DIWANI wa Rungwa, Tarafa ya Itigi, wilayani Manyoni, Singida,
Edward Machapaa, amependekeza adhabu ya kuchapwa viboko itolewe kwa
watendaji wanaokula fedha za wananchi zilizotolewa na serikali kwa
ajili ya kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo.
Machapaa alitoa pendekezo hilo kwenye mkutano maalumu wa Baraza la
Madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo uliofanyika mjini Manyoni
alipokuwa akijadili hoja ya matumizi mabaya ya fedha za miradi ya
maendeleo.
Alisema kumekuwepo malalamiko mengi na ya mara kwa mara juu ya fedha
za miradi kutumika vibaya au hata kwa baadhi ya watendaji kula fedha
hizo, hivyo umefika wakati wa kubadili mbinu ya kutoa adhabu kwa kutoa
adhabu ya viboko.
“Ndugu mkurugenzi, kwa hili hapa inatakiwa tutafute dawa, huyu mtu
anayekula hela kama ni mtendaji kwanini asichapwe bakora 12, ili
akamuonyeshe mkewe?” alisisitiza Machapaa na kusababisha madiwani
wenzake pamoja na wakuu wa idara kuangua kicheko.
Diwani huyo alitumia fursa hiyo kuwashawishi madiwani wenzake
kubadilika na kuonya kwamba endapo hawatabadilika serikali itaendelea
kutuma wakaguzi na adhabu ya kuwakata mishahara itaendelea kuwepo mwaka
hadi mwaka.
Pia alipendekeza watendaji hao wafukuzwe hata watatu kwa kuanzia na huenda wengine wakaogopa baada kuona adhabu hiyo.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Supeet Mseya, alisema katika
kipindi cha mwaka 2013/2014 halmashauri hiyo ilipata mafanikio mengi
na kuyataja baadhi kuwa ni kuendelea kupata hati safi ya ukaguzi wa
matumizi ya fedha na halmashauri kuendelea kupata ruzuku ya CDG.
Mafanikio mengine ni kuboreshwa kwa huduma za afya kwa asilimia 95
kwa kutoa kinga na tiba kwa ajili ya magonjwa mbalimbali, uendelezaji
wa ujenzi wa vituo vitatu vya afya katika kata za Makuru, Mitundu na
Itigi, ujenzi wa zahanati tatu katika vijiji vya Ntope, Igwamadete
Rungwa, na ukamilishaji wa hosteli nne katika shule za Itigi, Makuru,
Rungwa na Sanza.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment