Home » » Watu wasiofahamika wamnyang’anya bunduki Mzee wa miaka 71.

Watu wasiofahamika wamnyang’anya bunduki Mzee wa miaka 71.


Kamanda wa Polisi, mkoa wa Singida, SACP Geofrey Kamwela akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) ofisini kwake.

WATU wasiofahamika idadi na makazi yao,wamevamia nyumba ya Daudi Karata (71) mkulima na mkazi wa kijiji cha Nguamghanga tarafa ya Mgori wilaya ya Singida mkoa wa Singida,na kunyang’anya bunduki aina ya shot gun na risasi zake nne.

Kabla na kufanya unyang’anyi huo,kundi hilo la watu wasiofahamika,lilimkata kata mapanga mzee Karata  sehemu mbalimbali za mwili kwa lengo la kufanikisha azma yao kwa urahisi zaidi.

Kamanda wa Polisi, mkoa wa Singida, SACP Geofrey Kamwela amesema tukio hilo limetokea januari 21 mwaka huu saa tano asubuhi huko katika kijiji cha Nduamghanga tarafa ya Mgori.

Amesema mzee huyo Karata,alipatiwa matibabu katika kituo kidogo cha kutolea huduma za afya kilichoandaliwa kwa muda kijijini hapo.

“Jeshi la polisi linaendelea na msako mkali ili kuwakamata watu hao na kuwafikisha mahakamani.Pia linatoa wito kwa raia wema kutoa taarifa pindi wapatapo taarifa zo zote juu ya tukio hilo”,amesema kamanda Kamwela.

Habari kutoka kijiji hicho cha Nduamghanga,zinadai kwamba baada ya mzee Karata kunyang’anywa bunduki yake shot gun,saa mbili baadaye,kundi la watu zaidi ya 300 wakazi wa kijiji cha Handa wilaya ya Nchemba mkoa wa Dodoma,walivamia kijiji hicho huku wakiwa wamebeba mapanga,rungu,pinde na bunduki moja.

Kundi hilo linadaiwa
kumuuawa mhudumu wa wanyamapori wa kijiji hicho,Athumani Jumanne Mkatapori kwa kumkata kata kwa mapanga.

Kundi hilo linadaiwa lilikuwa linataka kuwakomboa ng’ombe wao 180 waliokamatwa kwa kuchungia ndani ya hifadhi ya akiba ya msitu wa Mgori.


Hata hivyo,kundi hilo,halikuweza kuwapata ng’ombe wao na badala yake likaishia kunyang’anya ng’ombe 68,mbuzi 101,kondoo sita na punda watatu mali ya Abrahamani Mohammed (60) na kutokomea nao kusikojulikana.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa