Home » » Msindai: Lowassa jembe la maendeleo

Msindai: Lowassa jembe la maendeleo

  Aeleza anaunga mkono harakati zake za maendeleo
  Akanusha kuzungumzia masuala ya urais Monduli
Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Mikoa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama hicho mkoani Singida, Mgana Msindai,akiongea na waandishi wa habari jana.
Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mgana Msindai amekanusha vikali madai kuwa amemuunga mkono, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, katika suala la kuwania urais wa mwaka 2015.
Badala yake Msindai ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, amesema anamuunga mkono kwa nguvu zote Lowassa katika juhudi zake za kuwaletea Watanzania maendeleo.

Msindai alitoa ufafanuzi huo jana kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam baada ya kuwapo kwa taarifa kwenye vyombo vya habari zikimkariri kuwa alitoa kauli ya kuunga mkono Lowassa katika mbio za urais.

Alisema siku ya tafrija nyumbani kwa Lowassa, Monduli, alizungumza kama kiongozi kuwa anaunga mkono jitihada za Lowassa katika kuleta maendeleo ya wananchi baada ya kueleza kuwa ameanza safari ya kuwasaidia Watanzania na kuwa ina vikwazo vingi, lakini Mungu ndiye msaada wake.

“Lowassa hajatamka kuwania urais, alichosema ni kuendelea na safari ya kuwasaidia Watanzania katika nyanja za elimu, afya, barabara na mengine, nami nilisema namuunga mkono katika hayo kwa kuwa ni kiongozi hodari mwenye kufanya kwa vitendo na si vinginevyo,” alisema Msindai.

Aidha, alisema anashangazwa na kauli za wenyeviti wa CCM kutoka mikoa mbalimbali kuanza kumshutumu bila ushahidi wa kutosha na kwamba hakuna mahali Lowassa ameeleza kuwania nafasi ya urais.

Alisema amefanya kazi serikalini kwa miaka 28, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kwa miaka mitano, mwenyekiti wa CCM miaka mitatu na Mbunge kwa miaka 15, anafahamu vyema sheria, kanuni na taratibu za serikali na chama na kwamba chama kinaendeshwa kwa vikao na si vinginevyo.

“Lowassa kafanya makubwa mengi ya maendeleo ya Watanzania na hakuna asiyejua, hivyo, mimi kwa niaba ya wenzangu nimemuunga mkono kwenye hilo, lakini baadhi ya watu kwa makusudi wametafsiri kauli hiyo vingine na kuanza kuchafua jina langu,” alisema.

Aidha, alisema wapo waliozusha kuwa ameitwa na Kamati Kuu ya CCM (CC) ili kuhojiwa jambo ambalo si kweli.

Alisema kwa sasa wanajikita katika kujenga chama na si kusaka urais na wakati ukifika kwa mujibu wa sheria na taratibu za chama anayetaka nafasi hiyo atajitokeza na kwamba hawezi kukichafua chama chake na kwenda kinyume cha sheria, kanuni na taratibu.

Msindai alisema amewapa siku saba waliotoa kauli kuwa alitoa kauli ya kumuunga mkono Lowassa katika mbio za urais wakanushe au kutoa vielelezo vya kuthibitisha vinginevyo atawasiliana na chama kwa hatua zaidi za kisheria.

Alisema baadhi ya viongozi waliojiita kuwa ni wenyeviti wa mikoa wa Tanzania Bara na Zanzibar waliotoa taarifa katika vyombo vya habari wakimhusisha na suala hilo hawasemi ukweli.

Taarifa inayodaiwa kuwa ni ya wenyeviti hao ambayo waliitoa kupitia Idara ya Habari (Maelezo) juzi bila kutiwa saini na mmoja wao, ilisema kuwa vyombo vya habari vimemnukuu Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Iringa, Msambatavangu.

Taarifa hiyo ilidai kuwa wao ni viongozi na wajumbe wa Nec, hivyo hawatarajii kukiuka katiba, sheria, kanuni na taratibu zozote zikiwamo za uchaguzi kwa kuwa wanatambua kuwa kumuunga mkono mgombea mtarajiwa si sahihi hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Pia ilidai kuwa wenyeviti hao hawatarajii kuwa chanzo cha kumharibia mgombea yeyote kwa kumsababishia kukosa sifa za kugombea, pia hawatarajiwi kusigina demokrasia ndani ya chama kwa kumbeba mgombea mmoja.

Kulingana na taratibu za uchaguzi Tanzania na kama ilivyoainishwa kwenye Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 mwaka ujao ni wa uchaguzi ambao Rais Jakaya Kikwete atakuwa anamaliza muhula wake wa pili wa miaka mitano.

Tayari kuna makundi mbalimbali ya watu yanatajwa kuwa katika kujipanga kuwania urais mwakani, lakini hadi sasa hakuna ambaye yuko tayari kutamka wazi kuitaka nafasi hiyo miongoni mwa miamba ya CCM inayotajwa kuwa na nia hiyo. 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa