HALMASHAURI ya Manispaa ya Singida, inatarajia kutumia sh bilioni 31.7 katika bajeti yake ya mwaka wa fedha wa 2014/2015.
Kaimu Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Deus Luziga, alibainsha hayo
alipokuwa akitoa mapendekezo ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha mbele ya
kikao maalumu cha bajeti cha Baraza la Madiwani kilichofanyika kwenye
ukumbi wa mikutano wa manispaa hiyo.
Alisema kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015 Halmashauri ya Manispaa ya
Singida imeandaa bajeti yake kwa kuzingatia mwongozo wa bajeti wa
taifa, sera ya taifa ya kuondoa umasikini.
Alisema kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 15.287 ni mishahara ya
watumishi, ruzuku ya serikali kuu kwa matumizi mengineyo sh bilioni
1.860, sh bilioni 11.621 ni ruzuku ya miradi ya maendeleo wakati sh
bilioni 2.986 ni mapato ya ndani.
Alisema wanatarajia serikali kuu itawapatia ruzuku ya sh milioni 181 kwa ajili ya kufidia ushuru na kodi iliyofutwa.
Kaimu mkurugenzi huyo alisema bajeti ya Manispaa ya Singida
imeongezeka kwa sh bilioni 13 ambayo ni sawa na aslimia 43 ya lengo la
kukusanya zaidi ya sh bilioni 18.1 katika bajeti ya mwaka wa fedha wa
2013/2014.
“Ongezeko hili limechangiwa pamoja na kuongezeka kwa ajira mpya na
nyongeza za mishahara na kuongezeka kwa miradi ya maji ambayo maelekezo
yake ni kutekeleza miradi katika vijiji 20,” alifafanua.
Aidha, alisema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2013/2014 halmashauri
iliidhinishiwa kutumia sh bilioni 18.125 kwa ajili ya kutoa huduma
mbalimbali ikiwemo mishahara ya watumishi.
Hata hivyo, alisema mapato ya ndani yameongezeka kutoka sh bilioni
1.928 mwaka 2013/2014 hadi kufikia sh bilioni 2.986 kwa mwaka
2014/2015.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment