze kutambuliwa kuwa ni wafungwa,” alisema Mbuta.
Chanzo: Tanzania Daima

WALIMU SINGIDA WATISHIA KUKWAMISHA ZOEZI LA SENSA

Fredrick Ndahan, Singida Yetu
Baadhi ya walimu wa shule za sekondari na msingi katika Manispaa ya Singida wametishia kutoshiriki katika kutoa taarifa katika zoezi la sensa baada ya kutolewa katika orodha ya makalani na makalani wandamizi wakati wa zoezi hilo.
Wakiongea na mwandishi wa habari hizi katika maeneo tofauti tofauti wamesema hakuna haja ya kushiriki katika zoezi hilo kwani walioteuliwa hawana vigezo kama ilivyoanishwa katika tangazo la nafasi za kazi lilotolewa.
Walimu hao wamesema kuwa kunamawakala hawajamaliza elimu ya sekondari jambo ambalo linaweza kukwamisha zoezi hilo kwa kusimamiwa na watu wasio na sifa stahiki.
Akizungumza kwa masharti ya kutotajwa jina lake huku akionesha mitihani aliyofaulu baada ya zoezi la semina amesema nashangaa kuona jina lake na baadhi ya walimu wenzake licha kuchaguliwa kushiriki katika zoezi la sensa kama wakufunzi lakini wamewekwa maofisa wengine ambao hawakushiriki mafunzo ya awali ya zoezi la sensa.
Mbali na tatizo hilo pia kuna makalani wengine wamepangiwa kufanya shughuli hiyo katika maeneo ambayo si makazi yao kinyume cha utaratibu.
Manispaa ya Singida jana ilianza semina ya makalani wandamizi katika ukumbi wa chuo cha maendeleo singida (FDS).
Blogzamikoa

DIANA CHILOLO AOMBA UENYEKITI WA CWT

Na Nathaniel Limu, Singida

JUMLA ya wanachama wanne wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) mkoani Singida akiwamo Diana Chilolo, wameomba nafasi ya uenyekiti ngazi ya mkoa kupitia jumuiya hiyo.

Chilolo ambaye ni mbunge wa Viti Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, anatetea nafasi yake ya mwenyekiti wa UWT.

Wengine wanaoomba nafasi hiyo ni Esta Masinga, Sundi Samike na Pendo Kone.

Akizungumza mjini hapa jana, Katibu wa UWT Mkoa wa Singida, Sija Lukwale, alisema nafasi ya uenyekiti kwa upande wa Manyoni imeombwa na Elizabeth Bajile, Neema Mwitizi na Mwanahawa Yusufu.

“Waliomba nafasi hiyo ya Mwenyekiti UWT Singida Vijijini ni Christina Jambi, Hadija Kissuda, Salma Kundya, Neema Ipande na Amina Ititi. Wilaya mpya ya Ikungi walioomba ni Theresia Nkuwi, Christina Hamisi na Helena Ayubu,” alisema Sija.

Aliwataja Jenifa Miana, Hawa Athumani na Neema Imari kuwa wameomba nafasi ya uenyekiti wa UWT Wilaya ya Iramba wakati nafasi hiyo katika Wilaya mpya ya Mkalama, imeombwa na Elipendo Machafuko, Mariam Kahola na Magreth Kinota.

“Katika nafasi hii ya uenyekiti wa UWT wilaya na mkoa, wagombea watachujwa na vikao husika kwa ajili ya kubaki na wagombea watatu tu,” alisema.

Alisema uchaguzi wa nafasi hizo utafanyika mara uchujaji wagombea utakapomalizika.

Aidha, alisema nafasi ya mjumbe wa Baraza Kuu Taifa CCM kutoka Singida, imeombwa na Theresia Nkuwi, Fatma Toufiq, Duda Mughenyi na Hadija Majii.

Alisema nafasi ya mjumbe wa Mkutano Mkuu CCM Taifa imeombwa na Sarah Mkumbo, Mwajuma Shaha na Hadija Majii.
Chanzo: Mtanzania

WAZIRI NYARANDU KUCHMBA KISIMA SINGIDA

Na Emmanuel Michael, Singida
WAKAZI wa kijiji cha Mnung’una jimbo la Singida kaskazini  pamoja na maeneo jirani hivi karibuni  wanatarajia kuondokana na tatizo la ukosefu wa maji safi na salama lililokuwa linawakabili kwa miaka mingi.

Matumaini ya kumalizika kwa tatizo  hilo yamekuja baada ya mbunge wa jimbo hilo Mhe Lazaro Nyalandu  kufadhili uchimbaji wa kisima kirefu kwa gharama ya shilingi milioni 25 katika eneo hilo.
Mbunge Nyalandu amesema kukamilika kwa kisima hicho kilichoanza kuchimbwa jana kutaondoa adha kwa wananchi kutembea umbali mrefu na kupoteza muda wa kufanya shughuli za maendeleo kwa kutafuta maji.
Amesema kisima hicho kinachotarajiwa kuwa na uwezo wa kuzalisha lita 10,000 za maji  kwa saa moja ni sehemu ya  utekelezaji kwa  vitendo  sera ya taifa  ya maji inayotaka huduma hiyo kupatikana  umbali usiozidi mita 400 kutoka makazi ya watu.
Baada ya kukamilika kwa uchimbaji wa kisima  hicho, mradi huo unatarajia kuwanufaisha zaidi ya wananchi elfu saba kwa kujipatia  huduma maji  safi na salam kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, kunywesha mifugo yao na  kuendesha  kilimo cha bustani.

SERIKALI KUTOA FIDIA YA NG’OMBE WALIOUAWA

Na Nathaniel Limu, Singida

SERIKALI imeahidi kutoa Sh milioni sita ikiwa ni fidia ya ng’ombe 22, wanaodaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na askari wa Pori la Akiba la Maswa lililopo Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu.

Inadaiwa ng’ombe hao walipigwa risasi na kuuawa Desemba, 2009 baada ya kuingizwa ndani ya hifadhi hiyo kinyume cha sheria zinazolinda hifadhi za wanyama pori.

Ahadi hiyo imetolewa mjini hapa juzi na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na wakazi wa Kata ya Sakasaka jimboni Kisesa.

Alisema lengo la uamuzi huo ni kuimarisha uhusiano mzuri zaidi kati ya askari wa wanyama pori na wakazi wa vijiji vinavyozunguka pori hilo.

“Pia ni sehemu ya mikakati inayochukuliwa na Serikali ya kuhakikisha mgogoro wa muda mrefu kati ya uongozi wa Pori la Akiba Maswa, wananchi wa vijiji vinavyozunguka pori hilo unamalizika na kurejesha amani na utulivu katika eneo hilo,” alisema Nyalandu.

Aidha, alisema Serikali inatarajia kuunda kamati huru itakayotafuta ufumbuzi wa mgogoro huo wa muda mrefu.

“Katika kamati hii, kutakuwepo na mwakilishi mmoja kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na wajumbe wengine watakuwa ni watu huru watakaozitendea haki pande zote mbili.

Alisema kamati hiyo itatoa taarifa yake wizarani mapema kabla ya vikao vya Bunge vinavyoendelea mjini Dodoma kumalizika.

“Napenda kukumbusha kuwa ni marufuku kuchungia, kulima, kuingiza au kufanya shughuli zozote za kijamii ndani ya hifadhi ya wanyama pori, mfugaji au mtu yeyote atakayevunja sheria halali zilizopo atachukuliwa hatua kali za kisheria,” alisema Nyalandu.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Rosemary Kirigini, alisema Hifadhi ya Pori la akiba Maswa ipo kwa mujibu wa sheria.
Chanzo: Mtanzania

BEI YA VYAKULA VYA FUTARI YAPANDA MARA MBILI SINGIDA


Fredrick Ndahani
BEI ya vyakula katika Manispaa ya Singida imepanda mara dufu katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani ambapo bei ya maboga imepanda toka sh.500 hadi kufikia kati ya sh.1,000 na 2,000 kwa boga moja.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kupanda kwa bei ya viazi, maboga, na bidhaa nyingine ambazo na kuwakazwa wakazi wa mjini hapa.
Mmoja wa wauzaji wa bidhaa hizo katika soko la Marunda na Mboga mboga Deus Mwijage alisema kuwa wamelazimika kupandisha bei ya maboga kutoka na kukosekana kwa mihogo ambayo ilikuwa inasaidia wakati wa mwezi wa ramadhani.
Blogzamikoa

MGOMO WA WALIMU WAENDELEA SINGIDA


Fredrick Ndahani, Singida
Mgomo wa Walimu umezidi kuchukua kasi Mkoani Singida ambapo asilimia kubwa ya walimu katika Manispaa ya Singida, wameitikia mgomo huo licha ya serikali mkoani humo kutishia kuwafukuza kazi walimu waliogoma.
Mgomo huo umeendela katika shule za msingi kumi na moja ikiwamo shule ya msingi Ukombozi, Kibaoni, Mahembe, Ipembe, Sumaye, Singidani, Mughanga, Sabasaba, Utemini  Minga na Nyerere ambapo walimu wakuu ndio wameonekana kufika shuleni.
Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Ukombozi Samwel Kingu amesema wamelazimika kufika shuleni hapo kulinda mali za shule kwa kuwa wanahofia kuwepo kwa uharibifu wa mali hizo.
Naye Katibu wa CWT wa Mkoa Aran Jumbe amesisitiza walimu wote kuendelea kukaa majumbani mpaka tamko rasmi kutoka kwa Rais wa Chama hicho la kuendelea na kazi litakapotolewa.
Blogzamikoa

MWENYEKITI WA KITONGOJI AFUNGWA KWA WIZI


na Jumbe Ismailly, Singida
MWENYEKITI wa Kitongoji cha Miyombwe, Kijiji cha Mkinya, wilaya mpya ya Ikungi amehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa sh 100,000 iliyokuwa itumike kugharamia ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Dungunyi, wilayani hapa.
Mwenyekiti huyo, Michael Khaliki (53) amehukumiwa kifungo hicho na Hakimu Terisophia Tesha wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Tesha alisema ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka umethibitisha bila kuacha shaka kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo aliloshitakiwa nalo.
Alisema kutokana na kosa hilo, anampa adhabu ya kulipa faini ya sh 300,000 na akishindwa atumikie kifungo cha miaka miwili jela.
Hata hivyo, mshitakiwa huyo alishindwa kulipa faini hiyo, hivyo kulazimika kwenda kuanza kutumikia kifungo hicho.
Awali, Mwanasheria wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida, Antidius Rutayuga, aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshitakiwa, ili iwe fundisho kwake na watu wengine wenye tabia kama hiyo.
Kwa upande wake, mshitakiwa Michael aliiomba mahakama imhurumie kwa kuwa ni kosa lake la kwanza na pia ana familia kubwa inayomtegemea.
Katika kesi hiyo, ilidaiwa kuwa Septemba 16 mwaka 2008 katika Kijiji cha Mkinya, mshitakiwa alitumia sh 100,000 kwa matumizi yake binafsi iliyokuwa itumike katika ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Dungunyi.
Chanzo: Tanzania Daima

MWENYEKITI WA KITONGOJI AFUNGWA KWA WIZI


na Jumbe Ismailly, Singida
MWENYEKITI wa Kitongoji cha Miyombwe, Kijiji cha Mkinya, wilaya mpya ya Ikungi amehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa sh 100,000 iliyokuwa itumike kugharamia ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Dungunyi, wilayani hapa.
Mwenyekiti huyo, Michael Khaliki (53) amehukumiwa kifungo hicho na Hakimu Terisophia Tesha wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Tesha alisema ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka umethibitisha bila kuacha shaka kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo aliloshitakiwa nalo.
Alisema kutokana na kosa hilo, anampa adhabu ya kulipa faini ya sh 300,000 na akishindwa atumikie kifungo cha miaka miwili jela.
Hata hivyo, mshitakiwa huyo alishindwa kulipa faini hiyo, hivyo kulazimika kwenda kuanza kutumikia kifungo hicho.
Awali, Mwanasheria wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida, Antidius Rutayuga, aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshitakiwa, ili iwe fundisho kwake na watu wengine wenye tabia kama hiyo.
Kwa upande wake, mshitakiwa Michael aliiomba mahakama imhurumie kwa kuwa ni kosa lake la kwanza na pia ana familia kubwa inayomtegemea.
Katika kesi hiyo, ilidaiwa kuwa Septemba 16 mwaka 2008 katika Kijiji cha Mkinya, mshitakiwa alitumia sh 100,000 kwa matumizi yake binafsi iliyokuwa itumike katika ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Dungunyi.
Chanzo: Tanzania Daima

CCM Singida yabariki agizo la RC Kone



Na Nathaniel Limu
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Singida, kimebariki amri halali iliyotolewa na mkuu wa mkoa wa Singida, Dk. Parseko Kone, ya kupiga marufuku wafanyabiashara binafsi kununua alizeti moja kwa moja kutoka kwa mkulima.

Baraka hizo zimetolewa na chama hicho katika kikao chake cha halmashauri kuu kilichofanyika Julai 5, mwaka huu mjini hapa.

Kwa mujibu wa tamko la chama hicho lililotolewa na CCM mkoa wa Singida, limeeleza kuwa pamoja na mambo mengine, limebaini kuwa amri hiyo ni halali, haikueleweka vizuri kwa wananchi.

Mbali na hatua hiyo CCM, imeagiza elimu ya kutosha kuhusu amri hiyo, itolewe ili lengo la amri hiyo liweze kutekelezwa kwa makini.

Taarifa hiyo ya CCM imeeleza kuwa, amri iliyotolewa na Mkuu wa mkoa wa Singida Dk. Parseko Kone, haikukataza mtu au kikundi chochote kununua zao la alizeti, isipokuwa imeelekeza kwamba ni vyama vya msingi vya ushirika ndivyo vitakavyonunua moja kwa moja zao hilo kutoka kwa wakulima na kisha kuwauzia wafanyabiashara binafsi.

Awali agizo hilo la Mkuu wa mkoa liliagiza kwamba mbali na vyama vya ushirika kuwepo, yaanzishwe magulio katika maeneo mbalimbali ambayo wakulima wa alizeti watauza kwa watu mbalimbali, kwa kufuata bei elekezi kama njia ya kuwanufaisha moja kwa moja kuliko ilivyokuwa awali.

“Wenye viwanda vya kukamua mafuta, wanaruhusiwa kuanzisha ushirika wao wa kununua alizeti, ili mradi wafuate bei elekezi,” ilieleza taarifa hiyo ya CCM katika tamko lao

Akifafanua zaidi, Dk. Kone, alisema hivi sasa ameteua kamati ambayo itajikita katika kuhakiki uwepo na uwajibikaji wa vyama vya msingi vya ushirika.

“Pia tutachunguza uwajibikaji wa viongozi wa vyama hivyo kuanzia ngazi ya mrajisi wa vyama vya msingi vya ushirika juu ya uadilifu na utendaji kazi wao. Wale ambao wataonekana kuwa kikwazo katika maendeleo ya wakulima wa alizeti, tutawashughulikia mara moja,” alisema RC Kone
Chanzo: Mtanzania

Tamko La CHADEMA Juu Yaliyojiri Singida



CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Tamko Kuhusu Yaliyojiri Katika Mkutano wa Hadhara wa CHADEMA Uliofanyika Kata ya Ndago Siku ya Jumamosi Tarehe 14 Julai 2012

1. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kiliandaa mikutano ya hadhara katika Jimbo la Iramba Magharibi. Mikutano hiyo ilitolewa taarifa polisi na jeshi hilo lilitoa baraka zake kama utaratibu wa sheria unavyotaka kwa barua yake ya tarehe 12 Julai 2012 Kumb. Na. KIO/B1/1/VOL.V/268

2. Mkutano wa kwanza ulipangwa kufanyika katika Kata ya Ndago katika viwanja vilivyo karibu na kituo cha mabasi ambapo pia ni hatua chache karibu kabisa na Kituo cha Polisi Ndago. Mkutano huu ulipangwa kuanza saa nane mchana.

3. Msafara wa kitaifa unaofanya ziara ya ukaguzi wa chama, katika mkoa wa Singida chini ya uratibu wa Ofisa wa Sera na Utafiti Makao Makuu, Mwita Mwikwambe Waitara, (ikiwa ni maandalizi ya operesheni nyingine kubwa mkoani humo itakayofanyika baadae), uliwasili katika eneo la Mkutano majira ya saa tisa na nusu alasiri. Tulikuta wananchi wengi wakiwa wanatusubiri. Kabla ya Mkutano kuanza tulipewa taarifa kwamba kuna kikundi cha vijana kimeandaliwa kuvuruga mkutano wa CHADEMA kwa kufanya fujo, ikiwemo kurusha mawe ili mkutano huo usifanyike. Suala hilo lilielezwa mkutanoni mapema na Mheshimiwa Waitara, mbele ya askari polisi.

4. Wakati tukijiandaa kuanza hotuba, vijana wapatao wanane walianza chokochoko kwa kutoa matusi na punde mawe yakaanza kurushwa kutoka sehemu mbalimbali. Wakati fujo zinaanzishwa na kile kikundi, Mheshimiwa Waitara alikuwa bado anazungumza na wananchi kuwaandaa kusikiliza wazungumzaji wengine. Vurumai hiyo ilizimwa na wananchi wenyewe wa Ndago waliokuwa na hamu ya kusikiliza ujumbe wa viongozi wa kitaifa wa CHADEMA.

5. Kwa kweli tunawashukuru wananchi wengi wa Ndago walioonesha ujasiri mkubwa kuweza kuwaondoa vijana wale eneo la mkutano, kisha mkutano ukaendelea, huku wananchi wakionesha kila hamasa ya kufurahia hoja kutoka kwa wazungumzaji, akiwemo Mheshimiwa John Mnyika, ambaye aliombwa ahudhurie ziara hiyo kwa nafasi yake ya Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA.

6. Mpaka tunamaliza mkutano huo ambao wananchi waliufurahia sana kwa namna ulivyohutubiwa kwa amani na utulivu huku wazungumzaji wakijenga hoja juu ya mstakabali wa jimbo na taifa lao kwa ujumla, mamia ya wananchi waliohudhuria walitaka tuendelea kuhutubia, lakini tulibanwa na ratiba ya kuwahi mkutano wa pili, eneo la Kinampanda

7. Lakini kutokana na vurugu hizo zilizokuwa zikisababishwa na kikundi cha vijana ambao tayari ilishatolewa taarifa yao kwenye mkutano huo, lakini askari waliokuwepo hawakuthubutu kuchukua hatua, tulilazimika kuomba msaada kutoka kwa OCD na R.P.C, ambapo baadae wakati mkutano unakaribia kuisha tuliona gari la polisi kutoka Mjini Singida likiwa na askari waliojipanga rasmi kwa ajili ya kuzuia vurugu likifika pale eneo la mkutano, lakini wakati huo hali ilishatulia na hotuba zimetolewa vizuri.

8. Kutokana na hali hiyo ya vurugu, zilitolewa taarifa Kituo cha Polisi cha Ndago, ambapo lilifunguliwa jalada NDG/RB/190/2012. Katika jalada hilo tulitaja baadhi ya majina ya watu waliokuwa vinara wa kundi lililokuwa likifanya fujo kwenye mkutano mbele ya askari polisi. Majina hayo ni; 1. Daniel Sima, 2. Tito Nitwa, 3. Bakili Ayubu, 4. Yohana Makala Mpande, 5. Ernest Kadege, 6. Abel John, 7. Athuman Ntimbu, 8. Martin Manase, 9. James Ernest, 10. Simion Makacha, 11. Anton John, 12. Frank Yesaya

9. Kwa hakika askari polisi wa Ndago waliokuwepo mkutanoni mbali ya kutochukua hatua yoyote dhidi ya fujo tulizofanyiwa ikiwemo kupondwa mawe na kikundi kidogo cha wahuni, fujo zilipozidi askari wote walikimbia eneo la mkutano, akabaki OCS pekee ambaye naye alionekana dhahiri kutotaka kuchukua hatua stahili. Hakuonekana kufanya juhudi zozote za kuhakikisha amani inalindwa na ulinzi unaimarishwa katika eneo la mkutano na hatua zinachukuliwa dhidi ya watu walioonekana kudhamiria kufanya fujo. Mtu yeyote makini angeweza kuona kuwa askari wale waliokuwepo pale mkutanoni ‘almuradi’ tu lakini kama vile walikuwa na maelekezo maalum ya kuhakikisha hawachukui hatua yoyote katika kuzuia mpango wowote wa kusababisha vurugu na kuvunja amani.

10. Baada ya kumaliza mkutano wa Ndago kwa amani, tulikwenda Kinampanda ambako tulifanya mkutano mwingine mzuri kwa amani kabisa, ambapo mbali ya wananchi kuwa wametusubiri kwa hamu kubwa na kutusikiliza kwa makini hoja zetu, polisi katika eneo hilo walitupatia ushirikiano mzuri tangu wakati tunafika mpaka tulipomaliza mkutano huo.

11. Jioni wakati tumerudi hotelini, tukasikia kuna taarifa zinasambazaa kuwa kuna mtu/watu wamekufa katika eneo la Ndago. Habari hizo zilikuwa zinakanganya kwa sababu zilikuwa zikitaja idadi tofauti tofauti. Lakini kwa vyovyote vile kama ni kweli kuna tukio la mtu kufariki, CHADEMA tunasikitika sana kwa tukio hilo la uhai wa mtu.

12. Tunalaani taarifa zinazozidi kusambazwa ambazo zinawataja polisi kuwa wanatuhusisha CHADEMA na tukio la mtu aliyefariki. Hii ni ajabu kubwa kwamba tumetoka kwenye mkutano ule kwa amani kabisa mpaka tumemaliza mkutano wa pili kwa amani na polisi wakiwepo sehemu zote mbili, kisha tunasingiziwa masuala ambayo wenyewe hatukuwa na habari nayo tangu mkutano wa kwanza ukiwa unaendelea mpaka mkutano wa mwisho ulipomalizika.

13. Kutokana na habari hiyo ya kifo cha mtu inavyoenezwa kwa kuihusisha CHADEMA, tumebaini kuwepo kwa mbinu na mikakati ya chama tawala pia vyombo vya dola vikihusika kutaka kuwatisha wananchi wa Singida, Watanzania wote wapenda mabadiliko na viongozi wa CHADEMA katika mkoa huu, wasifanye kazi ya kisiasa kwa kuwabambikizia tuhuma na kesi na pia kuwafanya waonekane ni watu wa vurugu.

14. Tunapenda kusema hapa kuwa njama hizo hazitafanikiwa. Zitashindwa kama zilivyoshindwa njama zingine zote ambazo zimekuwa zikifanywa na vyombo vya dola, viongozi wa serikali na chama tawala dhidi ya CHADEMA na vuguvugu la mabadiliko nchini.

15. Tunawataarifu wananchi kuwa ratiba ya kufanya Operesheni nyingine kubwa katika Mkoa wa Singida, ikiongozwa na Katibu Mkuu, Dkt. Willibrod Slaa, itafanyika baadae kama ilivyoazimiwa na kikao cha Kamati Kuu.


Imetolewa leo Singida, Julai 15, 2012 na;

Waitara Mwita Mwikwabe

Afisa wa Sera na Utafiti CHADEMA Makao Makuu

ZIARA YA VIONGOZI WA CHADEMA MKOANI SINGIDA.


Afisa wa sera na utafiti CHADEMA Makao makuu,Waitara Mwita Mwikwabe,akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Ndago jimbo la Iramba Magharibi.
Mh. John Mnyika (katikati) na baadhi ya Viongozi wa CHADEMA.
Mshauri wa CHADEMA na mhadhiri wa chuo kikuu cha Dar-es-salaam Dk.Kitila Mkumbo akisalimia wakazi wa kijiji cha Ndago jimbo la Iramba Magharibi.
Mbunge wa jimbo la Ubungo jijini Dar-es-salaam John Mnyika akihutubia wakazi wa kijiji cha Ndago jimbo la Iramba Magharibi.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Ndago jimbo la Iramba Magharibi,wakiitikia salamu ya CHADEMA ya ‘nguvu ya umma’.
Baadhi ya askari wa FFU walioitwa kutuliza vurugu kwenye mkutano wa hadhara ulioitishwa katika kijiji cha Ndago kwa ajili ya viongozi wa CHADEMA kuzungumza nao.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Ndago waliohudhuria mkutano wa hadhara ulioitishwa kwa ajili ya viongozi wa CHADEMA kuzungumza nao.
(Picha zote na Nathaniel Limu).
Kwa Hisani ya Mo Blog

Singida wadhibiti kideri


na Hillary Shoo, Singida
SERIKALI imefanikiwa kudhibiti ugonjwa hatari wa mdondo, maarufu kama ‘kideri’ mkoani hapa, unaoua kwa wingi kuku wa kienyeji, katika halmashauri ya wilaya Singida.
Hayo yalibainishwa juzi na Mkurugenzi wa Maabara Kuu ya Taifa ya jijini Dar es Salaam, Dk. Sachindra Das, wakati akitoa taarifa ya ugonjwa huo, kwenye ukumbi wa chuo cha maendeleo mjini hapa.
Dk. Das alisema kuwa hali hiyo imeifanya halmashauri hiyo na Tanzania kwa ujumla kuongoza katika kudhibiti ugonjwa huo kati ya nchi nne za Afrika, zilizoshiriki kampeni hiyo ya chanjo.
Mkurugenzi huyo, alizitaja nchi zingine zilizoshiriki kampeni hiyo iliyodumu kwa miaka mitatu na kutarajiwa kumalizika Desemba mwaka huu, kuwa ni Zambia, Malawi na Msumbiji.
Alisema kampeni hiyo ilisimamiwa na kamati ya uratibu, mradi wa kitaifa udhibiti wa ugonjwa wa mdondo, kupitia Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, kwa kushirikiana na nchi ya Australia.
Aidha, mmoja wa wafugaji wa kuku wa kienyeji katika wilaya hiyo, Madai Njau, alisema kuwa kabla ya chanjo hiyo kuanza kutolewa, alikuwa akipoteza kuku wengi kutokana na kufa kwa ugonjwa huo.
Njau alifafanua kuwa baada ya kuzingatia sharti la chanjo, hivi sasa ananufaika kwa kiwango kikubwa na kuku wa kienyeji, ambao huuza mayai na kuku kwa wafanyabiashara wa jumla
Chanzo: Tanzania Daima

Kamati yaagiza waachimbaji, mwekezaji kutafuta suluhu


Gasper Andrew,
Singida 
KAMATI ya Ulinzi  na Usalama  ya Wilaya ya Iramba, mkoani Singida, imewataka wachimbaji wadogo wa dhahabu katika eneo la Sekenke wilaya humo,  kufikia mwafaka baina yao na mwekezaji mwenye leseni, vinginevyo sheria ichukue mkondo wake.

Kaimu Mwenyekiti wa  kamati hiyo,  Edward Ole Lenga, alisema agizo hilo linafuatia kushindikana kwa jitihada za kuzisuluhisisha pande hizo kwa njia ya mazungumzo.

 Ole Lenga alisema kushindikana kwa jitihada hizo kumetokana na kitendo cha wachimbaji wadogo, kugoma kusaini makubaliano  kati yao na mwekezaji  John Bina, ambaye amekubali kuingia ubia na  wachimbaji hao katika eneo la leseni yake.

 Ole Lenga ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Singida alisema hatua hiyo imeilazimisha kamati hiyo kuwataka wachimbaji hao, kufikia makubaliano nje ya mazungumzo rasmi.

Alisema vingine, Serikali itachukua hatua za kisheria  kwa mujibu wa taratibu, kanuni na sheria za madini nchini.


Kauli hiyo inakuja wakati Kamishina Msaidizi wa Madini  katika Kanda ya Kati,  Manase  Mbasha, akiwa amesema  wachimbaji hao wakiendesha  shughuli zao kinyume cha sheria na kwamba wanapaswa kushtakiwa.

Wachimbaji wadogo katika eneo la Sekenke, amegoma kuondoka katika eneo  hilo wala kuingia ubia na mwenye leseni,kwa madai kuwa leseni  yake inataja eneo la Mgongo na si Sekenke.
Chanzo: Mwananchi




 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa